Ujenzi Uwanja wa Mao Tse Tung ni moja ya matunda ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar

Muktasari:

Harakati za Dk. Shein zilifanikiwa kuzaa matunda ambapo hivi sasa uwanja huo uliojengwa na kampuni kutoka chini ya usimamizi wa serikali ya Mapinduzi tayari umekamilika na hivi sasa viwanja vya Mao vimekuwa vikitumika katika michezo mbalimbali ikiwamo ligi kuu ya Zanzibar.

Sekta ya michezo ni moja ya sekta muhimu sana katika utawala wowote duniani, kutokana na kuwa ni sehemu ya burudani, furaha, ushirikiano, umoja, kudumisha amani baadhi ya wakati huwa ni fursa ya upatikanaji wa ajira kwa vijana.

Zanzibar kama zilivyo nchi nyingine duniani imekuwa ikichukua jitiahada mbalimbali za kuhakikisha sekta ya michezo inakua kwa kasi zaidi ili kufikia hatua ya malengo tuliyoyaeleza hapo juu.

Pamoja na sekta ya michezo Zanzibar kuwepo katika miaka mingi ya nyuma lakini ni wazi kwamba katika kipindi cha miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar sekta hiyo imeonekana kukuwa kwa kasi zaidi kutokana na viongozi kuthamini, kujali na kuwa na mapenzi ya dhati kwa wananchi wao.

Licha ya kuwepo mafanikio mengi yaliopatikana katika sekta ya michezo katika kipindi cha miaka 56 ya Mapinduzi lakini katika makala haya tutaangalia mafanikio kwa upande wa ujenzi wa uwanja wa Mao Tse Tung Mjini Unguja. Ujenzi wa uwanja wa Mao Tse Tung ambao umejengwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa mashirikiano na serikali ya watu wa China lengo kuu ni kuurejeshea hadhi yake, kwani ni moja ya viwanja ambavyo vimebeba historia kubwa sana katika visiwa vya Zanzibar pamoja na nchi ya China.

Historia inaonyesha kuwa mashindano ya kwanza ya Afrika Mashariki Gossage, ambayo hivi sasa yanajulikana kwa jina la Chalenji yalifanyika kwenye uwanja wa Mao Tse-tung mwaka 1949, wakati huo uwanja huo ukijulikana kwa jina la ‘Seyyid Khalifa Sports Ground’. Katika miaka hiyo kiwanja hicho kilionekana kutumika kwa ajili ya mashindano mbalimbali ikiwamo ligi kuu, central, madaraja ya chini, daraja za kwanza pamoja na mashindano mengine ya kirafiki.

Kasi ya matumizi ya uwanja wa Mao ilipungua katika miaka ya 2000, baada ya kiwanja hicho kuanza kuharikibika pamoja na kupoteza haiba nzuri ya kuvutia kwa wachezaji, wadau pamoja na wanamichezo mbalimbali. Licha ya awamu mbalimbali za uongozi kuwa na lengo la kuimarisha uwanja huo, lakini kasi ya uimarishaji hadi kufikia kukamilika kwake ilifanyika katika kipindi cha miaka tisa ya uongozi wa Dk Ali Mohamed Shein.

Harakati za Dk. Shein zilifanikiwa kuzaa matunda ambapo hivi sasa uwanja huo uliojengwa na kampuni kutoka chini ya usimamizi wa serikali ya Mapinduzi tayari umekamilika na hivi sasa viwanja vya Mao vimekuwa vikitumika katika michezo mbalimbali ikiwamo ligi kuu ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Omar Hassan alieleza kuwa jumla ya gharama zote za mradi zilikuwa ni Tsh Bilioni 15 ambapo Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China walitoa msaada wa Tsh Bilioni 11.

Alisema kuwa mradi huo ulikuwa na maeneo ambayo yaligharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na maeneo mengine yaligharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo mpaka sasa fedha zote zimelipwa na hakuna deni lolote linalodaiwa.

Aliongeza kuwa mradi huo ulianza rasmi tarehe 3 Machi 2017 na ulitakiwa ukamilike mwishoni wa mwezi wa Mei, 2018 kwa kazi zile zilizomo kwenye makubaliano na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. Alieleza kuwa hata hivyo, baada ya kuangalia kwa makini ikaonekana kwamba kuna haja kubwa ya kumalizia maeneo yote ya uwanja ili uwanja upendeze zaidi hasa maeneo ya ukuta pembezoni mwa uwanja kwa kujaza zege nyengine.

Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa kupitia mahitaji hayo, ndipo kukapelekea kuchelewa kwa ujenzi huo kwa muda wa miezi mitatu na hadi ilipofika mwezi Agosti, 2018 ambapo kwa msaada wa Serikali ya China zilikuwa zimekamilika na kufikia Novemba 2018 kazi zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nazo zilikamilika.