Tume ya kurekebisha Sheria Zanzibar yajivunia mafanikio

Muktasari:

Wakati tukiangazia miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ni wazi kwamba kuna mafanikio mengi yameweza kupatikana ndani ya tume hiyo ambayo si vibaya kuyataja kwa japo kwa uchache wake, ilikuwa ni moja ya kuelezea mema yaliofanywa na tume hiyo chini ya Marais mbalimbali ikiwa kwa sasa ni Rais Dk. Ali Mohamed Shein.

 

Tume ya kurekebisha Sheria Zanzibar ni taasisi ya kiSheria Zanzibar ambayo inafanya kazi kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi lengo likiwa ni kuhakikisha maslahi ya jamii na umma kwa ujumla yanapatikana. Tume ya kurekebisha Sheria Zanzibar imeanzishwa rasmi mwaka 1986 chini ya Sheria namba 16, ambapo kazi kuu ni kuhakikisha inafanya marekebisho ya Sheria za Zanzibar ambazo zimetungwa na baraza la wawakilishi pale inapohitaji kufanya hivyo.

Licha ya tume hiyo kuwa na nguvu katika utendaji wa kazi zake lakini kwa muundo wa sasa wa Serikali ipo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria ya Zanzibar ambao ndiyo wasimamizi wakuu katika utendaji wa tume hiyo. Wakati tukiangazia miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ni wazi kwamba kuna mafanikio mengi yameweza kupatikana ndani ya tume hiyo ambayo si vibaya kuyataja kwa japo kwa uchache wake, ilikuwa ni moja ya kuelezea mema yaliofanywa na tume hiyo chini ya Marais mbalimbali ikiwa kwa sasa ni Rais Dk. Ali Mohamed Shein.

Kazi za tume

Katibu wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Kubingwa Mashaka Simba alisema jukumu kuu la tume ya kurekebisha Sheria Zanzibar, ni kufanya marekebisho ya baadhi ya Sheria ambazo zinaonekana kuhitaji kufanyiwa marekebisho kwa mujibu wa matumizi au maslahi ya wakati husika. Katika kipindi cha miaka tisa, tume imefanikiwa kupitia Sheria 37 kwa lengo la kuzifanyia maboresho kwa mujibu wa matumizi ya wakati husika, ambapo kati ya hizo Sheria 22, tayari zimeridhiwa na Serikali Kuu na kuanza kutumika katika utoaji wa huduma kwa jamii.

Lengo kuu la kufanyika kwa marekebisho hayo ni kuhakikisha Sheria husika zinapunguza chan-gamoto mbalimbali za kiSheria zinazowakabili wananchi katika upatikanaji wa haki za msingi. Miongoni mwa Sheria ambazo zimefanyiwa marekebisho ni Sheria ya adhabu, Sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai na Sheria ya ushahidi . Kwa mujibu wa Sheria ya ushahidi ya sasa, pamoja na mambo mengine inatambua ushahidi wa mtoto mdogo bila ya kuungwa mkono na ushahidi wa mtu mzima. Sheria hii imesaidia sana kupunguza changamoto ya ushahidi hasa katika makosa ya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto. Simba alisema licha ya hatua hiyo lakini bado wanaendelea na mchakato wa kuangalia au kusikiliza wanajamii na Serikali kwa ujumla juu ya Sheria gani inahitaji kufanyiwa marekebisho ili kutoa haki kwa mujibu wa wakati uliopo. Hata hivyo tume wakati wa kufanya mapitio ya Sheria inawashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo mahakimu, mawakili wa kujitegemea, wanasheria wa Serikali, walimu, wanafunzi, viongozi wa dini, askari polisi, asasi za kiraia ikiwemo wanasheria wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS).

Kuimarika utendaji kazi wa tume

Katibu Simba alisema licha ya tume hiyo kuanza kazi katika vipindi mbalimbali vya uongozi wa Rais waliopita, lakini kuanzia kipindi cha 2010 hadi 2019 chini ya uongozi wa Rais Dkt. Shein Tume hiyo imezidi kuimarika kiutendaji. Simba alisema kabla ya 2010, tume hiyo ilikuwa na watendaji wachache tu wakiongozwa na mwenyekiti tu, lakini baada ya kuingia madarakani Dkt. Shein aliendelea kuiboresha tume hiyo kwa kuchagua safu kubwa ya uongozi ikiwamo katibu, makamishna, wanaSheria pamoja na watendaji wengine mbalimbali. Alisema ongezeko la wafanyakazi hao kwa zaidi ya asilimia 50, ni moja ya mambo ambayo yameifanya tume hiyo kuwa na uhai zaidi katika utekelezaji wa majukumu yake kwa jamii. Simba alisema mbali ya hatua hiyo maamuzi ya Serikali inayoongozwa na Dkt. Shein kuhakikisha tume inakuwa na ofisi yake ndogo Pemba itakayosaidia ukuaji wa mafanikio kwa tume hiyo kutokana na hivi sasa pande zote mbili hutoa huduma bila ya usumbufu.

Upatikanaji Fedha

Simba anasema moja ya mambo ambayo yamewapa matumaini makubwa viongozi na watendaji wa tume hiyo ni kuongezeka kwa bajeti ya kifedha za uendeshaji wa tume hiyo. Alisema kasi hiyo imeonekana kukua zaidi ijapokuwa Serikali kukabiliwa na shughuli nyingi za maendeleo katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali haikuwaacha nyuma kwa kuwaongezea bajeti yao kutoka shilingi milioni 700 mpaka Tsh milioni 770.

Ushirikiano wa tume

Katibu Simba anasema licha ya tume hiyo kwa na mashirikiano na taasisi mbali mbali za kiSheria hapa Zanzibar, lakini pia imetanua wigo wake katika ushirikiano wa kiSheria nje ya nchi ambao umekuwa na mchango mkubwa katika uimarishaji shu-ghuli za tume hiyo. Alisema miongoni mwa jumuiya ambazo tume hiyo wameungana nazo ni Umoja wa Tume za Kurekebisha Sheria za Afrika Mashariki na Kusini (alraesa) na Umoja wa Tume za Kurekebi-sha Sheria za nchi wanachama wa jumuiya ya Madola (CALRAs). Alisema katika kuungwa mkono Serikali ya Zanzibar imekuwa ikiwalipia ada za uanachama wa Jumuiya hizo kila kipindi cha ulipaji ada, pamoja na kuwalipia na kuwapa ruhusa ya kushiriki vikao mbali mbali vinavyoandaliwa na Jumuiya hizo.