CCM kupinga matokeo ya Mdee, Mch. Msigwa mahakamani

Thursday October 29 2015

Msemaji wa Kambi ya Kampeni ya CCM, January

Msemaji wa Kambi ya Kampeni ya CCM, January Makamba . 

By Beatrice Moses, Mwananchi

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimelalamikia utaratibu wa ukusanya kura na kujumlisha matokeo kwenye baadhi ya majimbo, huku kikikusudia kukata rufaa mahakamani  kupinga matokeo ya Jimbo la  Mikumi, Kawe, Iringa Mjini na Ndanda.

Msemaji wa Kampeni ya CCM, January Makamba alisema jana kuwa kuna maeneo mengine walipoteza viti vya ubunge wameshindwa kihalali, lakini ni tofauti na kwenye majimbo hayo.

Alisema wamebaini kuna ukiukwaji  wa taratibu za uchaguzi kwenye majimbo hayo ambayo wagombea wa Chadema, Halima Mdee ameibuka mshindi Kawe, Joseph Haule ‘Profesa J’ (Mikumi), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini na Sisulu Mwambe  (Ndanda).

“Wasimamizi katika majimbo  haya wamevuruga uchaguzi kutokana na utata uliojitokeza wakati wa kujumlisha kura, CCM iliomba kura zihesabiwe upya, lakini ikanyimwa haki hiyo ya msingi ambayo ipo kisheria, lakini kwenye baadhi ya majimbo ikiwamo Nyamagana wapinzani walipewa fursa hiyo,” alisema January.

Alisema uamuzi wa kwenda mahakamani una lengo la  kujiridhisha kwamba utashi wa wananchi umeheshimiwa.

“Bado tunaendelea kukusanya taarifa ya maeneo mengine tulikopoteza viti ili kuona kama kulikuwa na ukiukwaji wa kubadilisha  matakwa ya wapiga kura wengi,” alisema.

Advertisement

January alitumia nafasi hiyo pia kupongeza ushindi waliopata Freeman Mbowe (Hai) na James Mbatia (Vunjo) na kukiri kwamba CCM walizidiwa na wananchi wametumia utashi wao katika kupiga kura.

“Tunakiri kwamba kwenye maeneo mengi tulikopoteza viti vya ubunge tumepoteza kihalali hatuna malalamiko, tunaheshimu uamuzi wa wananchi na tunajitathimini kama chama ili tubaini makosa na kujirekebisha,” alisema.

Alisema wanalaani vitendo vya vurugu ikiwamo kuharibu mali za CCM na Serikali uliofanywa na watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ikiwamo kuchoma moto ofisi za CCM katika Wilaya ya Mbozi, Temeke kwa Sandali na Mahakama  mkoani Songwe.

Alisema kinachoonekana hivi sasa ni baadhi ya wagombea walioshindwa kutofuata sheria badala yake kuendeleza siasa za uchaguzi kwenye mitaa kwa kuhamasisha  vurugu na maandamano.