ILO yaadhimisha siku ya kimataifa ya haki za kijamii

Muktasari:

Tarehe 20 Februari kila mwaka ulimwengu huadhimisha ‘Siku ya Haki za kijamii’, maadhimisho ya siku hii mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kuziba mianya ya kuwepo usawa ili kufikia haki za kijamii.”

Tarehe 20 Februari kila mwaka ulimwengu huadhimisha ‘Siku ya Haki za kijamii’, maadhimisho ya siku hii mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kuziba mianya ya kuwepo usawa ili kufikia haki za kijamii.”

Siku hii ni muhimu sana kwa Shirika la Kazi Duniani (ILO), ambalo tangu mwaka 1919 limekuwa jukumu lake la kuendeleza haki za kijamii kupitia kazi zenye staha.

Shauku ya kuwepo kwa haki za kijamii, ambayo ni haki ya kila binadamu, kwa wanaume na wanawake, bado ni muhimu kwa sasa kama ilivyokuwa wakati Shirika la Kazi Duniani (ILO) lilipoanzishwa karne moja iliyopita.

Ikikumbukwe kuwa Shirika hili lilisherehekea mwaka jana miaka 100 (karne moja) tangu kuanzishwa kwake, umuhimu wa kufikia haki za kijamii unazidi kuwa mkubwa, kutokana na kuongezeka kwa kutokuwepo kwa usawa ulimwenguni, ambayo ni kikwazo katika kuhakikisha kuwepo mshikamano wa kijamii, ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wanadamu kiujumla.

Kutokana na kuwepo mabadiliko ya tabianchi, mabadiliko ya idadi ya watu, maendeleo ya kiteknolojia na kiujumia, utandawazi, tunashuhudia ulimwengu wa kazi ambao unaendelea kubadilika kwa kasi kubwa.

Changamoto hizi zinapaswa kushughulikiwa ili kutoa fursa za kuwepo haki za kijamii katika ulimwengu wa kazi.Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya kazi na ajira linaendelea kuhimiza haki maeneo ya kazi, kuwepo kwa fursa za ajira zenye staha, kuwepo ulinzi wa jamii na kuimarisha mazungumzo ya kijamii kuhusu masuala kazi.

“Haki za kijamii ni mojawapo ya maeneo muhimu kwenye Azimio la Miaka 100 la ILO kuhusu mustakabali wa kazi, lililopitishwa kwenye Mkutano Mkuu wa 108 wa Shirika mwezi Juni 2019.

Azimio hilo linasisitiza uundwaji wa mustakabali wenye haki na endelevu kwa kuwekeza hasa kwenye maendeleo ya watu kupitia mbinu zinazowasaidia binadamu katika mustakabali wa kazi,” anasema Wellington Chibebe, Mkurugenzi Mkazi wa ILO kwa nchi za Tanzania, Burundi, Kenya, Uganda na Rwanda.

Hapa nchini Tanzania, Shirika la Kazi Duniani (ILO) linafanya kazi na Serikali kupitia Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Wizara na taasisi nyingine lengwa, kutekeleza programu mbalimbali kwa kushirikiana na vyama vya waajiri na wafanyakazi.

Programu hizi ni pamoja na; uundaji wa ajira, ujasiriamali, hifadhi ya jamii, utekelezaji wa sheria za kazi, VVU / Ukimwi, na kutokomeza utumikishwaji wa watoto.Katika maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Haki za Kijamii, ILO inatujulisha kuhusu umuhimu wa sera na mikakati jumuishi kuhusu ukuzaji ujuzi katika kuziba mianya ya kutokuwepo kwa usawa kwani hii ni mojawapo ya sehemu ambayo Shirika linaendelea kufanya kazi na Serikali na wadau wengine.

Kwa kushirikiana na wadau wake wa utatu (Serikali, vyama vya waajiri na wafanyakazi), tangu mwaka 2014 na hata kabla ya hapo, Shirika limekuwa likitoa msaada wa kiufundi kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika kuanzisha program ya utambuzi wa Mfumo wa Mafunzo ya Awali (Recognition of Prior learning) programu ikilenga watu ambao walipata ujuzi kwa mifumo isiyo rasmi, ambao wana viwango vya weledi vizuri lakini hawana sifa na vigezo rasmi.

Mfumo wa RPL hutoa utambuzi unaotegemeana na aina ya weledi na uthibitisho wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo, ambao mara nyingi unakuwa haujathibitishwa. Kuziba mianya ya kutokuwepo kwa usawa kupitia Utambuzi wa Mfumo wa RPL.

Jaribu kufikiri kuwa, umejifunza kwa miaka mingi ili kuwa mtaalamu mwenye ujuzi katika fani fulani lakini huna sifa, cheti au ushahidi wa weledi kuhusu ujuzi ulio nao.

Kwa bahati mbaya, asilimia kubwa ya Watanzania wanaofanya kazi wanaangukia katika eneo hili kutokana na kuongezeka kwa upatikanaji wa ujuzi usio rasmi. Mary Timothy (26) ni mpishi asiyeweza kuona vizuri na Simon France (41) ni fundi muashi kutoka Singida.

Hawa wawili ni watu waliopata mafunzo yasiyo rasmi lakini ni wafanyakazi wenye weledi mkubwa ambao wamefaidika na program ya RPL. Kutokana na ukosefu wa sifa rasmi, mara nyingi Mary na Simon wamejikuta ni miongoni mwa watu wanaoona kuwa wametengwa na fursa za kujikwamua kiuchumi.

Wanazo nafasi finyu katika kupata kazi zenye staha licha ya viwango vyao vya weledi kuwa sawa au wakati mwingine zaidi ya wale waliopata mafunzo katika taasisi rasmi za mafunzo.

Hawana namna nyingine isipokuwa kukubali kufanya kazi za kipato cha chini ili kupata riziki. RPL ni mchakato wa kutambua, kuorodhesha, kukagua na kuhakiki mafunzo yasiyo rasmi kwa kuunganisha viwango vya elimu na mafunzo rasmi.

RPL inatoa fursa kwa watu kupata sifa bila kupitia programu za elimu au mafunzo rasmi. Mpango huu unatekelezwa na VETA kwa msaada wa kiufundi kutoka ILO ili kuweka utaratibu wa ujumuishi wa jamii kwa kuruhusu wafanyakazi wenye ujuzi ambao hawana utambuzi rasmi na uthibitisho hivyo kupata cheti cha VETA.

Mary ambaye ni mama wa watoto wawili wa kike hakumaliza kidato cha sita, anabeba mzigo wa kuisaidia familia yake akiwa na ulemavu wa macho.

Kwa bahati nzuri alipata mafunzo ya uanagenzi (Capprentice) na sasa ana uwezo wa kupika vizuri akifanyia shughuli zake katika mgahawa mdogo uliopo mjini Singida.

Akiwa hana utambulisho rasmi wa ujuzi alioupata, Mary aliweza kuajiriwa na muandaaji vyakula wa kawaida ambapo haikuwa kazi ya staha. Kwa mfano, hakukuwa na mkataba wa kufanya kazi, malipo ni chini ya kima cha chini cha mshahara wa Serikali na hakuna masuala yahusuyo hifadhi ya jamii.

Kama ilivyo kwa Maria, Simon France alijifunza uashi akiwa bado kijana mdogo kwa kupitia mafunzo yasiyo rasmi kutoka kwa baba yake ambaye ni fundi muashi. Ni baba wa watoto wanne wenye elimu ya msingi, na hivyo ilibidi atafute ujuzi mahali popote anapoweza. Ilimlazimu kufanya kazi kama fundi msaidizi katika ujenzi wa hospitali akiwa bado kijana huko huko Singida.

“Nilijifunza mengi kuhusu ujenzi kutoka kwa mhandisi mmoja aliyekuwa akisimamia ujenzi ambaye alionekana kuniamini katika kazi hasa baada ya kuona kwamba nilikuwa nina shauku ya kujifunza. Wiki chache baadaye, mhandisi huyo aliniruhusu kutumia vifaa vya ujenzi na akaniambia naweza kujiunga na kikundi chake,” anasema Simon.

Kufikia mwaka 1998, Simon alifanikiwa kupata kazi isiyo rasmi kama fundi muashi. Alipata ahueni baada ya kupata chanzo cha mapato, lakini alikuwa anajua mapungufu yake kutokana na kukosa sifa rasmi suala ambalo mara nyingi lilimwacha afanye kazi ndogo ndogo na zenye malipo hafifu.Utafiti wa ILO unaonyesha kwamba mafunzo yasiyo rasmi ambayo Maria na Simon waliyapata yamegubikwa na mazingira ya kazi yasiyo salama, masaa mengi ya kufanya kazi, malipo au posho kidogo, kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia na kukosekana kwa utaratibu mzuri wa kubadilisha kazi zisizo rasmi kuwa rasmi.

Kwa sasa, kupitia programu ya RPL, Mary amefaulu mtihani wake wa tathmini katika upishi na anasubiri cheti chake.

“Ninategemea kufanya kazi katika migahawa mikubwa, au hoteli ambapo ninaweza kujifunza kutoka kwa wataalamu,” alisema. Cheti cha RPL kitaongeza matumaini yake ya kufanikisha ndoto hiyo. Kwa Simon, mabadiliko yamekuwa muhimu hususan ukizingatia ufaulu wake wa mtihani wa tathmini wa RPL mwaka 2017.

Simon sasa ni mmojawapo wa watahiniwa zaidi ya 3,600 ambao wamefaulu mitihani yao ya RPL na kupata cheti cha VETA katika kazi zao.Baada ya kupata cheti chake cha VETA katika uashi, Simon aliongezea uwezo wake wa kuvutia wateja wakubwa zaidi kama Serikali ambayo imempa mkataba wa kujenga jumla ya majengo matano ya shule mkoani Singida.

“Ilikuwa ngumu kwangu kupata mikataba ya Serikali kabla ya programu hii. Napata fedha zaidi kutoka kwenye kazi yangu hivi sasa kwa sababu nina cheti. Tangu kupata cheti changu cha VETA naweza kusema kwamba mapato yangu yameongezeka kwa asilimia 100,” alisema Simon.

Simon amepanua biashara yake kijiografia katika mikoa na wilaya tofauti na hivi karibuni amemaliza kazi mjini Dodoma na mara kwa mara hufanya kazi zake Singida vijijini na anasimamia hadi wafanyakazi 30. Hivi sasa ana wafanyakazi 10 wa kudumu wanaofanya kazi ya kudumu chini yake.

“Programu hii imenionyesha kuwa, kujifunza hakuna mwisho. Nategemea kujifunza zaidi kuhusu maendeleo ya teknolojia kwenye eneo langu la kazi ili niwe fundi bora zaidi,” alisema Simon.

Kufanikiwa kwa programu ya RPL kumesababisha Serikali kupanua programu hiyo na kulenga watahiniwa wapatao 10, 000, pia kutoa mafunzo ya wakaguzi wa eneo hili zaidi ya 240 kwa mwaka 2019.

Serikali pia imeongeza stadi nyingine kwa ajili ya kufanyiwa tathmini kutoka nne za awali yaani; uashi, fundi makanika, uzalishaji wa chakula, huduma za chakula / vinywaji na useremala na stadi zilizoongezwa ni pamoja na; ushonaji, ufundi chuma, ufundi bomba, uwekaji umeme majumbani na matengenezo ya vyombo vya moto.

ILO inaendelea kufanya kazi na washirika wa kitaifa kama VETA ili kuhakikisha kuwa mfumo wa RPL umeimarishwa na mchakato huo ni wa ubora na wa gharama nafuu.