Diwani Bukoba asomewa mashtaka akiwa Hospitali

Diwani mteule wa Kata ya Kagondo Manispaa ya Bukoba(NCCR Mageuzi)Dokta Anatory .

Muktasari:

Mtuhumiwa huyo alikamatwa siku ya kupiga kura tarehe 25,Octoba na baadaye kupata tatizo la afya wakati akihojiwa katika kituo cha polisi Bukoba ambapo alipelekwa hospitalini hapo kwa ajili ya kupatiwa matibabu na ameendelea kuwa chini ya ulinzi hadi aliposomewa mashitaka.

Bukoba. Diwani mteule wa Kata ya Kagondo Manispaa ya Bukoba(NCCR Mageuzi)Dokta Anatory Amani amesomewa mashitaka matatu yanayohusiana na kuingilia taratibu za uchaguzi huku akiwa amelazwa kwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kagera.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa siku ya kupiga kura tarehe 25,Octoba na baadaye kupata tatizo la afya wakati akihojiwa katika kituo cha polisi Bukoba ambapo alipelekwa hospitalini hapo kwa ajili ya kupatiwa matibabu na ameendelea kuwa chini ya ulinzi hadi aliposomewa mashitaka.

Kwa mujibu wa wakili wa Serikali Mwandamizi Athuman Kirati mtuhumiwa anakabiliwa na mashitaka matatu ya kuchukua vishina vya kupigia kura bila ruhusa,kufungua vishina vya kupigia kura na kuingilia mchakato wa upigaji kura bila kuwa na ruhusa hiyo kisheria.

Hata hivyo mtuhumiwa alikana mashitaka hayo ambapo kupitia kwa wakili wake Aaron Kabunga aliomba mteja wake apatiwe dhamana kwa kuwa mtuhumiwa amelazwa hospitalini hapo tangu alipokamatwa ambapo hakimu mfawidhi Denis Mpelembwa alikubali ombi la mtuhumiwa kupatiwa dhamana kwa kiasi cha shilingi milioni mbili.

Kesi hiyo inayomkabili Dokta Anatory Amani ambaye amewahi kuwa meya wa Manispaa ya Bukoba kupitia CCM, imehailishwa na itasikilizwa tena tarehe 12,Novemba,2015 ambapo mtuhumiwa amepewa sharti la kutosafiri nje ya Mkoa wa Kagera bila idhini ya mahakama.