Waangalizi waibana ZEC

Baadhi ya wakazi wa Kisiwa cha Unguja, wakisikiliza kwa kutumia simu za mkononi taarifa za uamuzi wa kufutwa kwa matokeo ya urais wa Zanzibar na wawakilishi kupitia redio mbalimbali baada ya kutangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

Waangalizi hao, wakiongozwa na Goodluck Jonathan, rais wa kwanza wa Nigeria kukubali kushindwa kwenye uchaguzi, pia wametaka viongozi wa kisiasa visiwani Zanzibar kuweka kando tofauti zao na kushirikiana kutafuta suluhisho la haraka la mgogoro kwa kuweka maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar.

Dar es Salaam. Waangalizi wa kimataifa wa Uchaguzi Mkuu nchini wameitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kueleza sehemu ambazo zilikuwa zina ukiukwaji wa taratibu na kuonyesha uwazi katika kufikia uamuzi wake wa kufuta matokeo ya uchaguzi wa rais wa visiwa hivyo na wawakilishi.

Waangalizi hao, wakiongozwa na Goodluck Jonathan, rais wa kwanza wa Nigeria kukubali kushindwa kwenye uchaguzi, pia wametaka viongozi wa kisiasa visiwani Zanzibar kuweka kando tofauti zao na kushirikiana kutafuta suluhisho la haraka la mgogoro kwa kuweka maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar.

Wakati waangalizi hao wakitoa tamko hilo, Serikali ya Uingereza imekuwa ya pili kuitaka ZEC kuendelea na mchakato wa uchaguzi.

ZEC ilifuta matokeo yote ya uchaguzi wa Rais na wawakilishi wa Zanzibar juzi, ikieleza kuwa imejiridhisha kuwa kulikuwapo na ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi na kutangaza kuwa itaitisha uchaguzi mwingine ndani ya siku 90. “Tumechukulia kwa uzito mkubwa tamko lililotolewa na mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ambalo alibatilisha uchaguzi wa Zanzibar,” inasema taarifa hiyo ya pamoja ya waangalizi wa kimataifa.

Waangalizi hao wameeleza kuwa katika ripoti yao ya awali walieleza jinsi walivyoridhishwa na mchakato wa upigaji kura na kuisifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ZEC na Watanzania kwa jinsi walivyojitokeza kwa wingi kupiga kura.

Ujumbe wa waangalizi hao unaongozwa na Jonathan wa Jumuiya ya Madola, Oldemiro Baloi (SADC), Armando Guabuza (Umoja wa Afrika) na Judith Sargentini (Jumuiya ya Ulaya (EU)).

“Tunashauri uongozi wa kisiasa wa Zanzibar kuweka kando tofauti zao, kuweka maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar mbele na kushirikiana kutafuta suluhisho la haraka la masuala ambayo yamesababisha tatizo hilo,” inasema taarifa hiyo.

Mapema jana, ubalozi wa Uingereza ulitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikieleza kuridhishwa na mchakato na kuitaka ZEC iendelee na kazi ya kuhesabu kura.

“Tunaitaka ZEC irejee katika mchakato wa kujumlisha kura bila kuchelewa,” inasema taarifa hiyo.Katika hatua nyingine, Maalim Seif Sharif Hamad amemtaka Rais Jakaya Kikwete na Ali Mohamed Shein wa Zanzibar kubeba dhamana ya uongozi kwa kusimamia Katiba na sheria za nchi katika siku chache zilizobakia za madaraka yao.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mtendeni, Maalim Seif alisema marais hao wawili wanatakiwa kuheshimu uamuzi wa Wazanzibari waliofanya Oktoba 25 na kuwataka washirikiane naye kuinusuru Zanzibar.

“Nawaomba sana Rais Kikwete na Rais Shein kukwepa matumizi ya nguvu, badala yake tushirikiane kutunza amani na haki za wananchi. Mimi niko tayari kushirikiana nao kama ambavyo nimekuwa nikifanya mara zote. Tushirikiane kuiepushia Zanzibar na Tanzania na fedheha ya kimataifa,” alisema Maalim Seif.

Wachambuzi wa kisiasa na wanasheria wamesema uamuzi wa ZEC ni ukiukwaji wa demokrasia nchini.

Profesa Mohamed Bakari kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema licha ya kuwapo kwa wangalizi wa uchaguzi, hali ya kisiasa inaweza kuwa mbaya zaidi.

”Hakuna hoja ya msingi ya kufuta uchaguzi huo ila ni hofu ya kuvunjwa Muungano, endapo Maalim Seif ataingia madarakani,” alisema Profesa Bakari.