Usimamiaji wa sheria, ubadilishaji wa mitazamo ndiyo silaha dhidi ya ukeketaji


Usimamiaji wa sheria, ubadilishaji wa mitazamo ndiyo silaha dhidi ya ukeketaji

Kulingana na utafiti wa demografia (Demographic health survey) uliofanywa mwaka 2016, unaonyesha, ukeketaji upo kwa asilimia 10 nchini (ambapo kwa kila wasichana mia moja, mmoja amekeketwa) ikiwa ni anguko la asilimia 4 ya takwimu za mwaka 2010 ambapo ukeketaji ulikuwa asilimia 14.

Ukeketaji au kwa jina lingine tohara kwa wasichana ni utamaduni usio wa kitabibu wa kubadilisha maumbile ya uke wa mwanamke.

Tatizo la ukeketaji ni gumu kulitokomeza moja kwa moja kwa sababu kuna viongozi wa kimila na baadhi ya wazazi hawataki kubadilika na kuipa kisogo mila hii.

Ukeketaji ni mila inayopingwa katika mataifa mengi duniani ikiwamo Tanzania huku baadhi ya matamko na mikataba ikiitaja mila hiyo kama moja ya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake.

Tatizo lingine ni “wataalamu wa jadi wa ukeketaji” ambao hutegemea ukeketaji kuendeshea maisha yao ya kila siku, huuona ukeketaji ni ajira yenye kipato kikubwa kuliko hata kujishughulisha na biashara nyingine yoyote ile, hali inayosababisha tatizo kuendelea kuwepo.

Hapa nchini, Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepiga hatua katika kulishughulikia tatizo la kuwalinda wanawake na watoto kwa kusaini na kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ya kuwalinda wanawake na watoto dhidi ya vitendo vya ukatili, kama vile ukeketaji na ndoa za utotoni lakini bado mifumo na miundo ya ndani ya nchi haiendani na matakwa ya mikataba hiyo.

Ugumu huu wa vita dhidi ya vitendo vya ukeketaji hauwezi kuwa sababu ya kutosha kuwafanya wadau mbalimbali kuacha kupambana, ndiyo maana shirika la Plan International limekuwa likichukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba utu, ustawi na haki za watoto zinalindwa kikamilifu.

Gazeti hili limefanya mahojiano na Msimamizi wa Miradi ya Ulinzi wa Mtoto kutoka Plan International, Jane Mrema kuhusiana na hali ya ukeketaji nchini na jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na shirika hilo.

Ukeketaji unafanyika vipi?

Ukeketaji au tohara hufanyika kwa kuondoa sehemu ya juu ya uke au uke wote, kuondoa mashavu ya uke, kuondoa mashavu ya uke halafu kushona sehemu ya uke na kuacha tundu dogo kwa ajili ya kupitisha mkojo na hedhi.

Ukeketaji ni utamaduni maarufu kwa Afrika, Asia, Mashariki ya Kati na kwa baadhi ya jamii ambazo utamaduni huu umekita mizizi.Kutokana na utafiti wa UNICEF mwaka 2016, unaonyesha kuwa, wanawake takriban milioni mia mbili wanaoishi katika nchi 30, kati ya hizo 27 zikiwa ni za Kiafrika, Indonesia, Iraq Kurdistan na Yemen, wamefanyiwa ukeketaji.

Ukeketaji hufanyika kumuandaa msichana kuwa mwanamke kamili na shupavu kwani inaaminika kuwa mwanamke anayefanyiwa ukeketaji anaheshimika, mwaminifu, mrembo na ishara ya kuwa tayari kwa kuolewa. Jamii hizo huwatenga wanawake ambao hawajakeketwa.

Licha ya kuwapo kwa mika-taba ya kimataifa na sheria mbalimbali zinazodhibiti vitendo vya ukeketaji na ndoa za utotoni (SOSPA ya mwaka 1998) bado vitendo hivyo vinaendelea. Shida ipo wapi?

Ni kweli, Tanzania tuna sheria mbalimbali zinazosimamia haki na ustawi wa watoto kwa mfano kama vile Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, Sheria ya Makosa ya Ukatili wa Kijinsia (SOSPA,1998) lakini pia tuna Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA) hizo zote zinaangazia katika kulinda haki ya mtoto.

Na kwa kiasi kikubwa Serikali sambamba na wadau mbalimbali wamekuwa wakijitahidi katika kutekeleza sheria hizo kwa nafasi zao.“Mimi nadhani changamoto kubwa ni utayari wa watu kubadili mitazamo na kutaka kuendelea kung’ang’ania mila zilizopita na wakati.

Na hili linajidhihirisha kutoka jamii husika, unaweza ukawaambia watu kuwa ukikeketa utafungwa wakakusikiliza lakini ukiondoka wanafanya kwa siri bila ya wewe kujua.

Hivyo kazi kubwa ipo hapo kwenye kubadili mitazamo ya jamii nyingi kuhusu tendo zima la ukeketaji.“Pia, ipo changamoto nyingine kwenye utekelezaji wa sheria hizo, kubwa hasa ikiwa ni watu wa ngazi ya chini kutofahamu kwa undani vipengele vya sheria hizi na hili linachangiwa na uhaba wa rasilimali watu na fedha ambazo zingeweza kusaidia kufikisha elimu juu ya sheria hizi na namna ambazo zinafanya kazi kwa makosa ya ukatili wa watoto na wanawake nchini,” anasema Jane.

Hali ya ukeketaji ipo vipi Tanzania?

Tanzania kwa sasa hali ya ukeketaji bado si nzuri. Kama bado ukeketaji unaendelea maana yake ukatili dhidi ya watoto haujaisha. Kunahitajika nguvu ya ziada kutokomeza vitendo hivi viovu licha ya takwimu kuonyesha kuwa vitendo hivyo vimepungua.

Kulingana na utafiti wa demografia (Demographic health survey) uliofanywa mwaka 2016, unaonyesha, ukeketaji upo kwa asilimia 10 nchini (ambapo kwa kila wasichana mia moja, mmoja amekeketwa) ikiwa ni anguko la asilimia 4 ya takwimu za mwaka 2010 ambapo ukeketaji ulikuwa asilimia 14.

Kinyume na matarajio ya wengi ya kuwa kupungua huko kwa vitendo vya ukeketaji nchini kungeakisi hadi ngazi ya mikoa, lakini hali ilivyo ni tofauti ambapo ukeketaji umeonekana kukithiri kwa baadhi ya mikoa; Manyara unaongoza kwa asilimia 58, Dodoma asilimia 47, Arusha ni asilimia 41 na Mara ni asilimia 32.

Takwimu hizi ni uthibitisho tosha wa namna vitendo vya ukatili wa watoto na wanawake vimekuwa vikiongezeka. Yapo baadhi ya maeneo ambayo ukatili umekuwa ukifanyika kwa wingi, asilimia kubwa ya maeneo hayo yakiwa ni yale tunayoyaamini kuwa salama kwa watoto wetu; maeneo kama vile shuleni, sehemu za ibada, mitaani, kwenye daladala, majumbani n.k.

Ipi nafasi ya Shirika la Plan International katika kutokomeza ukeketaji?

Shirika la Plan International linafanya kazi na jamii kwa ukaribu likiwa na malengo ya kuelimisha jamii, kuwafumbua macho watoto kutambua haki zao lakini pia kuimarisha mifumo ya ulinzi wa watoto.

Katika kukabiliana na changamoto ya ukatili dhidi ya watoto wa kike, limekuwa likiendesha miradi mbalimbali katika maeneo ambayo ukeketaji umekuwa ukifanyika kwa kiwango cha juu. Kwa sasa lipo mkoa wa Mara ambapo tunatekeleza mradi wa “Tokomeza Ndoa za Utotoni na Ukeketaji” sambamba na washirika wake Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) na wadau wengine.

“Tunautekeleza mradi huu kwa miaka mitano sasa, ambapo tumekuwa tukiwaelimisha watoto wa kike kufahamu madhara ya ukeketaji, wapi pa kupata haki zao na msaada pindi watakapokutana na vitendo vya aina hiyo,” anasema.

Pia, shirika hili linafanya kazi kwa ukaribu na wazazi juu ya madhara ya ukeket-aji na namna ya kuwalinda watoto. “Hatukuwatenga wazee wa kimila ambao ndiyo wenye kufanya uamuzi wa mwisho, tunafanya nao kazi kwa kujadiliana madhara ya ukeketaji na ndoa za utotoni na namna ya kutafuta njia mbadala ya kuwafunda watoto kutoka kwenye utoto kwenda kwenye utu uzima tofauti na ukeketaji.

“Plan International inafanya kazi na Serikali katika kuimarisha kamati za ulinzi wa mtoto katika ngazi ya vijiji, kata na wilaya kwa kuwajengea uwezo kwa mujibu wa mifumo ya Serikali, hili ni sambamba na utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA) 2017/2022.

Kamati hizi za ulinzi baada ya kujengewa uwezo uhusika moja kwa moja na jukumu la upokeaji wa kesi zinazohusu ukatili wa watoto, huzifuatilia kesi hizo na kuchukua hatua zaidi.“Mangariba ni kundi lingine tunalofanya nalo kazi kwa karibu ambapo huwa tunawaelimisha kuhusiana na madhara ya ukeketaji na lengo ni kuwafanya wawe mabalozi wa kupambana dhidi ya ukeketaji.

“Kundi lingine muhimu ambalo tunafanya nalo kazi ni wanaume na vijana kwa sababu tunaamini kwamba wanaume ni sehemu ya kutafuta suluhu kwa sababu wao wanapotumia nafasi zao kama viongozi wa familia ni rahisi kutumia mamlaka waliyonayo kukemea ukeketaji.

Tunawafikia wanaume kwa kutumia michezo kama vile mpira wa miguu na makundi ya “Waelimisha Rika,” anasema.

Ushirikiano na taasisi Tunafanya kazi na wadau mbalimbali; wapo tunaofanya nao miradi moja kwa moja kama vile Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Serikali na wengine ni wadau shirikishi kama vile Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni (TECMN) ambao tunafanya nao kazi katika masuala ya ushawishi na utekelezaji wa sera.

Wapo wadau wengine waliopo mkoa wa Mara, kama vile Msanga Centre ambao wanafanya shughuli za kuelimisha jamii kuhusu athari za ukeketaji na kutoa hifadhi kwa mabinti kipindi cha ukeketaji. Wadau wengine ambao wapo kwa ajili ya kubadilishana uzoefu kama vile UNFPA na wadhamini wetu Umoja wa Ulaya (EU).

Nini kinasimama kama alama ya mafanikio?

Kikubwa ni kwamba tumeweza kuwafikia wengi kwa kuwaelimisha kuhusiana na madhara ya ukeketaji kwa watoto wa kike. Tumewafikia mabinti katika jamii zao hususan wale ambao wapo katika hatari ya kukeketwa majumbani, kwenye shule n.k.Jitihada hizo zimezaa matunda mengine ambapo tumeshuhudia watoto wa kike baada ya kupatiwa elimu juu ya madhara ya ukeketaji wamekuwa wakikaidi kufanyiwa ukeketaji kwa kuamua kukimbia majumbani mwao na kwenda mahali salama zaidi kwao.

Mafanikio mengine ni uimarishaji wa kamati za ulinzi kwa mkoa wa Mara zimekuwa mstari wa mbele kusaidia kuwalinda watoto wa kike dhidi ya ukeketaji.

Tumefanikiwa pia kubadilisha mitazamo ya baadhi ya wazee wa kimila huko mkoani Mara. Kutokana na ukaribu wetu wa kufanya kazi na koo kadhaa za wazee wa kimila, kati ya koo 13 tulizofanya nazo kazi, koo 3 zimekiri kuacha kabisa ukeketaji na kutafuta njia mbadala za kuwan-daa mabinti zao (wapo wanaowapaka mabinti zao unga usoni kuashiria utayari wa mabinti hao kuolewa).

Eneo ambalo kunahitajika mkono wa Serikali ili kuongeza nguvu Moja ya eneo ambalo tunatamani Serikali iendelee kutilia mkazo ni utekelezaji wa sheria na ufuatiliaji.

Jamii itambue kuwa wakienda kinyume na sheria hizo watakabiliana na adhabu au kifungo cha aina fulani, hii itasaida kuon-geza uoga kwa baadhi ya watu kujihusisha na vitendo hivyo.

Sambamba na hilo, tunatamani kuona elimu juu ya sheria hizo zinazosimamia mustakabali wa watoto na wanawake nchini zinafikia ngazi ya chini ambayo ni jamii na inazifahamu kiundani.Licha ya sisi kama shirika, kufanya jitihada kubwa katika kubadilisha mitaza-mo na tabia za wazee wengi wa kimila lakini bado kuna changamoto, kubwa ikiwa ni ukaidi na kutokuwa tayari kwa baadhi ya viongozi wa kimila kubadilika.

Mkono wa Serikali unahitajika katika hili kuhakikisha kuwa viongozi hawa wanakuwa sehemu ya mabadiliko jamii inayotarajiwa nayo.

Ujumbe kwa Watanzania katika mapambano dhidi ya ukeketaji?

Suala la ulinzi wa watoto na wanawake ni mtambuka na ni la kila mtu, hivyo kila mtu anatakiwa kuwajibika kwa nafasi yake na kuhakik-isha kuwa utu na ustawi wa watoto na wanawake unakua, unalindwa na una-boreshwa.

Tusimame kama wadau, wazazi na Watanzania kuhakikisha kuwa watoto hawa ambao ni tunu za taifa hawakatishiwi malengo yao kupitia vitendo vya ukatili kama vile ukeketaji na ndoa za utotoni.

Wahamasishaji wa kupinga ndoa za utotoni na ukeketaji wakionyesha ishara ya kupinga ukeketaji.