Tanzania inaweza kuendelea kwa kasi na kujenga Taifa la kuigwa katika karne ya 21 kupitia jitihada za jamii na ushirikiano kati ya Serikali na wananchii

Muktasari:

[O&OD iliyoboreshwa imeidhinishwa na Serikali Oktoba 2019 kama sehemu ya mfumo wa kitaifa wa Upangaji Mipango na Utekelezaji. Mfumo huu utaenezwa kwa Sekretarieti za Mikoa yote 26 na Mamlaka za Serikali za Mitaa 185 Tanzania Bara.

Makala haya inawajulisha Watanzania kuhusu moja ya shughuli muhimu zinazofanywa kwa ushirikiano kati ya ya Tanzania na Japan kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA), inayojulikana kama O&OD Iliyoboreshwa.

O&OD Iliyoboreshwa ni nini?

Kwa zaidi ya miaka 10, JICA, imeshirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania, kujaribu kuandaa mtindo imara na endelevu wa maendeleo ya jamii na utoaji wa huduma kupitia Serikali za Mitaa bunifu na “Ushirikiano kati ya Serikali na Wananchi”.

Njia hii inaitwa O&OD Iliyoboreshwa. O&OD ni kifupisho cha “Opportunities and Obstacles to Development” yaani “Fursa na Vikwazo kwa Maendeleo” na dhana hii ilianzishwa na Serikali ya Tanzania mwaka 2001 kukuza upangaji shirikishi wa mipango ya maendeleo katika jamii. Tangu mwaka 2009, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-Tamisemi) na JICA wamekuwa wakitekeleza mradi wa ushirikiano kuboresha mfumo wa “O&OD” ili kuhuisha kwa ufanisi zaidi “Jitihada za Jamii” pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali za Mitaa na Jamii.

Dhana hii ya “O&OD Iliyoboreshwa” ipo katika msingi na urithi mkubwa wa kipekee wa nchi kutoka kwa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Faida ya kipekee duniani kwa Tanzania

JICA ilitambua kuwa katika Tanzania, kuna jamii nyingi ambazo watu wanajipanga na kufanya maamuzi ya kuboresha maisha yao na kuendeleza jamii bila kusubiri Serikali iwafanyie. Taasisi nyingi mfano shule za msingi, zahanati, barabara za vitongoji, skimu za umwagiliaji na miradi ya maji zimejengwa kwa nguvu za wananchi. Aidha, tumejifunza kwamba huu ni urithi kutoka kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere aliyeamini: “maendeleo ni ushiriki wa wananchi katika kujifunza kwa pamoja kupitia uzoefu walionao, wakitumia nguvu zao, rasilimali asilia zilizopo, mawakala wa mabadiliko na rasilimali kutoka nje.

Watu hawawezi kuendelezwa bali wanajiendeleza wenyewe kwa kushiriki shughuli zinazochangia maendeleo. Watu hawaendelezwi kwa kuwaburuza kwenye miradi mipya kama wanyama.”Hata hivyo, inasikitisha kuona siku hizi watu wengi wameacha utaratibu huu bora wa shughuli za maendeleo. O&OD Iliyoboreshwa inalenga kukumbuka na kuhuisha utamaduni huu mzuri wa Taifa uliofifia.

Taifa la Japan limepata maendeleo kupitia njia sawa kama ya Tanzania

Utamaduni huu muhimu wa Tanzania unatukumbusha uzoefu wetu wenyewe wa maendeleo katika nchi ya Japan. Mwanzoni, katika kujenga nchi na maendeleo yake mwishoni mwa Karne ya 19 na mwanzoni mwa Karne ya 20, Serikali ya Japan ilikuwa maskini na rasilimali chache za nchi zilielekezwa kwenye mpango mkakati wa Maendeleo hasa viwanda na majeshi kuepuka kutawaliwa na zilizokuwa Dola zenye nguvu za Ulaya.

Kwa kuwa Serikali haikuwa na uwezo wa kutosha kushughulikia mahitaji ya watu, kila jamii ilijaribu kukabiliana na umaskini na kuboresha maisha kupitia “Jitihada za Jamii”, viongozi na ushirikiano baina yao. Serikali za Mitaa zilitimiza jukumu muhimu la kuongoza jitihada za jamii, kuwatia moyo na kuwasaidia.

Serikali Kuu pia ilijaribu kuhakikisha mazingira wezeshi kwa Serikali za Mitaa kutekeleza jukumu hili.Kama ilivyoonekana hapo juu, maendeleo ya Japan hayakufikiwa kwa jitihada za Serikali pekee, bali kimsingi ni kila mwananchi, jamii na makundi (kampuni ndogo) waliofanya jitihada za kujiletea maendeleo. Serikali ilishukuru, ikasaidiana nao, kuwatia moyo na kukuza jitihada hizo.

Serikali haiwezi kufanya kila kitu peke yake

Kama ilivyokuwa kwa Serikali ya Japan wakati huo, Serikali ya Tanzania inakumbana na changamoto zilizo sawa za uhaba wa rasilimali kwa suala la bajeti na upungufu wa watumishi katika kutekeleza majukumu mbalimbali na makubwa. Haiwezekani Serikali kufanya kila kitu peke yake.

Kutokana na msingi wa uchambuzi huo, OR-Tamisemi na JICA walitambua wazi kuwa njia sahihi na ya ufanisi ya kuleta maendeleo katika nchi hii ni kutumia kikamilifu faida ya utamaduni mzuri uliopo wa “Jitihada za Jamii” ili kuongezea nguvu za Serikali kuelekea maendeleo ya kijamii na kitaifa na kuboresha maisha ya watu.

Kwa sababu hiyo, mradi wa “O&OD Iliyoboreshwa ulit-ambua kuwa msingi mkuu ni kujenga uwezo sahihi wa Watumishi wa Ugani katika Kata (kilimo, maendeleo ya jamii, elimu, afya, mifugo n.k.) ambao wapo mstari wa mbele katika kuongoza jamii na kushirikiana nao. Wanatarajiwa kuwa daraja kati ya jamii na Serikali.

Kutoa mafunzo kwa watumishi wa ugani wa kata namna ya kuiwezesha jamii

Mradi ulianzisha mfumo bunifu wa kutoa mafunzo kwa watumishi wa ugani kwa njia ya vitendo. Njia hii iliwajengea uwezo na mbinu za kuiwezesha jamii kutambua na kuthibitisha mahitaji yao ya msingi, kujipan-ga na kutekeleza shughuli mbalimbali kila inapowezekana badala ya kungoja Serikali iwafanyie.

Watumishi wa ugani waliopatiwa mafunzo haya wanaitwa “Wawezeshaji wa Kata” (WFs). Baada ya kupatiwa mafunzo, wawezeshaji wa kata hutembelea Vitongoji mara kwa mara. Baada ya kuwezeshwa na wawezeshaji wa kata, jamii huanza kutekeleza miradi ya vipaumbele kulingana na uwezo walionao. Ifuatayo ni mifano kadhaa ya mambo ambayo yamekuwa yakifanyika katika vijiji husika (tunasikitika kuwa tutaonyesha mifano miwili tu kati ya mingi iliyopo).

Vijiji vinabadilika kwa kasi kupitia O&OD IliyoboreshwaKijiji cha Maseyu - shule za awali katika vitongoji vyote vitano na ukamilishaji wa ujenzi wa Zahanati.

Ukisafiri kutoka Morogoro kuelekea Dar es Salaam kwa muda wa dakika 30 utaona Kijiji cha Maseyu kandokando ya barabara kuu. Hofu ya muda mrefu ya wanakijiji ilikuwa kuwapeleka watoto katika darasa la awali lililopo umbali mrefu kuvuka barabara kuu yenye hatari nyingi.

Baada ya ajali mbaya ya mvulana mmoja kuumwa na nyoka akiwa anarudi nyumbani kutokea shuleni, wananchi walisimama na kuamua kujenga darasa la awali katika kila vitongoji. Wawezeshaji wa kata walitekeleza jukumu kubwa la kuwezesha jamii kukubaliana na kuamua kujipanga kufikia ndoto yao.

Baada ya miaka miwili, vitongoji vyote vitano vilikamilisha ujenzi wa Shule za Awali jambo liliopunguza muda wa watoto kutembea kwenda shuleni, hatari ya kupata ajali na pia kuongeza uandikishaji kwa kasi. Haikuwa ujenzi wa madarasa ya awali tu, lakini pia wanakijiji walitafuta mtu mwenye uwezo wa kufundisha watoto katika Kitongoji na kumlipa mshahara.

Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ilitambua jitihada kubwa ya watu wa Maseyu kwa upendeleo mkubwa. Shule za Awali zote zimesajiliwa na Serikali kisheria na Halmashauri imepanga waalimu katika shule hizo kwa sasa. Kutokana na uzoefu walioupata katika ujenzi na ukamilishaji wa Shule za Awali, wanakijiji walishawishika kukamilisha Zahanati ya Kijiji iliyokuwa imetelekezwa kwa miaka kadhaa.

Kazi hii imewachukua karibu miaka 7 lakini waliendelea bila kukata tamaa, wakiendeleza kidogo kidogo, hatua kwa hatua na hatimaye wamekamilisha hivi karibuni. Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ilisaidia vifaa vya kuezeka na kupanga watumishi. Zahanati ilianza kutoa huduma rasmi Julai 2018.Wananchi wana imani kubwa kwa wawezeshaji wa Kata na Halmashauri ya Wilaya na wanajivuna kwa kusema kuwa kijiji chao ni bora katika Tanzania.

Zaidi ya hayo, ofisa mtendaji wa Kijiji aligombea na kushinda katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 na kwa sasa ni Diwani anayeongoza maendeleo ya Kata yake.

Mang’ula B na Mshikamano: Mabadiliko chanya ya mtazamo wa Wanakijiji

Kijiji cha Mang’ula B kipo katika Wilaya ya Kilombero kandokando ya barabara kuu ya kutoka Mikumi kwenda Ifakara. Kijiji kikiwa mkabala na lango kuu la kuingia Hifadhi ya Udzungwa, kinafikiriwa kuwa mazingira ya mji unaokua kwa kasi kikiwa na mwingiliano na uhamiaji wa watu. Kutokana na hali hii, Wawezeshaji wa Kata walipata changamoto kubwa kuhamasisha “Jitihada za Jamii”.

“Hatukuwahi kuiamini Serikali na watumishi wake hapo awali”. Mwanamke mmoja wa Kijiji hiki alituambia na kuendelea; Walitutembelea mara chache sana na walipofika walitulazimisha kufanya mambo tusiyoyakubali. Lakini hawa Wawezeshaji wa Kata ni tofauti. Tunawaona kila siku wakituongoza katika shughuli zetu, wanatusikiliza na kwa sasa ni sehemu ya jamii.

Tunawachukulia kama sehemu ya familia yetu. (Hali kama hii inaonekana kwenye picha) Sikutoa ardhi yangu kipindi ambacho TASAF walikuja kutengeneza barabara. Lakini kipindi hiki nimetoa ardhi yangu kwa sababu tuliamua wenyewe kutengeneza hii barabara pamoja na Wawezeshaji wa Kata.” Kijiji cha Mang’ula B kwa sasa ni Kijiji bora katika mradi. Wanakijiji wana umoja.

Wanawaamini Wawezeshaji wa Kata na Viongozi wa Kijiji. Mwenyekiti wa Kijiji Bw. Hamisi alichaguliwa kwa sababu alikuwa kiongozi mahiri wa kikundi katika shughuli za maendeleo. Wananchi walifanya ujenzi wa barabara yenye urefu kilometa 14 katika Kijiji na kujenga madaraja ya kuwezesha watoto kuvuka wakati wa kwenda shuleni (angalia picha), wametundika mizinga ya kisasa kandokando ya hifadhi kuzuia Tembo kuingia katika mashamba na kuharibu mazao.

Wananchi waliamua kujenga jengo la biashara lenye vyumba vya kupangisha ili kuwa na mapato ya ziada yatakayokuwezesha kugharamia miradi mingine zaidi. “Sikuwahi kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Kijiji”. Mmoja wa viongozi wa kikundi cha wanawake alituambia; “Sikufikiri kuwa mkutano huu ni kwa ajili yetu. Mkutano ulikuwa wa viongozi.

Lakini kwa sasa nahudhuria kwa sababu katika kufanya shughuli za kikundi, niliona kuwa nahitaji kushiriki katika kufanya maamuzi ya masuala yanayotuhusu hapa kijijini.” Kwa sasa anahudhuria mikutano siyo kwa sababu “anatakiwa kuhudhuria” ila kwa sababu “anataka kuhudhuria.”

Tunayo ndoto

Ndoto ya kweli tuliyonayo ni kuwa Tanzania itakuwa na vijiji vizuri kama hivi nchi nzima vyenye nguvu na umiliki wa maendeleo yao katika misingi imara ya uzalendo, kujivunia na kuipenda jamii yao.

Tunaamini kuwa inawezekana kabisa katika nchi hii, kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa karibu kati ya jamii na Serikali za Mitaa, pamoja na usaidizi imara kutoka Serikali Kuu ili kuhakikisha mazingira wezeshi ya ushirikiano huu.

Kwa kufanya hivyo, Serikali itaweza kutoa huduma bora kwa wananchi kwa gharama ndogo, huku ikielekeza nguvu na rasilimali chache zilizopo kwenye miradi mikubwa ya kitaifa ya maendeleo kama Japan livyoendeleza uchumi na ustawi wa watu wake.