Ukawa wateka manispaa Dar es Salaam

Thursday October 29 2015

HONGERA: Mbunge mteule wa Jimbo la Kawe, Halima

HONGERA: Mbunge mteule wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee akiwa amebebwa na wafuasi wake baada ya kutangazwa kuwa mshindi jijini Dar es Salaam juzi. Picha na Said Khamis 

By Waandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam/ mikoani. Vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimefanikiwa kushinda kata nyingi katika jiji la Dar es Salaam na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kuongoza mabaraza ya madiwani katika halmashauri za manispaa za Ilala, Kinondoni na Temeke.

Mbali ya kusimamia mabaraza hayo, pia Ukawa unaweza, kwa mara ya kwanza, kuongoza halmashauri ya jiji la Dar es Salaam.

Tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa mwaka 1992, CCM imekuwa ikishinda kata nyingi na hivyo madiwani wake kuunda halmashauri, lakini mwaka huu imepokonywa kata nyingi katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumapili iliyopita baada ya Ukawa unaoundwa na vyama vya NLD, CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi kunyakua ushindi katika kata hizo.

Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi huo yanayoendelea kutangazwa Ukawa umenyakua viti 53 vya udiwani katika majimbo ya Kinondoni, Ukonga, Ilala, Segerea, Temeke, Kibamba, Kawe, Ubungo, Mbagala na Kigamboni wakati CCM ikipata viti 38.

Moja ya Halmashauri ambazo Ukawa wataziongoza ni ya Kinondoni ambako umetwaa kata 22 kati ya 34. Katika halmashauri hiyo yenye majimbo ya Kawe, Ubungo, Kibamba na Kinondoni, Chadema imenyakua kata 17, CUF imeshinda kata 6, na CCM imetwaa kata 9 huku yakisubiriwa matokeo ya kata mbili.

Halmashauri ya Ilala yenye majimbo ya Ilala, Ukonga na Segerea, matokeo yanaonyesha kwamba Chadema ina kata 19, CCM kata 15 na CUF kata mbili. Madiwani wa kata hizo ndio watakutana kuteua meya na naibu meya wa halmashauri ya Ilala.

Advertisement

Halmashauri ya Temeke inayoundwa na majimbo ya Temeke, Kigamboni na Mbagala ina jumla ya kata 31. Katika jimbo la Temeke CCM ina kata 7, Chadema 5 na CUF 1; Kigamboni: CCM kata 6, Chadema 2 na CUF 1, wakati Mbagala CCM kata 7 na CUF tatu.

Aidha, upinzani umefanikiwa kutwaa majimbo sita kati ya 10. Majimbo hayo na majina ya wabunge wake kwenye mabano ni Kawe (Halima Mdee – Chadema), Kinondoni (Maulid Mtulia – CUF), Temeke (Abdallah Mtolea – CUF), Ukonga (Mwita Waitara –Chadema), Ubungo (Saed Kubenea – Chadema), Kibamba (John Mnyika- Chadema).

Waitara amepata ubunge baada ya kumbwaga aliyekuwa meya wa Ilala, Jerry Slaa (CCM); Mtolea amemshinda Abbas Mtemvu (CCM); Mdee amemwangusha Kippi Warioba (CCM), na Kubenea amemshinda aliyekuwa meya wa jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi (CCM).

Mnyika amembwaga Fenella Mkangalla (CCM), Mtulia amemshinda Idd Azzan (CCM). Bonna Kaluwa wa CCM ndiye mbunge wa Segerea, Faustine Ndungulile wa CCM amefanikiwa kutetea jimbo la Kigamboni sawa na Mussa Hassan Zungu aliyetetea jimbo la Ilala.

Matokeo ya mikoani

Jimbo la Ndanda lina kata 16; CCM (15), Chadema (1); Tandahimba: kata 30, CCM (10), CUF (16), Chadema (1); Kalenga: kata ni 15, CCM (13), Chadema (3); Iringa Mjini kata 18, Chadema (14), CCM (4); Isimani kata 14, CCM (11) Chadema (3); Ushetu kata 20, CCM (20); Serengeti kata 30, CCM (12), na Chadema (18).

Jimbo la Dodoma Mjini kata 41, CCM (34), Chadema (6); Mpwapwa lina kata 13, CCM (13); Kibakwe kata 18, CCM (18); Mbozi kata 11, CCM (7), Chadema (4); Mtwara Mjini kata 18, CUF (8), CCM (7), Chadema (3); Mwibara kata 12, CCM (7), Chadema (2), TLP (2) na CUF (1); Bunda Mjini kata 14, CCM (10) na Chadema (4); Bunda Vijijini kata 7, CCM (5) na Chadema (2).

Handeni Mjini kata 12, CCM (11), CUF (1); Handeni Vijijini kata 21, CCM (20), Chadema (1), Kilindi kata 21, CCM (20) kata moja haijafanya uchaguzi; Vunjo kata 16, NCCR (8), CCM (4), Chadema (4); Sikonge kata 17, CCM (14), Chadema (3); Kahama Mjini kata 20, CCM (19) Chadema (1).

 Momba kata 14, CCM (8), Chadema (6); Mbeya Vijijini kata 29, CCM (21), Chadema (7); Kisarawe: CCM (14), Chadema (2), CUF (1); Nanyumbu CCM (15), CUF (2), na Bagamoyo kata zote 11 zimechukuliwa na CCM.

Imeandikwa na Emma Kalalu, Elizabeth Edward, Bakari Kiango, Ephrahimu Bahemu na Harrieth Makweta.