Nyaraka muhimu unapochukua gari bandarini

Muktasari:

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inawaelimisha wadau na umma kwa ujumla kuhusiana na umuhimu wa fomu za Vehicle Discharge Inspection Transfer Tally (VDITT) na ile ya makabidhiano ya gari (Hand Over Form) wakati mteja anapopokea gari lake kutoka kwa wakala wake wa forodha.

 

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusiana na taratibu mbalimbali zinazohitaji kufuatwa ili kurahisisha utoaji huduma katika bandari zetu.

Njia mojawapo inayotumika katika katika kufikisha elimu hii kwa umma ni kupitia uandishi wa makala za elimu zinazoandaliwa na TPA na kuchapishwa katika vyombo mbalimbali vya habari.

Katika makala hii, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inakusudia kuwaelimisha wadau na umma kwa ujumla kuhusiana na umuhimu wa fomu za Vehicle Discharge Inspection Transfer Tally (VDITT) na ile ya makabidhiano ya gari (Hand Over Form) wakati mteja anapopokea gari lake kutoka kwa wakala wake wa forodha.

Fomu hizi zilianza kutolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa lengo la kuhakikisha wateja wanachukua magari yao kutoka bandarini yakiwa katika hali ile ile kama yalivyoshushwa na kupokewa kutoka melini.

Hatua hii ilichukuliwa na TPA ili kukabiliana na vitendo vya wizi wa vipuri vya magari ya wateja yakiwa katika hatua mbalimbali ya kusafirishwa kuanzia bandarini gari linapopakiwa melini mpaka mteja anavyopokea gari lake baada ya kufika salama.

Vehicle Discharge Inspection Transfer Tally (VDITT)

Vehicle Discharge Inspection Transfer Tally (VDITT) ni fomu inayotumika kuonyesha hali halisi ya gari lilivyopokewa bandarini baada ya kuteremshwa kutoka melini. Fomu ya VDITT imeainisha vipuri mbalimbali vinavyopaswa kuwemo katika gari na sehemu ya kutoa maelezo ya hali ya mwonekano wa gari.

Mara baada ya gari kuteremshwa kutoka melini, Karani wa TPA hulikagua na kujaza fomu hiyo kulingana na hali aliyoona kwa kuweka alama ya vema (√) kwa kipuri ambacho kipo kwenye gari na alama ya kosa (X) kwa kipuri kinachokosekana.

Karani akishakamilisha kujaza fomu hiyo ya VDITT ataiweka ndani ya gari husika mpaka mteja anapokuja kuchukua gari lake.Fomu ya VDITT ina umuhimu mkubwa sana kwa mteja na kwa TPA kwani fomu hiyo inaonyesha hali halisi ya gari lilivyopokewa bandarini baada ya kuteremshwa kutoka melini na kuthibitishwa na Ofisa Mkuu wa meli husika kwa kusainiwa na kugongwa muhuri.

Matumizi ya fomu hii yameondoa malalamiko kutoka kwa wateja na kulinda heshima ya TPA hivyo kuongeza uaminifu wa wateja kwa kuendelea kutumia bandari ya Dar es Salaam.

Wakati wa utoaji au uchukuaji wa gari (delivery) mteja akibaini gari lina tatizo lolote, anatakiwa kuikagua fomu ya VDITT iliyotumika kukagulia gari lake kama inaonyesha vipuri husika vipo au hapana.

Hii ni hatua muhimu ambapo mteja anashauriwa kujiridhisha kuhusu utimilifu wa gari lake kwa kutumia fomu hizi. Usahihi wa hali ya gari la mteja na ukamilifu wa vipuri unawekwa bayana na fomu za VDITT na fomu ya makabidhiano (Hand Over Form).

Matumizi ya stika za rangi ya kijani na nyekunduPamoja na fomu ya VDITT katika ukaguzi wa magari, TPA iliamua kutumia stika za kijani na nyekundu. Baada ya ukaguzi kufanyika na kuthibitika kuwa gari husika lipo sawa likiwa na vipuri vyote, karani wa TPA ataweka stika ya rangi ya kijana yenye alama ya vema (√) juu ya kioo cha mbele ya gari.

Umuhimu wa stika ya kijani ni kuonyesha kwamba gari hilo halina tatizo la kukosekana kwa kipuri chochote kwa gari husika.Endapo gari lililokaguliwa likibainika kuwa na dosari zozote ikiwemo kukosekana kwa baadhi ya vipuri, karani wa TPA ataweka stika ya rangi nyekundu yenye alama (X) juu ya kioo cha mbele cha gari husika.

Matumizi ya stika nyekundu yatathibitisha kwamba gari husika limepokelewa bandarini likiwa na dosari za kukosekana kwa baadhi ya vipuri kama fomu ya VDITT iliyotumika kukagulia gari husika itakavyokuwa inaonyesha.

Fomu ya makabidhiano ya gari (Hand over Form)

Fomu ya makabidhiano ya gari ni nyaraka ambayo hutumika na TPA kwa ajili ya kukabidhiana gari na mteja wakati anapochukua gari lake kutoka bandarini. Wakati wa utoaji au uchukuaji wa magari bandarini ni lazima kila gari liandikiwe fomu ya makabidhiano.

Fomu hii inaonyesha hali halisi ya gari mteja anapochukua gari lake bandarini na fomu ya VDITT ni fomu ambayo inaonyesha hali halisi ya gari lilivyopokelewa bandarini baada ya kuteremshwa kutoka melini.

Baada ya gari kuwasili na kuteremshwa kutoka melini, linahifadhiwa bandarini kusubiri mteja akamilishe taratibu za kuchukua gari lake. Katika kipindi hicho kunaweza kutokea tatizo lolote wakati gari likiwa bandarini hivyo TPA iliona kuna umuhimu mkubwa kuwa na aina ya nyaraka hii ya hand over form.

Nyaraka hii ni muhimu sana kwa mteja kwani itamuonyesha mteja hali halisi ya gari lake wakati wakala wake wa forodha alipolichukua kutoka bandarini. Kama gari husika litakuwa na tatizo lolote, fomu hii itamsaidia mteja kudai fidia kwa gari lake.

Ni muhimu sana kwa mteja anapopokea gari lake kutoka kwa wakala wake wa forodha akabidhiwe fomu hizi za VDITT na ile ya makabidhiano ya gari (hand over form).

Endapo mteja hatapatiwa fomu hizo na wakala wake anatakiwa kutoa taarifa TPA kwa kutuma ujumbe au kupiga simu za bure za TPA. Taarifa hizi hupewa umuhimu mkubwa na TPA kwani huiwezesha Mamlaka kuchukua hatua za makusudi za kukomesha vitendo vya aina yoyote ya usumbufu kwa wateja wetu. Namba hizo ni 0800110032 au 0800110047.

Bandari zetu, lango la biashara kitaifa na kimataifa.