Wamiliki wa shule nchini mmemsikia Dk Biteko?

Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko amekiasa Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi Nchini (TAPIE), kuzingatia masharti yaliyoainishwa katika barua na vyeti vya usajili wa asasi hiyo.

Dk Biteko amesema kuna baadhi ya wamiliki hukiuka masharti hivyo kusababisha migongano isiyo ya lazima na mamlaka zilizokasimiwa kusimamia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya uendeshaji wa asasi za elimu nchini.

Vilevile, amewataka kufuata sheria na kanuni za utoaji elimu, kuhimiza na kuimarisha maadili, nidhamu na malezi bora kwa watumishi na wanafunzi walio chini ya asasi zao.

Pia, amesema kuwa suala la uadilifu katika shughuli za uendeshaji na usimamizi wa mitihani ya kitaifa lisisitizwe na kutiliwa mkazo ili kupata wataalam wenye sifa stahiki.

Kauli ya Dk Biteko ni muhimu hasa katika kulinda usomi wenye weledi nchini, kumekuwa na maneno mengi kuhusiana na suala la uvujaji wa mitihani.

Suala la uvujaji wa mtihani liliwahi kuzungumzwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa kushirikiana na asasi zinginekwa kuanzisha mikakati kadhaa ya kudhibiti tatizo hilo kwa kukusanya maoni yatakayosaidia kupata ufumbuzi.

Pamoja na jitihada hizo suala la uvujaji wa mitihani na udanganyifu bado limeendelea kusuabua hadi sasa, na hasa suala la watahiniwa kuandika maneno ya kejeli na kuchora vitu visovyoelekewa kwenye karatasi za majibu ya mitihani.

Kwa kauli ya Dk Biteko ya kusisitiza uadilifu katika shughuli za uendeshaji na usimamizi wa mitihani ya kitaifa, linapaswa kusisitizwa na kutiliwa mkazo ili kupata wataalam wenye sifa stahiki.

Suala la uvujaji wa mitihani na udanganyifu linapaswa kubebwa kwa uzito wake na TAPIE, siyo jambo jema nchi ikawa na wahitimu waliopitia njia za mkato, kwenye udanganyifu wa mitihani.

Uaminifu wa Serikali kwa shule binafsi uendane na wajibu wao wa kutoa wananfuzi waliopitia kwenye tanuri la mafunzo na wakaiva ipasavyo.

TAPIE ni wadau muhimu katika maendeleo ya elimu nchini hivyo, wasikubali kuharibiwa sifa na wanachama wao wachache kwa tama ya fedha na kuvutia shule zao kwa madai ya kuwa na wanafunzi wengi wenye ufaulu mkubwa.

Dhana ya shule hii ndiyo inafaulisha sana, haipaswi kuendekezwa ni muhimu TAPIE ikashirikiana na Serikali kudhibiti viwango vya ubora elimu nchini kwa kuwasema wazi wazi wanachama wao wanaojaribu kutafuta sifa ya ufaulu mzuri wa shule zao.

Sote tunafahamu Taifa linahitaji elimu iliyo bora ambayo siyo tu kufaulu mitihani, bali pamoja na kumjengea uwezo mwanafunzi wa kutumia elimu aliyoipata kutatua changamoto anazokumbana nazo katika maisha ya kila siku.

Siyo sawa sawa kujenga mfumo wa elimu uliojikita zaidi katika kufaulu vizuri kwenye mitihani ya kumaliza shule na badala yake mwanafunzi ajengwe kielimu kwa maisha yake ya baadaye.

Dk Biteko ameonyesha kwamba Serikali haiwatupi sekta binafsi na hasa shule binafsi ili kuboresha sekta ya elimu nchini, lakini ahadi hiyo ya Serikali inapaswa pia kuheshimiwa na kutekelezwa kwa vitendo na TAPIE.

Haitokuwa sawa sawa Serikali inafanya jitihada za kuboresha elimu huku baadhi ya wamiliki wa shule kwenye sekta binafsi, wanafanya jitihada za kuonyesha shule zao ni bora kwa kufaulisha kwa alama za juu kwenye mitihani ya kumaliza shule kwa njia zisizo halali.

Maelekezo ya Dk Biteko kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama ya kuratibu mkutano wa pamoja kati ya TAPIE na Wizara za Ardhi, Fedha, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) yatasaidia kupata suluhu ya changamoto za pamoja.

TAPIE wana changamoto zao, lakini vile vile wazazi wanaosomesha watoto wao nao wana changamoto ambazo zinapaswa kushughulikiwa kwa pamoja.

Mazingira wezeshi yaliyowekwa na Serikali kwa sekta binafsi ambapo kwa sasa kuna shule binafsi nyingi, yanapaswa kutumiwa kwa manufaa ya maendeleo ya wanafunzi na nchi.