PSSSF inavyoshirikiana na Serikali kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati


PSSSF inavyoshirikiana na Serikali kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umetimiza mwaka mmoja tangu ulipoanzishwa rasmi Agosti 1, 2018 kwa Sheria Namba 2 ya Mwaka 2018.

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umetimiza mwaka mmoja tangu ulipoanzishwa rasmi Agosti 1, 2018 kwa Sheria Namba 2 ya Mwaka 2018.

Mfuko umeendelea kutoa huduma bora kwa wanachama wake. Wakati Serikali ya Awamu ya Tano ikitimiza miaka mitano, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Hosea Kashimba katika mahojiano na mwandishi wetu anaelezea jinsi Mfuko unavyotekeleza majukumu yake.

Je, PSSSF imeweza kuwafikia wanachama wake wote?

Katika kuhakikisha huduma za mfuko zinawafikia Watanzania wote, PSSSF imefungua ofisi katika mikoa 28 Tanzania Bara (ikiwa ni pamoja na mikoa mitatu ya kimkakati ya Ilala, Kinondoni na Temeke katika Mkoa wa Dar es Salaaam). Pia, tuna ofisi Tanzania Visiwani, zilizopo Unguja na Pemba.

Yupi anawezekana kuwa mwanachama wa PSSSF?

Kuanzia Agosti 1, 2018 walio-kuwa wanachama wa mifuko iliyounganishwa, yaani PPF, PSPF, LAPF na GEPF waliohamishiwa katika Mfuko wa PSSSF wataendelea kuwa wanachama na kuchangia katika mfuko wa PSSSF.

Watumishi wapya walioajiriwa kuanzia Agosti 1, 2018 na wanaoendelea kuajiriwa katika utumishi wa umma, mashirika ya umma na makampuni yote ambayo Serikali inamiliki zaidi ya asilimia 30 ya hisa watatakiwa kusajiliwa na kuchangia katika mfuko wa PSSSF.

Wanachama wa mfuko ni pamoja na wastaafu na wategemezi walio-kuwa wanalipwa pensheni na mifuko iliyounganishwa.

Kwa nini PSSSF inafanya uhakiki wa wanachama wake?

Uhakiki wa wastaafu na wategemezi wanaopata pensheni ni jambo la kawaida na lengo lake ni kuhakikisha mfuko unazo kumbukumbu sahihi za wastaafu wake na kwamba pen-sheni inalipwa kwa mlengwa halisi.

PSSSF imefanya nini kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda?

Kwa kutambua umuhimu wa viwanda katika kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati, mfuko unawekeza katika eneo la viwanda ikiwa moja kwa moja au kupitia ushirikiano na taasisi nyingine ikilenga kuleta manufaa kwa umma kwa kuongeza ajira kwa Watanzania na kuongeza mapato kwa Serikali.

Mfuko umewekeza katika kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi cha Karanga kilichopo, Kilimanjaro. Uwekezaji katika kiwanda hiki umejumuisha ukarabati wa kiwanda cha zamani na ujenzi wa kiwanda kipya.

Ukarabati wa kiwanda cha zamani umekamilika na uzalishaji umeanza na kiwanda kinazalisha jozi 400 kwa siku ambazo wateja wake wakubwa ni majeshi ya Tanzania pamoja na wanachi wa kawaida.

Ujenzi wa kiwanda kipya unaendelea. Mfuko umewekeza katika mradi wa machinjio na kuchakata nyama wa Nguru Ranch uliopo Morogoro. Utekelezaji wa mradi huu umefikia hatua nzuri na mkandarasi ameanza kazi ya kukarabati mifumo ya maji na umeme, kujenga mabwawa ya maji taka pamoja na kuleta na kufunga mashine zote za uchinjaji.

Machinjio haya yanatarajiwa kuchinja ng’ombe 100 na mbuzi 1000 kwa siku. Asilimia 80 ya soko la nyama itakayosindikwa litakuwa nchi za Arabuni na asilimia 20 itauzwa katika soko la ndani. Uzalishji rasmi unatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi Aprili 2020. Kadhalika, mfuko umeweke-za kiwanda cha kuchakata tangawizi cha Same.

Lengo la mfuko ni kusaidia wakulima wadogo na kuendeleza zao la tangawizi. Mashine za kuchakata tangawizi zimeshanunuliwa na kufungwa kiwandani hapo na uzalishaji unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Aidha, mfuko unatarajia kuwekeza kiwanda cha kusindika majani ya chai cha Mponde kilichopo Lushoto Tanga. Upembuzi yakinifu umekamilika na tumeomba kibali rasmi cha kuwekeza kwa Katibu Mkuu Hazina.

Uwekezaji wote huu ni unalenga katika utekelezaji wa sera ya uchumi wa viwanda ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira kwa Watanzania na pia kuongeza thamani ya Mfuko ili uweze kuwahudumia vizuri wanachama wake.

Mfuko umeweka mikakati gani ya kuhakikisha michango ya wanachama na makusanyo mengine ya Mfuko yanakusanywa vyema?

Kama ilivyo kwa taasisi nyingi za umma, PSSSF inatumia mfumo wa kielektroniki wa makusanyo ya Serikali (GePG). Mfumo wa GePG una manufaa kwa PSSSF na wanachama wake, kutokana na uwazi uliopo, lakini pia makusanyo kufika kwa wakati katika mfuko kwa ajili ya kuwekeza kwa wakati ili kulipa mafao yanatotolewa kisheria.

Kwa upande wa PSSSF, mfumo huu hutumika katika ukusanyaji wa michango ya wanachama, mapato ya uwekezaji na mapato mengine. PSSSF ilijiunga na mfumo huo tangu Februari 2019.Katika mfumo wa GePG mwajiri ananufaika na mambo yafuatayo: kujifanyia tathimini ya michango inayoletwa PSSSF, kujitengenezea ankara za malipo, kupata stakabadhi kwa wakati, kulipa michango wakati wowote, kupunguza safari za kwenda kwenye ofisi za mfuko kwa huduma mbalimbali na kutunza kumbukumbu ya ankara na stakabadhi zote za michango katika mfuko.

PSSSF inanufaika na GePG katika maeneo mbalimbali ikiwemo: kuongeza uwazi, kuongeza ufanisi wa ufuatiliaji wa michango kwa waajiri, kukusanya michango kwa wakati na kuwezesha mfuko kufanya ulinganifu wa michango.

Hadi sasa mfuko una wanachama wangapi?

Mpaka sasa mfuko una jumla ya wanachama 660,630 hii ni kwa mujibu wa hesabu zinazoishia mwezi Desemba, 2019. Pia, mfuko una wastaafu 131,522 ambao wamehakikiwa na wanapokea pensheni kila mwezi. Kwa kawaida mfuko hulipa pensheni tarehe 25 ya kila mwezi.

Katika ulipaji wa mafao, Mfuko umetekeleza jukumu hili la msingi na umelipa mafao kiasi gani na kwa wanachama wangapi?

Mfuko umetekeleza vyema jukumu hili la msingi la kulipa mafao ya wanachama wake. Tangu kuanza kwa PSSSF mwaka 2018 hadi Desemba 2019 Jumla ya wanachama 44,098 wamelipwa mafao yenye thamani ya trilioni 2.09.