Shirika la Restless Development linavyosisitiza elimu dhidi ya ukeketaji

Muktasari:

“Vile vile wanawake wengi ambao hawajasoma ndiyo wanaonyanyasika dhidi ya ukeketaji na pia huonekana kutokuwa na mchango wa kiuchumi hivyo huishi maisha ya kimaskini na kuendelea kunyanyaswa. Kutokana na hali hiyo, ukeketaji unagusa sehemu zote mbili kwenye haki ya afya ya uzazi na ukatili wa kijinsia,” Bateyunga.

Utafiti mwingi uliofanywa umeelezea vitendo vya ukeketaji kuwa ni utamaduni ulioota mizizi nchini.

Utamaduni huu wa ukeketaji umekuwa ukirithiwa kutoka kizazi hadi kizazi, huku ukitumika kama njia ya kuwaandaa watoto wa kike kuelekea utu uzima.

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na jitihada mbalimbali zinazofanywa kutokomeza tatizo la ukeketaji ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Moja ya jitihada hizo ni kuwapo kwa mikataba mbalimbali ya kimataifa na sheria zinazoshughulikia ukeketaji. Hata hivyo, bado vitendo hivi vimeendelea kutamalaki.

Pengine wanaharakati, mashirika yasiyo ya kIserikali, vyombo ya ulinzi na usalama na Serikali kwa pamoja  vimesahau au havijaweza kutilia mkazo suala la ubadilishaji mitazamo ya watu juu ya ukeketaji.

Restless ina harakati za kubadili mitazamo Ili kubadili mitazamo hii, elimu inahitajika. Na hiyo ndiyo kazi inayofanywa na Shirika la Restless Development, ambalo limejikita katika uelimishaji jamii kuhusiana na madhara ya ukeketaji na sheria zinazosimamia jambo hilo.

Ofisa mwandamizi wa mradi wa Tutimize Ahadi unaoratibiwa shirika hilo, Sima Bateyunga anasema ukeketaji ni kile kitendo kinachohusisha kukata au kuharibu sehemu ya uke (kinembe) kwa njia zisizokuwa za kitabibu.

Anasema sababu za ukeketaji zimegawanywa katika makundi mawili; ambazo ni sababu za kijamii na kiuchumi.

“Nikianza na sababu za kijamii, hapa tunazungumzia utamaduni wa eneo husika, ambapo jamii nyingi zinazofanya ukeketaji huamini kuwa, tendo hilo anapofanyiwa mwanamke humpa heshima. Achilia mbali heshima, mwanamke aliyekeketwa ni rahisi kuchumbiwa na kuolewa kwani hata baadhi ya wanaume huona fahari kuoa mwanamke wa namna hiyo,’’ anasema.

Anaongeza: “Pia, jamii hizo huamini kukeketa humuondolea mwanamke hamu ya kujamiiana na humkinga na maradhi. Ukeketaji katika jamii hizo huwa ni sherehe kubwa ya kumuandaa msichana au mtoto wa kike kuelekea utu uzima.

Kuhusu sababu za kiuchumi, anasema jamii zinazotekeleza utamaduni huu huona kuwa njia pekee ya kuongeza au kukuza uchumi wa familia ni kuozesha binti aliyekeketwa, kwani mahari ya binti aliyekeketwa huwa kubwa kuliko yule asiyekeketwa.

‘’Wanafamilia nao hupata zawadi mbalimbali katika sherehe za ukeketaji. Mangariba nao huendesha maisha yao kwa kukeketa na ikitokea ngariba anasifiwa kwa kukeketa vizuri ndani ya muda mfupi hupendelewa zaidi na wale wanaotaka kuwakeketa mabinti zao,” anafafanua.

Madhara ya ukeketaji

Bateyunga anasema ukeketaji sio tu ni ukatili dhidi ya watoto wa kike, lakini pia huambatana na madhara mbalimbali.

Kwa mfano, binti aliyekeketwa anakuwa katika hatari ya kupoteza maisha kwa sababu ya kupoteza damu nyingi kutoka kwenye jeraha alilolipata, hupunguziwa hamu ya kujamiiana na hivyo kukosa kufurahia tendo hilo na hupata msongo wa mawazo.

Anasema ukeketaji pia husababisha kwa kiasi kikubwa vifo vitokanavyo na uzazi, maambukizi, matatizo ya fistula na kuzaliwa kwa watoto njiti.

Nafasi ya Shirika la Restless katika kupinga ukeketaji

Bateyunga anasema Shirika la Restless Development linaendesha mradi unaojulikana “Tutimize Ahadi” unaolenga katika kufuatilia ahadi zilizowekwa na serikali kwenye masuala ya afya ya uzazi na ukatili wa kijinsia ambapo, ukeketaji kulingana na Shirika la Afya ulimwenguni (WHO) unahusishwa na haki za afya ya uzazi na ukatili wa kijinsia.

“Wanawake waliokeketwa baada ya jando wengi wao huwa wanaolewa na tunafahamu kuwa msichana akiolewa katika umri mdogo anakosa nafasi ya kuendelea na shule, pia ana uwezekano mkubwa wa kufariki wakati wa kujifungua kwa maana wengi wao wanaolewa wakiwa wadogo kabla hata viungo vya uzazi havijakomaa,” anaeleza.

Anasema shughuli kubwa inayofanywa katika mradi huo ni kuelimisha jamii kuhusiana na ukeketaji hususan madhara yake.

“Vile vile wanawake wengi ambao hawajasoma ndiyo wanaonyanyasika dhidi ya ukeketaji na pia huonekana kutokuwa na mchango wa kiuchumi hivyo huishi maisha ya kimaskini na kuendelea kunyanyaswa. Kutokana na hali hiyo, ukeketaji unagusa sehemu zote mbili kwenye haki ya afya ya uzazi na ukatili wa kijinsia,” anasema Bateyunga.

Hali ilivyo nchini Tanzania

“Kutokana na  Utafiti wa Demografia na Afya mwaka 2015/16, inaonekana kuwa asilimia 40 ya wanawake wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 49 wanafanyiwa ukatili wa kimwili tangu wakiwa na umri wa miaka 15,’’ anasema.

‘’Utafiti huo unaenda mbali zaidi na kuthibitisha kuwa, asilimia 10 ya wanawake wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 49 wamefanyiwa ukeketaji, ambapo kati ya hao asilimia 35 wamefanyiwa ukeketaji kabla ya kufikisha mwaka mmoja.’’

Pia, maeneo ya vijijini yameonekana kuongoza kwa vitendo hivi vya ukeketaji ambapo ni asilimia 13 wakati mijini ni asilimia 5 tu.

Mafanikio yaliyofikiwa na Restless Development

Anasema: ‘’Kwanza kabisa ile hali ya kukubalika kwetu sisi ni mafanikio makubwa sana. Serikali imekubali kushirikiana na sisi na tumekuwa tukifika hadi kwenye mikutano mbalimbali inayofanywa katika ngazi ya vijiji chini ya viongozi wa Serikali za mitaa.’’

Anasema shirika lao linafanya kazi katika mikoa ya Iringa, Dodoma, Ruvuma na Dar es Salaam, huku likitumia wigo mpana wa mtandao wa vyombo vya habari hapa nchini kufikisha elimu kwa Tanzania nzima.

Maadhimisho ya kimataifa kupinga ukekektaji Anasema wakati leo dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji, shirika lao limeamua kushiriki kwa kusambaza uelewa juu ya athari za ukeketaji ‘’ Pia,  kuwasihi kutoa taarifa pale ambapo wanakumbana na vitendo hivyo katika mamlaka husika, uelewa kuhusu sheria zinazosimamia masuala ya ukeketaji na adhabu ambazo mtu atakabaliana nazo akigundulika anaendelea na ukeketaji,” anasema.

Maeneo ya kuongeza nguvu

Kwa mujibu wa Bateyunga, maeneo ambayo nguvu zaidi inahitajika ni vijijini kwa sababu elimu haifiki inavyotakiwa. Mijini anasema kuna fursa nyingi za watu kupata taarifa kupitia vyombo kama redio, magazeti, televisheni, intaneti, lakini vijijini hakuna nafasi hiyo na huko ndiko kulikoshamiri vitendo hivyo.

Ujumbe

Bateyunga anasema ukeketaji ni dhuluma kwa  mtu na hilo linaonekana   kupitia vifo mbalimbali vitokanavyo na ukeketaji na madhara mengine mengi.

‘’Jamii iachane na masuala ya ukeketaji kwa sababu hayana tija kwa vizazi vyetu vya sasa na hata baadaye. Pia, watu wanapoona vitendo hivi vinaendelea kutokea watoe taarifa katika mamlaka husika ili sheria ichukue mkondo wake,’’ anaiasa jamii.