CEMOT: Wagombea wengi waridhika na Matokeo

Muktasari:

Muhtasari uliotolewa leo na Mwenyekiti mweza wa Cemot, Martina Kabisama ulieleza kuwa hadi juzi jioni, asilimia 73 ya waangalizi wao 717 waliokuwepo kwenye vituo vya kuhesabia kura waliripoti kuwa wagombea wa ubunge walikubaliana na matokeo.

Dar es Salaam. Wakati zoezi la kuhesabu na kutangaza matokeo ya Uchaguzi likiwa mwishoni, mwamvuli wa waangalizi wa ndani (Cemot) umesema kuwa sehemu kubwa ya wagombea wa ubunge na udiwani walioshindwa walikubaliana na matokeo ya kura walizopata.

Muhtasari uliotolewa leo na Mwenyekiti mweza wa Cemot, Martina Kabisama ulieleza kuwa hadi juzi jioni, asilimia 73 ya waangalizi wao 717 waliokuwepo kwenye vituo vya kuhesabia kura waliripoti kuwa wagombea wa ubunge walikubaliana na matokeo.

Kabisama alisema kuwa robo ya wagombea wa ubunge walioshindwa sawa na asilimia 27 walipinga matokeo hayo ya uchaguzi uliofanyika Jumapili iliyopita.

“Katika swali liliuliza je, wagombea walioshindwa walikubali matokeo, waangalizi wetu 697 sawa na asilimia 97 waliripoti kuwa wagombea wa ngazi ya udiwani walikubali kushindwa.

“Ni kiwango kidogo sana cha wagombea wa udiwani kama asilimia tatu hivi ndiyo waliyokataa matokeo ya kura walizopata,” alisema Kabisama.

Cemot ni mwamvuli wa taasisi ya waangalizi wa ndani wa Uchaguzi (Temco) na muungano wa waangalizi wa ndani wa Uchaguzi kutoka asasi za kiraia (Tacceo) ambao unafuatilia mwenendo wa Uchaguzi nchini.

Hata licha ya baadhi ya wagombea kukataa matokeo ya Uchaguzi huo, muhtasari huo wa Cemot, unabainisha kuwa sehemu kubwa ya nchi haikutawaliwa na vurugu baada ya kutangazwa matokeo.

Kabisama alisema ni asilimia tano tu ya maeneo yote yaliyoangaliwa yalikuwa na vurugu baada ya kutangazwa matokeo ya ngazi ya udiwani wakati katika ngazi ya ubunge asilimia 10 kulikuwa na vurugu.

Ripoti hiyo ya Cemot inaenda sanjari na taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Polisi wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja aliyesema kuwa sehemu kubwa nchini Uchaguzi ulifanyika salama kasoro maeneo machache ambayo baadhi ya wafuasi wa vyama hasa vijana waliendelea kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani kwa kisingizio cha kucheleweshwa matokeo.

“Vijana hawa wamekuwa wakiongozwa na hisia potofu za kwamba wanaibiwa kura, nitumie fursa hii kuwaonya kuacha vitendo hivyo mara moja, jeshi la polisi linaendelea kuchukua hatua za kuwadhibiti na wengine tayari wameshafikishwa mahakamani,” alisema Chagonja katika mkutano wake na wanahabari juzi jioni.

Ili kukabiliana na vurugu hizo za kudai matokeo, Kabisama aliwataka maofisa waliomaliza kuhesabu kura kutangaza matokeo haraka au kuwajulisha wananchi kinachoendelea ili kupunguza sintofahamu.