Mshairi nguli Amiri Andanenga afariki dunia, azikwa

Jeneza lililobeba mwili wa aliyekuwa mshairi, mtaalamu nguli wa lugha ya Kiswahili,  Mzee Amir Sudi Andanenga (sauti ya kiza)  wakati wa mazishi yake yaliyofanyika leo Mei Mosi, 2024 kwenye makaburi ya Kinondoni Shamba mkoani Dar es Salaam. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Alikuwa mtu wa mashairi hasa ya kimapokeo, aliyefahamu historia ya washairi nchini.

Dar es Salaam. Mwanasheria na mwandishi wa vitabu vya riwaya za fasihi za Kiswahili na Kiingereza, Charles Mroka amemuelezea hayati Amir Andanenga kama mtu aliyekuwa na kipaji cha kutunga mashairi.

Andanenga aliyekuwa mwanafasihi nguli na mwasisi wa Chama cha Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (Ukuta) amefariki usiku wa kuamkia leo Mei Mosi, 2024, katika Hospitali ya Dokta Mvungi Kinondoni alikokuwa akipatiwa matibabu.

Mroka amesema hayo leo wakati wa maziko ya nguli huyo yaliyofanyika kwenye makaburi ya Kinondoni Shamba.

Amesema Tanzania imepoteza mtu kwenye tasnia ya ushairi hasa ya kimapokeo na mtu aliyekuwa anafahamu historia ya washairi nchini.

"Andanenga ni kizazi kilichofanya kazi na washairi nguli kama hayati Shaaban Robert, Saadani Kandoro na wengine wengi. Alifanya kazi na vizazi vyote na alikuwa mshauri mzuri na hazina ya historia ya Kiswahili na ushairi," amesema.

Amesema kama ni sifa au tuzo wasanii wapewe wakiwa hai.

"Andanenga ni mtu aliyependa ushairi, Kiswahili na wakati wote ukimtembelea nyumbani hata kama unahitaji kumbukumbu ya ushairi fulani mbali na kwamba alikuwa haoni alikuwa na uwezo wa kukupatia bila kusaidiwa na mtu," amesema.

Amesema Andanenga kabla ya kuwa mshairi alikuwa mfanyakazi wa Serikali na alikuwa anafanya kazi Ofisi za Bunge la Tanzania akiwa karani na baadaye kuhamishiwa Wizara ya Maji.

Amesema mwaka 1972  alipata maradhi ya macho na alifanyiwa operesheni akiwa katika hatua hiyo bahati iliyokuwa mbaya macho yake yalipoteza nguvu kabisa ya kuona.

"Licha ya kwamba lengo la operesheni ile ilikuwa nzuri lakini ilisababisha asione tena. Ingawa hali hiyo haikumkatisha tamaa baada ya kupofuka macho alianza kutumia mfumo wa uchapaji wa mtu asiyeona," amesema.


Amesema aliendelea kuchapa kazi zake kwa mfumo huo na alitoa diwani mbalimbali ikiwemo diwani ya ustadhi na nyingine ambazo hazijaingizwa kwenye mfumo wa mtandao.

"Diwani ya Ustadhi iliendelea kukaa na alikuwa anapigania zitumike kwenye taasisi za elimu kuwaomba watumie kwenye mtalaa, ndipo mwaka 1998 iliteuliwa kuwa kitabu cha kiada kwa wanafunzi wa sekondari fasihi ya Kiswahili mashairi," amesema

Amesema hata hivyo nguli huyo aliyewahi kutunukiwa tuzo sufufu za lugha ya Kiswahili kutokana na ubora wake wa kutunga aliendelea kutunga vitabu vingine kama Bahari ya elimu ya ushairi na vilitumika mataifa mbalimbali ikiwemo Rwanda na Kenya.

"Ukiacha kazi yake ya ushairi Andanenga alikuwa mtu anayeibua maswali na misamiati mbalimbali mfano kuna neno 'bahati mbaya' alikuwa anakataa bahati ni kitu kizuri utasemaje kitu kizuri kiwe bahati mbaya ni vizuri kuita isivyo bahati badala ya kusema bahati mbaya," amesema.

Amesema alikuwa mzee wa kuzua mjadala ingawa alikuwa anakusanya wafuasi wengi ambao wanasema isivyo bahati ingawaje kuna wanazuoni wengine wanampinga.

"Andanenga alikuwa na kichwa kinachoweza kunasa maneno na mwenyewe anasema alisoma hadi darasa la nane Mkoa wa Ruvuma ingawa hakuendelea kutokana na sababu za kiuchumi," amesema

Jumanne Undi aliyekuwa rafiki wa karibu, amesema Andanenga alizaliwa Kilwa mkoani Lindi mwaka 1936 amefariki akiwa na miaka 88.

Amesema mashairi mengi aliyoandika yalikuwa yanavutia, yakagusa maisha ya watu moja kwa moja. Lakini yalijaa utajiri mkubwa wa lugha, nahau, methali na vibwagizo vingi.

Yalisaidia kukuza lugha adhimu ya Kiswahili, kiasi kwamba yaliitangaza nchi kwa mapana.

Kutokana na utajiri huo, vitabu vingi alivyotunga mashairi na hata wale walioandika katika magazeti, vilitumiwa kufundishia katika shule za msingi na sekondari, na baadhi yake vilitumiwa kwa kiwango kikubwa katika vyuo vya elimu ya juu.

"Kwa bahati mbaya, umahiri na ushindani wa watunga mashairi ulianza kufifia miaka ya 90, na tangu wakati huo hadi sasa ni watunzi wachache sana waliobaki, na hata wao hawatungi tena yenye mguso na hisia kubwa kama walivyokuwa watunzi wa zamani," amesema Undi