Mpina: Natimiza wajibu, sikwenda bungeni kucheza disko na mawaziri

Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Mwaukoli Kata ya Kisesa wakati wa Tamasha la Ngoma za Asili. Picha na Stella Ibengwe

Muktasari:

  • Mbunge huyo amekuwa kwenye mvutano na mawaziri akiwakosoa bungeni kila anapopata nafasi ya kuchangia huku nao wakisimama kumjibu na kufafanua kile anachokizungumza.

Simiyu. Mbunge wa Jimbo la Kisesa (CCM), Luhaga Mpina amewajibu wanasiasa wanaosema hakuna maendeleo aliyofanya katika jimbo lake badala yake amesema  yeye hakutumwa bungeni “kucheza disco na mawaziri bali kufanya kazi”.

Amewaonya wote wanaopambana naye kwamba wataishia kudhalilika kwa kuwa hawezi kucheka na waziri ambaye hatekelezi majukumu yake ipasavyo.

Mpina ametoa kauli hiyo leo Mei mosi, 2024 wakati akizungumza na wananchi kwenye Tamasha la Ngoma za Asili katika Kijiji cha Mwaukoli, Kata ya Kisesa, Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.

Hivi karibuni, mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed akiwa kwenye ziara yake jimbo la Itilima, alisema katika jimbo la Kisesa hakuna maendeleo yaliyofanyika, wananchi wanakabiliwa na changamoto nyingi na mbunge wao hajafanya maendeleo yoyote.

Mbali na kiongozi huyo wa CCM, mawaziri wamekuwa wakimpiga vijembe Mpina bungeni huku wakimtaka ajielekeze kwenye shughuli za maendeleo ya wananchi badala ya kupinga kila kitu kinachoelezwa na mawaziri.

Akizungumza kwenye tamasha hilo, Mpina amesema anapoona waziri aliyepewa jukumu la kusimamia wizara hatekelezi jukumu lake, hawezi kucheka naye kwani wananchi wamemtuma bungeni kufanya kazi ya kuleta maendeleo na lazima atimize wajibu huo.

“Acheni tuwaletee maendeleo, hao wengine wanaopita na kujitapa kuwa hakuna kilichofanyika, sisi tuko imara, tuko makini na maendeleo yataendelea kupatikana… wataendelea kudhalilika. Sikutumwa bungeni kwenda kucheka na mawaziri au kucheza disko, bali kufanya kazi,” amesema Mpina.

Mbunge huyo amekuwa kwenye mvutano mzito na mawaziri ambapo na amekuwa akiwakosoa bungeni kila anapopata nafasi ya kuchangia hoja na mawaziri nao wamekuwa wakisimama kumjibu na kufafanua kile anachokizungumza.

Juni 2023, wakati akichangia Bajeti ya Serikali, Mpina alisema kuna mazingira ambayo yanasababisha biashara ifungwe na kutoa mfano kiwanda au mgodi unatiririsha sumu kwenye vyanzo vya maji, hata hivyo alipinga biashara kufungwa kiholela bila sababu za msingi.

Hata hivyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wakati akijibu hoja zilizotolewa na wabunge, alitumia muda mrefu kumpiga vijembe Mpina kuhusu hoja yake ya kupinga biashara kufungwe kwa wamiliki wanaodaiwa kodi.

Siyo Mwigulu pekee, Mpina amekuwa akiwakosoa mawaziri wengine pia akiwemo January Makamba wakati akiwa Waziri wa Nishati na Wiziri ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira); Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, Waziri wa Ujenzi, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.

Mbali na kula sahani moja na mawaziri, Mpina amekuwa akiibua hoja nzito bungeni na nje ya bunge ambazo zinaibua mjadala mpana kwenye mitandao ya kijamii.

Wakati hoja ya Katiba mpya ikipigiwa kelele na vyama vya upinzani, mbunge huyo wa CCM aliibua sakata la mchakato wa Katiba mpya bungeni akihoji hatua za maandalizi zilizofikiwa na Serikali katika jambo hilo.

Katika hatua nyingine, Mpina alitaka kuundwa kwa timu kuchunguza mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) katika kipande cha Tabora hadi Kigoma baada ya kubaini gharama za ujenzi ni kubwa kuliko vipande vingine kwa Sh3.4 bilioni kwa kila kilometa.

Novemba 13, 2022, Mpina alimtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalumu kwenye deni la Taifa akisema Serikali ilikopa fedha zaidi ya kiasi kilichoidhinishwa na Bunge huku deni la Serikali likifikia Sh71.55 trilioni.


CCM yambana

Kufuatia kauli zake hizo, January 24, 2024, Kamati ya Usalama na Maadili Wilaya ya Meatu, Mkoa wa Simiyu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ilimwita Mpina kujibu tuhuma mbalimbali.

Hata hivyo, matokeo ya hatua hiyo hayakutangazwa wazi badala yake CCM wilaya ilisema imewasilisha ripoti kwenye chama hicho ngazi ya mkoa.


Maendeleo yanaonekana

Wakati jimbo hilo likidaiwa halina maendeleo, Diwani wa Kata ya Kisesa, Magulu Yanga amesema wanaendelea kusimamia shughuli za maendeleo ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri ikiwemo miradi ya afya, miundombinu, elimu na maji.

Amesema katika suala la utamaduni, ni sehemu ya kutoa elimu kwa wananchi kupitia sanaa mbali na kupata burudani, hivyo amewaomba wananchi kuendelea kushirikiana ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kukuza uchumi.

Mkazi wa Kata ya Kisesa, Peter Mhoja amesema kulikuwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara lakini kwa sasa imefanyiwa kazi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa, miradi ya sekta ya afya na maji, hivyo maendeleo yanaonekana.

Kwa upande wake, mkazi mkazi wa Kijiji cha Mwaukoli, Paskazia Alphonce amesema awali walikuwa wanatembea zaidi ya kilomita nane kufuata huduma za afya, lakini sasa tatizo limekwisha baada ya kujengwa kwa kituo cha afya.