RC Arusha apiga marufuku mikusanyiko kushangilia matokeo

Mkuu  wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda.

Muktasari:

Ntibenda aliyasema hayo jana Jijini hapa wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mchakato wa uchaguzi jijini humo ambapo pia aliwapongeza wasimamizi wa uchaguzi  ngazi ya Kata, Ubunge, Udiwani pamoja na Urais kwa kufanikisha zoezi hilo kwa amani na utulivu.

Arusha . Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda  amepiga marufuku mikusanyiko na ushangiliaji wowote wa masuala ya kisiasa jijini Arusha na kuwataka wananchi kuwa watulivu wakati wakisubiri Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), kutangaza mshindi wa nafasi ya Uraisi.
Ntibenda aliyasema hayo jana Jijini hapa wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mchakato wa uchaguzi jijini humo ambapo pia aliwapongeza wasimamizi wa uchaguzi  ngazi ya Kata, Ubunge, Udiwani pamoja na Urais kwa kufanikisha zoezi hilo kwa amani na utulivu.

Ntibenda alisema amani ya nchi ni muhimu kuliko jambo lolote hivyo ni vyema wananchi wakaidumisha kwa kuwa watulivu huku wakisubiri mgombea atakayetangazwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungao wa Tanzania.

“Ningependa kuwataka wananchi wa Jiji la Arusha kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho tunasubiria nani atatangazwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo kwa mamlaka niliyokuwa navyo nakataza maandamano yoyote ya kisiasa na mikusanyiko isiyokuwa na tija,”alisema.

Alisema washindi na walioshindwa wote ni wananchi wa Jiji la Arusha na wote ni watanzania  na hivyo kukataza kuzomeana sanjari na kushambuliana kisiasa katika maeneo mbalimbali.

"Hakuna mtu mwenye mamlaka ya kutangaza matokeo na naomba amani tuliyonayo idumishwe nawapongeza wasimamizi wa uchaguzi kwa kusimamia vyema uchaguzi wetu hadi leo hii umeisha salama na hakuna vurugu". Alisema.

Alisema idadi ya waliojiandikisha kupiga kura Mkoa mzima wa Arusha ilikuwa 1,000,988 , idadi ya waliopiga kura ni 730,970 sawa na asilimia 73.4 , kura halali ni 718,933 , zilizoharibika 12,036 sawa na asilimia 5.9.

Ntibenda aliyasema hayo baada ya kutokea baashi Ya makundi ya vyama vya siasa jijini Arusha  yaliyokuwa yanahamasishana juu ya kufanya maandamano ya nchi nzima kupinga matokeo ya Urais kwa madai kuwa yameibwa na baadhi ya wapinzani wao CCM ambayo hata hivyo yaligundulika na kuimarisha ulinzi.

Ends…