Rais mteule aikosoa CCM

Muktasari:

Alisema kwamba asiposema atakuwa ni  mnafiki kwa sababu uchaguzi umekwisha bora wawekwe wazi kwa sababu anaona ni bora kuishi na mchawi kuliko mnafiki, alimuomba Mwenyekiti  wa chama hicho Jakaya asiwahurumie wanaokihujumu, hivyo kusababisha washindwe kufika kwenye malengo.

Dar es Salaam.  Rais Mteule Dk John Magufuli ameamua kufunguka kuhusu ugumu aliokabiliana nao wakati wa mchakato wa kampeni akieleza kuwa  uchaguzi wa mwaka huu umekuwa na changamoto kubwa kutokana na hujuma zilizofanywa na wanafiki waliojificha ndani ya Chama cha Mapinduzi(CCM).

Alisema amekerwa na hali hiyo kiasi cha kushindwa kuvumilia kuizungumzia jana, hasa baada ya kuona  uchaguzi umekwisha, hivyo ni vyema wanafiki hao wakajisalimisha kwa kutubu  kwa kuwa wamekigharimu chama hicho na kusababisha kiwe kwenye  wakati mgumu.

Alisema kwamba asiposema atakuwa ni  mnafiki kwa sababu uchaguzi umekwisha bora wawekwe wazi kwa sababu anaona ni bora kuishi na mchawi kuliko mnafiki, alimuomba Mwenyekiti  wa chama hicho Jakaya asiwahurumie wanaokihujumu, hivyo kusababisha washindwe kufika kwenye malengo.

“Nisiposema nitakuwa mnafiki msema kweli ni mpenzi wa Mungu watubu wajirekebishe ni mara kumi kuwa na mpinzani kutoka nje kuliko ndani ya chama,mipango yenu mtaipanga mchana usiku wataitoa nje ni afadhali uwe na mchawi atakuroga ufe kuliko mnafiki ndani, ” alisema.

“ Lakini ukweli utabaki kuwa ukweli  wewe ni mwenyekiti lakini ulikaa na wanafiki ndani ya CCM, ndiyo wametufanya wakati mwingine tufike hapa tulipofika, ndiyo wametufanya tufike hapa tulipo , leo kwa hiyo nakuomba ukitengeneze chama chetu vizuri ukishamgundua mnafiki usikae naye fukuza kesho, nimeona hili nilizungumze lakini unisamehe sana kwa sababu ningebaki nalo moyoni ningenisababishia kiungulia,ambacho nimekiona wakati nazunguka nikiwa kwenye kampeni,” alisema Dk Magufuli.

Kuanza kazi haraka

wahakikishiwa wananchi kuwa  mara baada ya kuapishwa siku hiyo hiyo atanza kufanya kazi, kwa kuwa hakuomba nafasi hiyo kwa majaribio bali kuwatumikia wananchi kwa dhati.

Pia ameomba ushirikiano mzuri kutoka kwa wananchi ili waweze kufanikisha yale ambayo wameahidi wakati wa kampeni yeye na na Makamu Rais Samia Suluhu Hassan,  ili waweze kutimiza wajibu wa kuwatumikia  bila kinyongo na kuyatimiza yake waliyoahidi wakati wa kampeni.

“Kwa hiyo niwaombe  ndugu zangu watanzania wote bila kujali vyama vyetu tunaomba sana ushirikiano wenu , tusipopata ushirikiano wetu hatuwezi kuyatimiza kwa wakati, tisipopata ushirikiano mzuri kutoka kwenye mtatuchelewesha mara unataka kufanya hizi mara kuna maandamano yakashindwe, yakalegee  yakabaki huko huko yalikoanzia, kwa sababu sisi tunataka tufanye kazi,” alisema Dk Magufuli na kushangiliwa.  

Aliongeza  kusema“ Katika kuzunguka kwetu kwa  wananchi wameona kuna kero nyingi za maji, umeme, miundombinu, wananchi wanataka zitatuliwe haraka, niwaombe watanzania bila kujali  vyama naomba ushirikiano wenu mzurI, ili tufanikishe hayo tuliyoahidi wakati wa kampeni,” alisisitiza.  

Amsifu JK

Rais huyo Mteule alimsifu  Rais wa awamu ya nne Dk Jakaya Kikwete  akisema kwamba ni wa tofauti kwani licha ya kumtembeza katika maeneo karibu yote ya Ikulu , lakini pia amekuwa na busara za kukubali na kuendeleza madaraka ya kupokezana.

“ Nataka niseme mheshimiwa Rais una moyo wa pekee, Mungu akujalie sana viongozi wengi Afrika wanapokaribia kuondoka madarakani wengine huwa wanatengeneza hata katiba tofauti ili katiba ili waendelee kubaki madarakani, lakini wewe upo tayari kuondoka hata leo,” alisema.

Dk Magufuli alisema anaamini kwamba wananchi wataendelea kumuombea, kumlinda kwa kuwa amethamini Tanzania Kwanza, hivyo ataendelea kuhitaji busara zake pale itakapobidi atakapoingia madarakani.  

Awali akitoa maoni yake mara baada ya Dk Magufuli kukabidhiwa cheti cha ushindi, Mratibu wa Taifa wa ULINGO, Dk Ave Maria Semakafu alisema anaamini wanawake wengi wamefurahishwa na ushindi huo kwa sababu kwa umewezesha pia kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi kuwa na Makamu wa Rais mwanamke Samia Suluhu Hassan.

“ Tumefungua ukurasa mpya kwani miaka 20 ya tamko la Mkutano wa wanawake  Duniani wa mwaka 1995 Beijing, tumekuwa na mrejesho mzuri kuhusu mwitikio wa Serikali kuweka ushiriki sawa wa nafasi za uongozi badala ya kuwafanya wanawake wawe watu wa kupiga kura kwa kuchagua viongozi wa ngazi mbalimbali lakini sasa nao wanachaguliwa, wanaaminika na kupewa nafasi kubwa ya uongozi kama hii,” alisema Dk Semakafu .

Alisema uchaguzi wa mwaka huu umekuwa ni wa kihistoria katika mambo mengi licha ya ushindani wa kisiasa lakini wanawake wawili walikuwa ni wagombea akiwamo Anna Mgwira aliyekuwa akigombea nafasi ya urais kupitia chama cha ACT Wazalendo.

“ Binafsi nilikuwa nafuatilia kwa karibu kampeni zao kulikuwa na mwitikio mkubwa wa watu walikuwa wakiwasikiliza na hakukuwa na hali ya udhalilishaji wa kuona kwamba hawastahili kwa sababu tu wao ni wanawake ,” alisema .