VETA yajipanga kuwaandaa Watanzania kuijenga Tanzania ya uchumi wa viwanda


VETA yajipanga kuwaandaa Watanzania kuijenga Tanzania ya uchumi wa viwanda

“Uhitaji wa mafunzo ya ufundi stadi unazidi kuongezeka kila mwaka. Watu wametambua kuwa ujuzi wa aina hiyo unasaidia Watanzania kuajirika kwa urahisi zaidi na wengine kujiajiri wanapohitimu mafunzo hayo”.  Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dk Pancras Bujulu.

Sekta ya viwanda ni sehemu muhimu ya uchumi wa kisasa ambako bidhaa hutengenezwa kwa wingi kwa kutumia mashine na michakato maalumu.

Viwanda uhesabiwa kati ya shughuli za sekta ya upili (Secondary) ya uchumi kwa jumla ambako malighafi zinabadilishwa kuwa bidhaa, kwa mfano pamba kuwa kitambaa na nguo.

Kutokana na umuhimu wa sekta ya viwanda, Tanzania imejiwekea malengo ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na moja ya njia ya kufikia lengo hilo ni kuwa na uchumi unaotegemea viwanda.

Hata hivyo, katika dhamira hiyo ya kuifanya nchi kuwa ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, kunahitajika mikakati stahiki ya mazingira yatakayohakikisha dhamira hiyo inafanikiwa kwa wakati.

Moja ya mikakati hiyo ni kuwekeza katika kutoa elimu ambayo itasaidia kuzalisha wataalamu watakaotekeleza shughuli hizo za viwanda pamoja na kuweka mazingira mazuri ya viwanda vilivyopo ili viongeze uzalishaji.

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ni moja ya taasisi za elimu zinazolenga kutoa suluhisho la upatikanaji wa wataalamu watakaotekeleza shughuli za uzalishaji viwandani.

VETA ni taasisi iliyojipanga kila kona kwa ajili ya kuhakikisha wanalikamata soko kwa upande wa rasilimali watu watakaohitajika kufanya kazi kwenye viwanda na kuwafundisha wengine.

VETA inatambua kuwa, katika kipindi hiki kunahitajika mikakati thabiti ya kupanua wigo na kuimarisha ubora wa mafunzo ili kwenda sambamba na mahitaji ya kuanzisha na kuendeleza viwanda, ili kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dk Pancras Bujulu anabainisha mikakati mbalimbali ambayo wanaendelea kuiweka na kuitekeleza ili kuendelea kuongeza uzalishaji wa nguvu kazi yenye ujuzi katika ufundi stadi.

Kujenga vyuo vipya 39 ndani ya miaka miwili

“Uhitaji wa mafunzo ya ufundi stadi unazidi kuongezeka kila mwaka. Watu wametambua kuwa ujuzi wa aina hiyo unasaidia Watanzania kuajirika kwa urahisi zaidi na wengine kujiajiri wanapohitimu mafunzo hayo”.

Uanzishwaji wa viwanda vya aina mbalimbali nchini pia umekuwa chachu kwa Watanzania wengi, hasa vijana kusaka fursa za kusoma mafunzo ya Ufundi Stadi ili waweze kunufaika na nafa-si za ajira zinazotokana na uanzishwaji huo wa viwanda,” anasema Dk Bujulu.

Anasema kuwa, Mamlaka (VETA) imekuwa na changamoto ya kupokea maombi mengi ya kujiunga na mafunzo zaidi ya uwezo wa vyuo vyake kudahili.

Mamlaka inaitazama changamoto hiyo kama fursa ya kupanua wigo na nafasi za mafunzo hayo. Kwa ufupi, VETA inatambua jukumu kubwa ililo nalo katika kuandaa nguvu kazi inayohitajika katika uendeshaji viwanda na kuongeza ajira kwa vijana.

“Umuhimu wa ufundi stadi umeongezeka zaidi katika kipindi hiki cha mwelekeo wa Serikali ya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unaoendeshwa na viwanda. Unaweza kujiuliza ni viwanda gani vitaendeshwa kwa tija bila kuwa na mafundi stadi?

Bila shaka jibu liko wazi, hakuna! Kwa kutambua hilo, sisi VETA tumejiwekea dira ya Tanzania yenye mafundi stadi mahiri na wa kutosha,” anabainisha Dk Bujulu.

Dk Bujulu anaeleza kuwa katika mpango mkakati wake wa miaka mitano unaotekelezwa kuanzia 2018/2019 hadi 2022/2023, VETA imeweka lengo mahsusi la kuongeza upatikanaji wa mafunzo ya ufundi stadi kwa makundi yote kwa haki sawa.

Mpango huo umezingatia umuhimu wa kupeleka fursa za mafunzo katika maeneo mbalimbali ikiwemo, vijijini na mijini; watu wenye changamoto mbalimbali za kimaisha, kama vile ulemavu au hali ngumu kiuchumi, na wanawake na wanaume sawia.

“Tunataka kila Mtanzania mwenye uhitaji wa mafunzo ya ufundi stadi aweze kuyapata kwa urahisi katika eneo alilopo na katika hali aliyo nayo ili hatimaye, waweze kuboresha maisha yao na kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa Taifa. Kwa sasa VETA inamiliki jumla ya vyuo 33 huku ikitarajia kuongeza vingine 39 ifikapo mwishoni mwaka 2020,”anasema Dk Bujulu na kuongeza kuwa

Ifikapo mwishoni mwa mwaka 2020 matarajio ni kuwa na jumla ya vyuo 72 vinavyomilikiwa na VETA na hivyo kuongeza udahili kutoka 302,000 wa sasa hadi kufikia wanafunzi zaidi ya laki saba (700,000) kwa mwaka.

Dk Bujulu anaitaja miongoni mwa miradi ya ujenzi wa vyuo vipya kuwa ni katika Wilaya za Urambo, Nkasi, Ileje, Muleba, Itilima, Kasulu, Kilindi (Mabalanga), Ngorongoro, Babati, Newala na Chato.

Mingine ni katika Wilaya za Kongwa, Nyasa, Ruangwa na Kasulu Halmashauri ya Mji. Wilaya nyingine vilikoanza kujengwa vyuo vya VETA (katika hatua za awali) ni Kilindi, Korogwe, Ukerewe, Igunga, Lushoto, Kishapu, Rufiji, Uyui, Kwimba, Bahi, Mafia, Longido, Mkinga, Uvinza, Ikungi, Iringa Vijijini, Pangani, Mbarali, Monduli, Buhigwe, Ulanga, Masasi, Butiama, Chemba na Chunya. Vyuo hivyo vinajengwa kwa kutumia rasilimali na nguvukazi ya VETA kwa utaratibu wa “Force Account”.

Pamoja na vyuo vya Wilaya, VETA pia inaendelea na ujenzi wa vyuo vya ngazi ya Mkoa katika mikoa ya Geita, Rukwa na Kagera. Pia, inaendelea na mipango ya kujenga katika mikoa ya Njombe, Simiyu na Songwe.

Dk Bujulu anaendelea kueleza kuwa, pamoja na mkakati wa ujenzi wa vyuo vipya, VETA imekuwa ikibuni njia mbalimbali za kupanua wigo wa utoaji mafunzo ili kuwafikia Watanzania walio wengi katika maeneo yao na kwa gharama nafuu.

Mfano wa njia hizo ni pamoja na utoaji mafunzo kwa njia ya masafa, kama vile kutumia mitandao ya simu na kompyuta; mfumo wa uanagenzi (kwa kuhusisha viwanda na kampuni mbalimbali), Mafunzo ya muda mfupi katika sekta isiyo rasmi pamoja na kufanya utambuzi na urasimishaji wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo (maarufu kama RPL).

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mkuu wa VETA anasema kuwa suala la ubora wa mafunzo nalo linapewa uzito mkubwa, hasa kwa kuzingatia kuwa utoaji mafunzo ya ufundi stadi unajikita zai-di kwenye vitendo.

Anaeleza kuwa VETA imeendelea kufanya jitihada za kujenga na kuboresha karakana kati-ka vyuo mbalimbali. Anatoa mfano wa kiwanda cha kisasa cha kutengeneza Samani cha VETA kilichopo katika Chuo cha VETA Dodoma kilichozinduliwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof, Joyce Ndalichako, Septemba 30, 2019.Pamoja na kiwanda hicho, Dk Bujulu anasema ununuzi na usimikaji wa vifaa vya mafunzo umefanyika kwenye karakana za vyuo mbalimbali nchini, zikiwemo karakana za umeme wa viwandani za VETA Tanga na Mwanza.

Karakana ya ushonaji VETA Pwani; Karakana za ufundi wa zana za kilimo za VETA Kihonda na Arusha; karakana ya uchoraji wa ramani za majengo ya VETA Moshi na karakana za umeme na uchomeleaji na uungaji vyuma za VETA Mtwara.

Vyuo vya ufundi stadi vinatoa mafunzo katika fani zaidi ya 80 zilizogawanywa katika sekta za ajira 13, ambazo ni ufundi mekanika, uuundi umeme, ufundi ujenzi, ufundi magari na mitambo, huduma za biashara, mavazi na nguo, usafirishaji na uchukuzi, uziduzi (utafutaji, uchimbaji na uchakataji madini), uchapaji, urembo na ususi, kilimo na usindikaji chakula, ukarimu na utalii pamoja na fani za sanaa.

Kwa maoni:

Barua pepe: [email protected]

Simu: 0736505027