Ukeketaji unavyotumika kama kitegauchumi


Ukeketaji unavyotumika kama kitegauchumi

Sababu zilizotolewa kuchangia kufanyika kwa vitendo vya ukeketaji zinatofautiana kuanzia kwenye utamaduni na kuzingatia maadili yake, shinikizo la kijamii, imani, na ustawi wa msichana au mwanamke.

Ukeketaji umekuwa ni utamaduni unaoshikiliwa na baadhi ya makabila, koo au jamii, kwa muda mrefu sasa.

Ingawa taratibu hutofautiana kutoka kabila moja hadi lingine, sababu kuu inabakia kwenye huo utaratibu wa kufanyia mabadiliko sehemu za siri za mwanamke kupitia utamaduni huo.

Sababu zilizotolewa kuchangia kufanyika kwa vitendo vya ukeketaji zinatofautiana kuanzia kwenye utamaduni na kuzingatia maadili yake, shinikizo la kijamii, imani, na ustawi wa msichana au mwanamke.

Licha ya kuthibitishwa wazi kuwa ukeketaji haufanyiki kwa kuzingatia utaratibu wa kitabibu na zaidi ya hayo, husababisha hatari kubwa kwa afya sambamba na madhara ya mwili, kisaikolojia na kimhemuko.

Sababu nyingine kubwa ambayo haiangaliwi sana ni ukweli kuwa ukeketaji umeonekana kuwa shughuli ya kujikwamua kiuchumi.

Mahojiano yaliyofanyika na mangariba wa zamani yalithibitisha kwamba walikuwa wanafanya vitendo hivyo kama chanzo cha kujipatia riziki, achilia mbali fahari inayohusishwa nayo.

“Wakati wowote bibi yangu alipokuwa akiwakeketa wasichana mbalimbali, familia za wasichana wale zilimletea mbuzi. Mara tu wale mbuzi walipofanikiwa kuzaa, bibi yangu alinipa watoto wa mbuzi. Wakati mwingine wanamletea kuku, kuku wale huwa tunawauza kwa ajili ya kupata fedha kwa matumizi yetu ya kila siku,” anasimulia Hawa kutoka Singida.

“Mangariba pia hupata pesa kupitia shughuli hizi. Tulikuwa tunatoza shilingi 30,000 za Kitanzania (takriban Euro 12) kwa kila msichana uliyemkeketa. Tulipokea pia kondoo na kuku kutoka kwenye familia hizo,” alisema Namaiyani kutoka Arusha.

Bibi Suzan ana umri wa takriban miaka 80. Mwaka 2018 alipelekwa gerezani kwa miezi sita kujishughulisha na ukeketaji. Alizungumza na Doris Mollel na kuelezea jinsi maisha yake yalivyoathiriwa bila chanzo mbadala cha mapato:

“Niliporudi nyumbani kutoka gerezani, nilikuta nyumba yangu imechakaa kutokana na mvua kubwa zilizokuwa zikinyesha. Ilinibidi niende kuishi kwa mwanangu. Sina mtu yeyote wa kunisaidia kuikarabati nyumba yangu na kwa hivyo ninaishi hapa tu. Nilikuwa nategemea shughuli hii ya ukeketaji kama chanzo cha mapato lakini sasa sijui nini kingine cha kufanya.”

Hawa na Namaiyani wameweza kuachana na ukeketaji na kufanya shughuli zingine za kujipatia kipato. Hawa ni mkunga na mkulima mdogo wa mazao, wakati Namaiyani ana biashara yake ndogo ya kutengeneza na kuuza bidhaa za shanga.

Kama tulivyosoma katika matoleo yaliyopita, wasichana ambao hukeketwa wanaandaliwa kuwa wake bora ambao huonwa kuwa wasafi na waaminifu kwa waume zao wa baadaye.

Katika mahojiano yaliyofanyika katika Mkoa wa Mara, ilionekana kuwa wasichana ambao wamekeketwa waliweza kuleta ng'ombe wengi zaidi kama mahari ya ndoa ukilinganisha na wasichana ambao hawajakeketwa.

Sherehe za ukeketaji pia hutoa nafasi kwa watu kufanya biashara zaidi. Ng'ombe ambao watachinjwa kwa ajili ya kulisha watu, mapambo au vitu ambavyo hununuliwa na kwenda kukabidhiwa wasichana waliokeketwa kuashiria utimilifu wa tohara, zawadi, vinywaji na chakula vitalazimika kuandaliwa kwenye sherehe hizo. Katika Mkoa wa Mara, mwezi unaofanyika ukeketaji huitwa "mwezi wa baraka" kwa sababu ya kiasi kikubwa cha pesa kinachotumika na biashara kuingiza faida kutokana na jambo hilo.

Kipunguni Knowledge Centre ni kituo kilicho nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, ni jitihada za makusudi zilizofanywa na Mtanzania, Selemani Bishagazi ambaye alikuwa na lengo la kukabiliana na ukeketaji na ndoa za utotoni kwa kubuni njia mbadala za kiuchumi.

Wakati Neema Ngelime, mmoja wa wanaharakati watano wanaochipukia wa masuala ya ukeketaji, alipotembelea taasisi hiyo alishuhudia shughuli za uchumi na uzoefu wa kubadilishana maarifa.

Mzee Zablon, ambaye ni mzee wa kimila kutoka Tarime, Mkoa wa Mara ambaye tulimsoma katika matoleo yaliyopita, alitoa ardhi kwa kituo hicho bila ya malipo, kwa ajili ya ujenzi wa makazi yatakayokuwa salama kwa walionusurika na wasichana walioko hatarini kukeketwa. Jamii ya Kipunguni ilitaka kuhakikisha kuwa hakuna msichana yeyote anayekeketwa katika eneo lao.

Wanufaika wote katika jamii walilazimika kujitolea kutokomeza ukeketaji na papo hapo walipatiwa ujuzi mpya wa kilimo, ufugaji wa kuku na ng'ombe, ushonaji na usimamizi wa biashara.

Neema alikutana na wasichana na wanawake ambao walikuwa wamedhamiria kuvunja huo utamaduni. Alikutana na Upendo ambaye ni mwathirika wa ukeketaji. Alisimulia jinsi wazazi wake walivyonunua ardhi kutoka kwenye zawadi walizopokea kwenye sherehe yake alipokeketwa.

Akiwa ameamua kuvunja utamaduni huo alimchukua mdogo wake hadi kituo cha polisi ili amuepushe na janga hilo. Upendo sasa ni sehemu ya jamii ya Kipunguni na anaamini kuwa kuwawezesha wanawake kiuchumi pia kutasaidia kutokomeza ukeketaji.

Salome ni mwathirika wa vitendo hivyo, alikeketwa akiwa bado mdogo. Alifikiria kuwakeketa binti zake walipofikia umri sahihi lakini baada ya kufika katika kituo hicho na kusikia kutoka kwa manusura na mangariba wa zamani juu ya athari za ukeketaji, alishawishika kuacha.

Kipunguni Knoweldge Centre ni mfano jitihada zilizoanzishwa na kutekelezwa na wanajamii wenyewe ambao wanaelewa sababu ya kiuchumi inayochangia kuendelea kuwepo kwa vitendo vya ukeketaji. Walikabiliana na jambo hili na hadi 2018, walifanikiwa kufikia lengo lao, ambapo hakukuwa na msichana aliyekeketwa katika jamii ya Kipunguni kwa mwaka 2018.

Ni wazi kuwa, kuna sababu nyingi zinazoendeleza vitendo vya ukeketaji, huku sababu ya kiuchumi ikitajwa kuwa ndiyo mzizi. Juhudi za mtu mmoja, Selemani Bishagazi ziliweza kuileta pamoja jamii katika kuhakikisha kuwa ukeketaji unakomeshwa na unatokomezwa moja kwa moja.

Katika sehemu inayofuata tutasoma juu ya jinsi mtu mmoja mmoja anavyoweza kufanya mabadiliko.