Mchango wa kila mmoja wetu ni muhimu dhidi ya ukeketaji


Mchango wa kila mmoja wetu ni muhimu dhidi ya ukeketaji

Namaiyani na Valerian ni watu ambao wanawakilisha idadi ya watu tofauti, lakini wana jambo moja wanalofanana, wote wanataka jamii isiyokuwa na ukeketaji, isiyo na aina zote za ukatili wa kijinsia. Katika maisha yao ya kila siku, wanaishi kufanya mabadiliko.

Katika safari zao zote, wanaharakati wanaochipukia wa masuala ya ukeketaji na wahamasishaji waligundua kuwa watu binafsi wamekuwa na athari kubwa katika jamii wanazozihudumia.

Wakiendeshwa na shauku ya kutokomeza ukeketaji, wakati mwingine watu hawa hukabiliwa na changamoto kubwa kutoka kwenye jamii zile zile wanazojaribu kuzilinda.

Tumesoma katika toleo lililopita, mafanikio yaliyopatikana kutokana na jitihada za watu tofauti katika mikoa iliyotembelewa na wahamasishaji wetu watano.

Kutoka kwa wanandoa kule Singida ambao waliamua kutumia uzoefu wao kufundisha watu wengine juu ya athari za ukeketaji, hadi kwa manusura wa ukeketaji, mangariba wa zamani na wazee wa jadi ambao kwa njia moja au nyingine wameweka jitihada zao binafsi kwa kukabilian na ukeketaji kutoka kwenye jamii zao.

Katika toleo hili tutaangalia watu wawili ambao hujitofautisha na wengine kwa kufikiria mbali zaidi, hii ikiwa sehemu ya maisha yao ya kila siku katika kuhakikisha Tanzania inaachwa huru dhidi ya vitendo vya ukeketaji.

Wakati wa mazungumzo kati ya Diana Lukumay, mwanaharakati wa masuala ya ukeketaji, na Namaiyani, ambaye ni ngariba wa zamani wa Mkoa wa Arusha, iligundulika kuwa vita dhidi ya ukeketaji ni ngumu na inahitaji mikakati makini na endelevu.

“Wanatuita sisi wazimu na wapotoshaji, kwa sababu ya kupinga vitendo vya ukeketaji. Tunajaribu kufikia wasichana wengi iwezekanavyo lakini rasilimali zetu ni hafifu. Kwa mfano, nina familia inayoniangalia na pia nina mume. Wanaume hawapendi sisi kujiingiza katika utetezi wa haki za wanawake dhidi ya ukeketaji. Kuna wakati inanibidi kutembea zaidi ya kilomita 20 au 30 kusambaza uelewa juu ya athari za ukeketaji.

Kuna watoto ambao hawaendi shuleni. Nimefurahi kutokana na juhudi za hivi karibuni za Serikali watoto wengi wanakwenda shule, lakini wapo wazazi wengine bado wanazuia watoto wao kwenda shule. Kwa mfano, nawafahamu wasichana watatu ambao wangetakiwa kuanza shule ya msingi wakiwa na umri wa miaka 15 lakini baba yao alipokea mahari zao na kuwadanganya.

Nilijitahidi kuzungumza na mama zao na kutafuta njia za kuwaandikisha shuleni kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya kuwazuia wasiolewe. Mmoja wao alisema anaogopa namna muwewe atakavyolichukulia jambo hilo na hivyo nilienda kuongea na waalimu wa shule hiyo.

Tulipanga kwamba mama ampeleke msichana kliniki ya kijijini na mwalimu atakuja kliniki na kuagiza mama amuandikishe msichana shuleni. Halafu, mama ataenda nyumbani akilia na kusema kwamba walimu walimlazimisha binti yao aende shule na hakuna kitu angeweza kufanya juu yake. Angalau kwa njia hiyo asingeingia matatizoni na muwewe na mtoto yule angeenda shule. Kuna wasichana wengi zaidi katika vijiji ambao hawajaandikishwa shule.

Nimeshuhudia wanawake wengi wakipitia machungu. Tunahitaji kuwakomboa wanawake na wasichana. Wao ndiyo kesho yetu. Tunahitaji kufanya hivi zaidi vijijini.”

Kaskazini mwa Mkoa wa Mara, zaidi ya wasichana 2,500 wameokolewa na Kituo cha ATFGM Masanga, kati ya 2008 na 2017, wanawake wengine zaidi ya 400 waliokolewa kufanyiwa ukeketaji 2018.

Valerian ni Ofisa wa program anayefanya kazi katika Kituo cha Masanga. Valerian alizungumza na Rebeca Gyumi, mwanaharakati aliyetembelea Mkoa wa Mara, juu ya uzoefu wake katika kukabiliana na ukeketaji katika eneo hilo:

“Kuna tukio moja ambalo haliwezi kufutika kwenye akili yangu. Inamhusu msichana ambaye alikuwa karibu kutolewa kafara kwa sababu alikuwa na mjamzito kabla ya kukeketwa. Baba yake alifariki wakati huo huo binti huyo alipokuwa mjamzito. Wiki mbili baada ya kuzikwa na wazee walikuwa wamekuja kuhitimisha ibada za mazishi, walisema kwamba baba yake alifariki kwa sababu binti yake alikuwa amepata ujauzito nje ya ndoa na hakuwa amefanyiwa tohara. Walisema yeye ni laana katika familia. Walipanga kumtoa kafara msituni huko Serengeti.

Niliarifiwa juu ya tukio hili na nilikwenda kuuliza msaada kutoka kwa polisi na kwa pamoja tukafuatilia hili. Tuliwakuta msituni wakikaribia kumtoa sadaka msichana ambaye alikuwa hajitambui wakati huo. Tulimpeleka hospitalini na alipopata fahamu alituambia yote yaliyokuwa yametokea.

Kwa bahati mbaya, hatukuwahi kumwona mzee huyo ambaye alikuwa amepanga ufanyikaji wa jambo hilo la kumtoa msichana huyo sadaka, na hata mama yake alikuwa alitoweka.

Kuna matukio mengi ambapo nimehatarisha maisha yangu lakini naamini yote yalistahili kwa sababu siwezi kusimama kuona mtoto ameumizwa kwa njia yoyote. Naamini jambo la muhimu zaidi ni kubadili mawazo ya watu kupitia elimu na kujenga uwezo.

Nakumbuka baada ya kuhitimu na niliamua kuja Mara kutoka Dar es salaam, nakumbuka jinsi marafiki na wenzangu walivyonikatisha tamaa. Hawakudhani kama lilikuwa wazo nzuri kuja na kukabiliana na masuala ambayo yamo katika utamaduni wa watu kwa mamia ya miaka. Lakini sikuvunjika moyo na sijutii kuja hapa,  ”alihitimisha Valerian.

Namaiyani na Valerian ni watu ambao wanawakilisha idadi ya watu tofauti, lakini wana jambo moja wanalofanana, wote wanataka jamii isiyokuwa na ukeketaji, isiyo na aina zote za ukatili wa kijinsia. Katika maisha yao ya kila siku, wanaishi kufanya mabadiliko.