Mafanikio ya ZFDA ndani ya miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar

Muktasari:

Wakala wa chakula dawa na vipodozi ZFDA katika  kufikia miaka 56 ya mapinduzi imeweza kupata mafanikio makubwa kama kuongezeka kwa idadi ya biashara na bidhaa zilizosajiliwa, kupungua kwa bidhaa feki na zilizomaliza muda wake wa matumizi na utoaji wa vibali umeongezeka hali inayoonyesha kwamba wananchi wamepata uelewa wa kutosha juu ya taratibu za uuzaji na usambazaji wa bidhaa zinazodhibitiwa na ZFDA.

Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi (ZFDA) ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Afya ya Zanzibar iliyoanzishwa chini ya kifungu nambari 3(1) cha sheria nambari 2:2006 na marekebisho yake Sheria namba 3:2017 ya Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi. Wakala ilianza kufanya kazi zake mnamo mwezi Januari mwaka 2007.

Mkurugenzi Mtendaji ndie mkuu na msimamizi wa Wakala (ZFDA) ambae atawajibika kuwasilisha Ripoti zote za taasisi katika Bodi ya Ushauri ya ZFDA, ambapo Bodi hiyo ya ushauri itawajibika kuwasilisha ripoti hizo kwa Waziri mwenye dhamana ya mambo ya Afya Zanzibar.

Bodi ya Ushauri inaundwa na Mwenyekiti ambaye ameteuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyeiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Katibu wa Bodi ya Ushauri ambaye ni Mkurugezi Mtendaji wa ZFDA ambaye pia ameteuliwa na Rais wa Zanzibar na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ambao wameteuliwa na Waziri wa Afya zanzibar kutoka katika taasisi za Serikali pamoja na taasisi binafsi.

Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi katika kuleta ufanisi wa kazi za kila siku ina idara zifuatazo:-

  • Idara ya Huduma za Wakala,
  • Idara ya Ubora na Usalama wa chakula,
  • Idara ya Dawa na Vipodozi na
  • Idara ya Huduma za Maabara.

Jukumu la ZFDA ni kulinda na kuimarisha Afya za Wananchi wa Zanzibar katika kudhibiti ubora na usalama wa chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi. Jukumu hili linafikiwa kwa kuhakikisha kwamba bidhaa zinachunguzwa katika maabara ya ZFDA kabla ya kuruhusiwa kuingia na kutoka ndani ya Zanzibar.

Aidha ZFDA inafanya kazi ya ukaguzi na usajili kwa majengo na sehemu zote ambazo zinashughulika na uzalishaji, uhifadhi, uuzwaji na ufungashaji wa bidhaa ambazo ZFDA inazisimamia. Mfano wa majengo ambayo ZFDA inayakagua na kuyasimamia ni viwanda, migahawa, bekari, mabucha, vioksi, maduka ya chakula, maduka ya dawa za binadamu na mifugo, maduka ya vifaa tiba, gari za kusafirishia chakula, mashine za kusagia nafaka na maduka ya vipodozi.

Makala hii inalenga kuonyesha jinsi gani miaka 56 ya mapinduzi pamoja na matunda ya Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar  yamesaidia kufikia lengo hilo la ZFDA na pia kutoa pongezi na shukrani za dhati kwa Raisi wa Zanzibar na Serikali kwa ujumla kwa kuweka sera na sheria madhubuti kwa kupitia ilani ya chama cha mapinduzi (CCM) na kuhakikisha inaimarisha Afya Bora kwa wananchi wake kwa kutumia bidhaa za chakula, dawa na vipodozi ambazo ni salama kwa matumizi ya binaadam.ili kufikia dhamira njema ya mapinduzi ya Zanzibar.

 

Wakala wa chakula dawa na vipodozi ZFDA katika  kufikia miaka 56 ya mapinduzi imeweza kupata mafanikio makubwa kama kuongezeka kwa idadi ya biashara na bidhaa zilizosajiliwa, kupungua kwa bidhaa feki na zilizomaliza muda wake wa matumizi na utoaji wa vibali umeongezeka hali inayoonyesha kwamba wananchi wamepata uelewa wa kutosha juu ya taratibu za uuzaji na usambazaji wa bidhaa zinazodhibitiwa na ZFDA.

Mafanikio ambayo ZFDA imeyapata chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufikia miaka 56 ya mapinduzi ya Zanzibar ni kama ifuatavyo:-

  1. Mabadiliko ya sheria.

Mabadiliko ya sheria kutoka Bodi ya Chakula na Dawa na kuwa Wakala wa Chakula na Dawa. Mabadiliko hayo yalifanyika mnamo mwaka 2017 ambapo sheria nambari 3 ya mabadiliko ya sheria nambari 2:2006 ya mwanzo ya Bodi ya Chakula na Dawa ilipitishwa kupitia chombo cha kutunga sheria yaani Baraza la Wawakilishi na kutiwa saini na Raisi wa Zanzibar. Mabadiliko hayo ya sheria yameipa nguvu zaidi za kisheria taasisi ya ZFDA katika kutekeleza kazi zake za kila siku.

Pia Katika kuhakikisha tunatimiza majukumu yetu ZFDA inashirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi katika kuhakikisha ubora na usalama wa bidhaa hizo. Katika kufanikisha ushirikiano huo, ZFDA inashirikiana na Baraza la Wawakilishi ambalo ndio chombo cha kutunga sheria za Zanzibar ikiwemo Sheria ya Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi. Aidha wakala inawashirikisha wajumbe wa baraza hilo katika ukaguzi wa majengo wa  ndani  na nje ya Zanzibar ili kuongeza wigo wa kazi zetu. Mfano wa ukaguzi uliowashirikisha wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni pamoja na ule uliofanyika katika jijini Dar-es-Salaam  pamoja na wa viwanda vya nje ya Tanzania.

 

  1. Kupata ruzuku kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

ZFDA kupitia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kufikia mapinduzi matukufu ya Zanzibar chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt.  Ali Mohamed Shein inapata msaada  mkubwa ambao unawashirikisha  viongozi wa juu wa Serikali, mawaziri na watendaji  wote kwa ujumla. Aidha wakala imepata  kutoka serikalini  ruzuku licha ya kuwa inakusanya mapato yake yenyewe na kuruhusiwa kutumia baadhi ya makusanyo yake.

 

  1. Kuongezeka kwa wataalam

Katika kufikia malengo, ZFDA kufikia miaka 56 ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar imepata jumla ya wataalamu 70 kuanzia 2010 hadi 2019. Ili wataalam hao wazidi kufanya kazi kwa kupatikana weledi katika majukumu yao ya kila siku, hivyo basi wakala unaendelea kupata wataalam siku hadi siku ili kuendelea kudumisha usalama wa chakula dawa na vipodozi katika jamii kama inavoeleza ilani ya chama cha mapinduzi.

  1. Kuboresha kazi za kitaalamu kwa vitengo (Technical Working Group’s)(TWG’s) vitengo hivyo ni kama vifuatavyo:-
  • GMP-Good manufacturing practice (uzalishaji bora viwandani)
  • IMS –Information management unit (mfumo wa kielekroniki)
  • QMS-Quality management system (mfumo wa utoaji huduma bora kwa wateja)
  • PV-Pharmacovigilance (ufuatiliaji wa athari za dawa )
  • CT-Clinical Trial(majaribio ya dawa kabla ya matumizi)
  • MD-Medical Devises (vifaa tiba)
  • PMS-Post Market Surveillance (ufuatiliaji wa dawa sokoni)
  1. Kupata ithibati ya kimataifa (ISO 9001:2015 Certification)

ZFDA inafanya kazi zake kwa kufuata miongozo ya kitaifa na kimataifa kama vile mfumo wa utoaji huduma bora kwa wateja na vile vile imeweza kupata ithibati ya kimatifa kwa kutekeleza kiwango cha ISO 9001:2015. 

  1. Kutegemea kupata ithibati ya kimataifa ya utoaji huduma bora za maabara (Accreditation)ISO:17025:2017.

 

  1. Ununuzi wa vifaa vya Maabara. Mpaka kufikia miaka 56 ya mapinduzi ya Zanzibar, wakala imepata vifaa vipya na vya kisasa vya maabara kwa kupitia wahisani wa kimaendeleo ili kuweza kufikia azma ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar, maabara hiyo iweze kufanya kazi kitaalam zaidi na kwa weledi, vifaa hivyo ni kama vifuatavyo:-
  • HPLC-(high performance liquid chromatograph) ni kifaa inachotumika kuchanganua,Kutambua na kupima kiwango cha aina ya chemicali iliyokuwemokatika mchanganyiko.
  • Vicam-inapima sumu kuvu (unyevu nyevu)
  • Incubator-kuotesha vijidudu kwa ajili
  • Autoclave-inatumika kwa ajili uua vijidudu
  • Oven –kupima unyevunyevu katika sampuli
  • Bio safety-kifaa kinachotumika kuzuia sumu isisambae
  • Fume-hood–kifaa inachozuia gesi za chemicali zisambae.

 

  1. Ununuzi wa gari na vyombo vya usafiri kwa ajili ya ukaguzi,

jumla ya gari tano (5) zimenunuliwa ambapo gari tatu ni ufadhili kutoka kwa mhisani wa kimaendeleo Global Fund (GF) na gari mbili (2) zilizonunuliwa na afisi ya wakala wa Chakula na Dawa.

  1. Mashirikiano na jumuiya mbalimbali za kimataifa (EAC/SADC/ICDRA). Katika kufanikisha kazi za ZFDA ni vyema kuimarisha mahusiano na jumuiya mbalimbali za kikanda, kitaifa na kimataifa. Hivyo basi ZFDA kupitia kitengo chake cha mashirikiano na jumuiya hizo kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na nyinginezo, imeweza kupiga hatua za pamoja, kwa mfano kuanzishwa kwa ukaguzi na usajili wa pamoja wa dawa kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika Mashariki ili kuweza kuwa na mfumo na viwango vya pamoja.
  2. Ujenzi wa  Jengo jipya la ofisi na maabara ya kisasa ya ZFDA. Katika kufikia miaka 56 ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar Serikali ya Mapinduzi inahakikisha kwamba ZFDA inajenga jengo zuri ambalo litakuwa chachu ya maendeleo kwa ZFDA na wananchi kiujumla jengo hilo ni ofisi na maabara ya kisasa ambalo dhamira ya mapinduzi ya Zanzibar matukufu kutoa huduma nzuri kwa wananchi wake. Jengo hilo ambalo liko katika hatua  nzuri za ujenzi linatarajiwa kutumia shilingi za kitanzia billioni mbili na millioni mia moja (Sh2,105,683,863) fedha ambazo zimetolewa na Serikali kwa asilimia mia moja. Ujenzi huo unategemea kukamilika mnamo mwezi Novemba  2020 .
  3. Kuboresha ofisi za ZFDA Pemba. Kupitia mapinduzi matukufu ya  Zanzibar, ZFDA pia ina lengo  la kuboresha ofisi zake Pemba ili kufikia dhamira nzuri ya kiongozi wetu hayat sheikh Abeid Aman Karume Kwa kuwapatia vifaa mbalimbali ikiwemo gari na vifaa vya ofisi.

 

Licha ya mafanikio yaliyopatikana lakini bado kuna changamoto mbalimbali ikiwemo wafanyabiashara kughushi nyaraka za kuingiza bidhaa ndani ya Zanzibar, uwepo wa bandari bubu jambo ambalo linahatarisha ubora na usalama wa bidhaa zinazoingia Zanzibar.

Aidha, katika kutatua changamoto ZFDA inadhibiti bidhaa zisizofaa kwa matumizi ya biaadamu kwa kuziteketeza au kuzirudisha katika nchi zilizotoka. Zoezi hili hufanyika kwa mujibu wa Sheria ambapo muombaji hupewa kibali cha kuteketeza na gharama za uteketezaji hutolewa na mfanyabiashara mwenyewe, zoezi hilo husimamiwa na maofisa kutoka taasisi mbalimbali kama vile vyombo vya ulinzi na usalama, manispaa, halmashauri, sheha wa shehia husika, idara ya mazingira, waandishi wa habari na mfanyabiashara mwenyewe na kwa upande mwengine mfanyabiashara hulazimika kurudisha bihaa hiyo katika nchi iliyotoka kwa gharama zake mwenyewe.  

Kwa kupitia vikao maalum vijulikanavyo kama bango kitita (BK) ambavyo mwenyekiti wake ni Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein katika kujadili masuala mbalimbali ya kimaendeleo  pamoja na  fursa zilizopo na mipango mbalimbali  kwa ajili ya kuibua changamoto zinazozikabili taasisi mbalimbali za serikali ikiwemo ZFDA na kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.

Aidha, kufikia miaka 56 ya mapinduzi ZFDA inashirikiana na Waziri wa Afya katika kupanga mipango na kuelezea majukumu yetu ambayo tunayatekeleza kwa kuthibiti ubora na usalama wa chakula, dawa na vipodozi. Hivyo basi ZFDA inashirikiana na waziri ili kupanga mipango ya kimaendeleo kwa kufikia matunda ya mapinduzi ili wananchi wapate bidhaa bora na salama.            

Vile vile, ZFDA inashirikiana na wizara tofauti ikiwemo wizara ya Biashara na viwanda, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Nchi, Afisi ya Rais Tawala za Mikoa Idara Maalum na vikosi vya SMZ, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara inayoshughulikia mambo ya Muungano na Mazingira pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Aidha, katika kuadhimisha miaka 56 ya mapinduzi ya Zanzibar ZFDA pia ina mashirikiano na mashirika binafsi na taasisi za kimaendeleo ili kufikia malengo iliyojiwekea. Kutokana na sera nzuri za mapinduzi matukufu ya Zanzibar na mashirikiano ya Serikali, ZFDA imepata misaada kutoka kwa wafadhili wa kimaendeleo mbalimbali duniani ikiwemo EAC, GF na  WHO.

Hivyo basi ZFDA inatoa  pongezi za dhati kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutimiza miaka 56 ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar tangu yalipotokea Januari 12, 1964 .