Ukeketaji na ndoa za utotoni ni janga linalohitaji nguvu za pamoja kulipinga


Ukeketaji na ndoa za utotoni ni janga linalohitaji nguvu za pamoja kulipinga

Ukeketaji au kwa jina lingine tohara kwa wasichana ni utamaduni usio wa kitabibu wa kubadilisha maumbile ya uke wa mwanamke.

Ukeketaji au kwa jina lingine tohara kwa wasichana ni utamaduni usio wa kitabibu wa kubadilisha maumbile ya uke wa mwanamke.

Tohara hufanyika kwa kuondoa sehemu ya juu ya kinembe au kinembe chote, kuondoa kinembe na mashavu ya uke, kuondoa mashavu ya uke halafu kushona sehemu ya uke na kuacha tundu dogo kwa ajili ya kupitisha mkojo na hedhi.

Ukeketaji ni mila inayopingwa katika mataifa mengi duniani ikiwemo Tanzania huku baadhi ya matamko na mikataba ikiitaja mila hiyo kama moja ya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya wasichana na wanawake milioni 200 wamekeketwa duniani, kwenye nchi zenye utamaduni huu. Pia, inakadiriwa kuwa zaidi ya wasichana milioni 3 wako hatarini kukeketwa kila mwaka hii ni kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Tanzania haijasalimika katika janga hili

Tanzania ilipitisha sheria dhidi ya ukeketaji tangu mwaka 1998. Kumekuwa na juhudi binafsi na za pamoja katika kumaliza vitendo hivi, ndani na nje ya mipaka ya nchi. Tangu mwaka 1998, vitendo vya ukeketaji vimepungua na kufika asilimia 10 kutoka asilimia 18.

Japo kuna viashiria vinavyoonyesha matokeo chanya ndani ya miaka ishirini, bado kuna mikoa inayoongoza kwa vitendo vya ukeketaji nchini, mikoa hiyo ni; Manyara (58%), Dodoma (47%), Arusha (41%), Mara (32%) na Singida (31%).

Maswali ya kujiuliza ni kwamba, kwa nini vitendo vinavyosababisha matatizo mengi, tena visivyokuwa na ulazima wowote bado vinaendelezwa katika karne ya 21, miaka ishirini baada ya sheria kupitishwa kuvipinga?

Inakuwaje kuna familia zinaridhia na kushinikiza vitendo vitakavyowaumiza watoto au ndugu zao, na kuwaletea madhara ya kudumu maishani mwao?

Ili kupata majibu ya maswali hayo na mengine kadhaa, timu ya vijana watano wa Kitanzania walijitolea kufunga safari kuzuru katika mikoa iliyoshamiri ukeketaji, waliweza kukutana na kuzungumza na watu mbalimbali, wakiwemo wasichana jasiri wanaopinga ukeketaji na ndoa za utotoni.

Vile vile walikutana na kina mama walioachana na ungariba na sasa wako mstari wa mbele wakihamasisha jamii iachane na ukeketaji. Walizungumza na wazazi, viongozi wa kimila na wa kijamii wanaopinga na wanaokubaliana na utamaduni wa ukeketaji.

“Wakati mwingine wanakuletea mama mjamzito umkekete, wakati wa kujifungua anapata shida sana maana mara nyingi kile kidonda hakijapona halafu anachanika. Saa zingine unakuta yule mtoto anafariki au hata mama na yeye anapoteza damu nyingi anakufa. Yaani kwa kweli anapata maumivu makubwa sana,” anasema mhamasishaji aliyeacha ungariba, Arusha.

Juhudi za kupinga na kutokomeza ukeketaji na ndoa za utotoni zimekumbwa na changamoto nyingi sana, kwa kuwa suala la ukeketaji lina sura nyingi sana. Ni dhahiri kuwa ukeketaji huathiri wasichana na familia zao kwa namna mbalimbali.

“Nilikuta nimezingirwa na watu wamejificha nyuso zao, wakanibeba kwa nguvu wakanipeleka msituni. Nikapiga kelele kweli kuomba msaada, namwomba mama yangu anisaidie lakini hakufanya kitu. Nikawa napiga kelele najaribu kupambana nao nikimbie lakini wapi. Hakuna aliyekuja kunisaidia,” anaeleza Sharon mkazi wa Mara.

“Usiku wa kwanza baada ya kufunga ndoa, ulikuwa mgumu sana kwangu. Yaani sikuwa na hamasa yoyote ya kukutana na mwanaume, niliumia sana ilikuwa vigumu sana kufurahia maisha ya ndoa ikifika kwenye suala hilo,” anasema Anna (sio jina lake halisi) kutoka Singida.

“Nilitamani sana siku ifike niwe na mke wangu. Ile siku ya harusi yetu nilikuwa nasubiri kwa hamu kwamba, leo naenda kuwa na mke wangu na kukamilisha ndoa yetu lakini mambo hayakwenda kama nilivyotarajia. Nilijisikia vibaya kwa kweli maana mwenzangu hata sikumuelewa, ni kama nilikuwa ninamlazimisha, nilijisikia vibaya sana,” anasema mume wa Anna, Singida.

“Eti walikuwa wamepanga nikirudi likizo baada wa wiki mbili wanikekete siku moja halafu kesho yake niolewe. Yaani kweli kabisa?,” anasema Nanyori mkazi wa Arusha.

Kwa upande wa ndoa za utotoni takwimu zinaonyesha kuwa, kila mwaka duniani, wasichana milioni 12 huolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18, idadi hiyo ni sawa sawa na wasichana 23 kila dakika, takribani msichana mmoja kila sekunde 2.

“Niliwaona wababa wawili wamekuja nyumbani kwa mjomba wangu wameleta makreti ya soda na ng’ombe. Kulikuwa na kama shamra shamra hivi, lakini sikujua tunasherehekea nini. Mama akaniambia kuwa wameleta mahari yangu,” anasema Naseko mkazi wa Manyara.

Kwa kuzingatia madhara, changamoto na uelewa mdogo wa suala zima la ukeketaji, kuna umuhimu mkubwa wa kushirikisha mitazamo, uzoefu na mapito ya watu mbalimbali waliokutana na wanaharakati wetu. Ni matarajio yetu kwamba majadiliano haya yataongeza mwanga wa ulewa na kuchochea juhudi za kutokomeza ukeketaji na ndoa za utotoni.