ATCL kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na India kujadili fursa za kibiashara

Muktasari:

“Katika mkakati wa biashara wa ATCL ambao ulianza mwaka 2017 ambao utamalizika 2022, tumeandaa safari maalum kwa wafanyabiashara nchini kwenda India (Mumbai) kwa jukwaa la kibiashara la siku mbili kuanzia Machi 5 hadi machi 6, 2020, ambayo itawasaidia wafanyabiashara kupata fursa za masoko kwani watatembelea maeneo mbalimbali ya biashara ikiwemo kituo maalum ambapo bidhaa zote duniani hufikia na kusambazwa”,  Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano cha ATCL, Josephat Kagirwa.

Hatua ya serikali kuifufua Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) inazidi kuleta neema kwa taifa kutokana na safari za ndege za kampuni hiyo kufanya safari zake mbalimbali ndani na nje ya nchi pamoja na bara la Afrika.

Serikali ya awamu ya tano ambayo hadi sasa imenunua ndege nane kwaajili ya kuifufua kampuni ya ndege ya ATCL matunda yake yameendelea kuonekana siku baada ya siku. Miongoni mwa matunda hayo ni kuboresha hali ya usafiri wa anga nchini, kuvutia wawekezaji, kuboresha sekta ya utalii na kufungua fursa za kibiashara katika nchi mbalimbali.

Katika mwendelezo wake wa kuchangiakatika nyanja ya uchumi wa nchi kwa kutumia safari zake, ATCL, imeandaa safari kwa wafanyabiashara wazawa itakayofanyika Machi 4, 2020 kwenda Mumbai India kwaajili ya kukuza biashara baina ya nchi za Tanzania na India.

Safari hiyo ambayo imeandaliwa kwa ushrikiano baina ya ATCL, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Kituo cha Uwekezaji cha India na mawakala wa ndege wa India pamoja na mambo mengine itahusisha kujadili fursa za kibiashara zilizopo katika nchi hizi mbili.

Akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano cha ATCL, Josephat Kagirwa alisema kuwa, safari hiyo itahusisha wafanyabiashara na abiria wa kawaida na lengo lake ni kukuza biashara kwa wafanyabiashara wa Tanzania kwa kuwaunganisha na soko la India.

“Katika mkakati wa biashara wa ATCL ambao ulianza mwaka 2017 ambao utamalizika 2022, tumeandaa safari maalum kwa wafanyabiashara nchini kwenda India (Mumbai) kwa jukwaa la kibiashara la siku mbili kuanzia Machi 5 hadi machi 6, 2020, ambayo itawasaidia wafanyabiashara kupata fursa za masoko kwani watatembelea maeneo mbalimbali ya biashara ikiwemo kituo maalum ambapo bidhaa zote duniani hufikia na kusambazwa”, alisema Kagirwa.

“Tutaondoka hapa tarehe 4 Machi, 2020, tarehe 5 Machi tutakuwa na mikutano kati ya wafanyabiashara wa India na Tanzania, tarehe 6 Machi tutafanya ziara katika masoko ambayo yanapokea bidhaa nyingi zinazotoka nchi mbalimbali kwenda India, tutatembelea masoko yanayouza bidhaa za mbogamboga na matunda na tarehe 7 Machi tutaanza safari ya kurejea Tanzania,” alisema Kagirwa.

Kagirwa alisema kuwa, safari hii ina gharama na tumeweka gharama ndogo ili kuwawezesha wafanyabiashara wengi kuhudhuria tukio hilo kubwa na lenye fursa nyingi.

“Gharama za safari hiyo ni kama ifuatavyo; dola za kimarekani 500 ambazo zitajumuisha kusafiri kwenda Mumbai na kurudi Dar, kupata fursa ya kukutana na wafanyabishara wa India, fursa ya kutembelea masoko mbalimbali. gharama za dola za kimarekani 700 zitajumuisha usafiri wa kwenda Mumbai na kurudi Dar, kukutana na wafanyabiashara, kutembelea masoko pamoja na huduma ya malazi kwenye hoteli ya kitalii kwa siku mbili,” alisema Kagirwa.

Alisema kuwa, mfanyabisahara anaruhusiwa kuongeza siku za kuendelea kubaki nchini India kwa gharama zake mwenyewe. Safari hii itafungua fursa kwa wafanyabiashara wengine.

“Safari hii ni sehemu ya mpango mkakati wetu wa kibiashara wa kuziunganisha nchi ambazo tunafanya safari zetu na ambako tumefungua vituo vyetu, tunaanza na Mumbai na baadaye katika masoko mengine hasa kule tunakoruka. Tunashirikiana kwa karibu na ubalozi wetu wa Tanzania nchini India na ubalozi wa India hapa Tanzania.” alisema Kagirwa.

Alisema kuwa, “tunayo imani kubwa kuwa watakaoshiriki watapata manufaa ya kibiashara. Tunatarajia kuendelea kutekeleza mkakati huu una mikakati mingine ya kibiashara katika masoko yetu yote ili tushiriki kikamilifu katika kukuza biashara,”

Alisema malengo mengine ni kuvu-tia soko la usafirishaji kati ya nchi hizo hususani wa mizigo. Kwa kufanya hivi tunatekeleza malengo ya serikali ya awamu ya tano ya kukuza uchumi wa nchi kupitia ufufuaji wa ATCL, kuweka unafuu wa safari za usafirishaji kwa njia ya anga nchini na nje ya nchi.

ATCL imekuwa mdau mkubwa wa wafanyabiashara katika masoko ya nje kwani mpaka sasa, ATCL inafanya safari za ndani katika vituo visivyopungua kumi,na safari za kwenda nje ya nchi katika nchi takribani saba ambazo zimekuwa na tija kubwa kwa taifa katika nyanja za utalii, elimu, afya, biashara nk. Kwa India (Mumbai) pekee yake tunaruka mara nne kwa wiki kati ya nchi hizi mbili kwa kutumia ndege aina ya B787-8 Dreamliner, yenye uwezo wa kubeba abiria 262 katika madaraja mawili ya biashara na kawaida pia hubeba mizigo zaidi ya tani 30.