Sophia alivyong’oa meno aigize tamthilia

Muktasari:

  • Akizungumza na gazeti hili mwigizaji huyo, amesema kwa kuwa anapenda kazi yake na ndiyo inamfanya alee familia yake, ilibidi ang’oe meno yake ili kuweka uhalisia na utofauti kwenye tamthiliya hiyo kwa kuwa ilihitaji mtu wa aina hiyo

Waswahili husema usione vyaelea ujue vimeundwa, msemo huu una akisi safari ya mwigizaji Afsa Omary maarufu kama Sophia, ambaye ili kuweka uhalisia kwenye Tamthiliya ya Jua Kali ya Lamata Leah ilimbidi ang’oe meno yake mawili ya juu.

Akizungumza na gazeti hili mwigizaji huyo, amesema kwa kuwa anapenda kazi yake na ndiyo inamfanya alee familia yake, ilibidi ang’oe meno yake ili kuweka uhalisia na utofauti kwenye tamthiliya hiyo kwa kuwa ilihitaji mtu wa aina hiyo.

 Kama wewe ni mfuatiliaji wa Jua Kali  basi huyu ni yule dada anayependa kunyoa upara mke wa Idd ambaye ana wake wawili, mwingine ni Semeni ambao wamekuwa hawaishi vitimbi kila mara.

“Nakumbuka siku ambayo naletewa stori inayohusu kung’oa meno na Lamata nilimwambia mimi naweza kutoa meno, alihoji utawezaje wewe una familia una mchumba siyo rahisi, lakini mimi nilimwambia inawezekana.

“Siku niliyoamua kufanya hivyo sikumshirikisha mama wala Lamata mwenyewe, walishtukia tu siku ya tukio, niling’oa meno mawili ya mbele maumivu yalikuwa makali sana lakini hilo halikunipa shida kwa sababu nilitaka kufanya uhalisia na kazi hii ndio inanipa maisha,” anasema msanii huyo.

Anasema baada ya kutoa meno mama yake na Lamata walishtuka na kutofurahishwa na tukio hilo lakini hawakuwa na chakufanya kwa sababu tayari alishafanya hivyo, hakuna njia nyingine.

“Mama yangu aliumia sana lakini baadaye akawa upande wangu kutokana na kukubali nilichokifanya kwa lengo la kupata fedha za kuendesha maisha, kwa upande wa mchumba wangu nilimuambia ni maigizo tu sijatoa meno, alikuja kutambua baadaye, akashtuka sana,” anasema Sophia ambaye amekuwa akipambana na Semeni kila mara kwenye maigizo ya ndoa yao.

Sophia anasema sini aliyokuwa anatakiwa kuigiza ni ile ya kuonyesha kuwa amefumaniwa na kupigwa akang’olewa meno.
“Nilielezwa kuwa sini ninayotakiwa kuigiza nikiwa sina meno ni ile ya kufumaniwa ambapo nilipigwa na kuonyesha kuwa nimetolewa meno mawili, sisi huwa tunaingiza uhalisia, baada ya hapo ndiyo nikaja kuolewa na Idd,” anasema Sophia.4


Dm za kumnunua  

Kutokana na uhalisia ambao amekuwa akiuonyesha kwenye Tamthiliya ya Jua Kali, Sophia ameiambia Mwananchi kuwa jinsi alivyoigiza kama changudoa wengi wamekuwa wakiona kama ni uhalisia na kuanza kumsumbua.

“Mimi ni mtoto niliyelelewa na mama yangu pekee kwenye maisha ya uhalisia kuna sehemu nimeyaigiza maisha yangu ndani ya Jua Kali, japo siyo yote lakini kuna wafuatiliaji wa tamthiliya hiyo wanaona ni uhalisia na kunifuata hadi kwenye maisha ya kawaida ili waweze kuninunua kingono jambo ambalo mimi sifanyi.

“Kwa wale ambao hawawezi kunifikia kirahisi wamekuwa wakitumia mtandao wangu wa kijamii ‘Instagram’ kwa kuingia DM na kuniambia kuwa wana kiasi fulani cha fedha tuweze kuonana ili tukamalizane, mara nina elfu 50, sijui laki, dah! nimekuwa nikiwadharau sana,” anasema.

Anasema changamoto hiyo ndiyo inamtesa pekee hadi sasa kwenye maisha yake ya uigizaji hasa kwenye kazi ya Jua Kali, mbali na kutoa meno ambayo anakiri kuwa hayampi shida yoyote kwani sasa anatumia ya bandia na maisha yanaendelea.


Jua Kali inamuumiza mama 

Anasema kwa kuwa vingi anavyoigiza kwenye Jua Kali vina akisi maisha ya nyuma, vimefanya mama yake awe anaumia kila akitazama tamthiliya hiyo.

“Mama yangu anafahamu namna nilivyokuwa napambana na maisha, kutokana na tamthiliya ya Jua Kali kuyaishi baadhi ya maisha tuliyopitia amekuwa akilia kila anapopata nafasi ya kuangalia kwa anakumbuka nyuma.

“Kiukweli mama yangu kuna muda namzuia asiangalie kwa sababu anakuwa hana raha, kila akiangalia tamthiliya anaona nayaishi maisha yangu lakini ni shabiki yangu namba moja kwa sababu nimekuwa nikiendesha maisha yake na yangu kupitia kazi hii ya sanaa,” anasema.


Mlela amkutanisha na Lamata 

Sophia ameeleza kuwa Yusuph Mlela amechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio yake kwani ndiye aliyemkutanisha na Lamata.

“Mlela ndiye aliyenifikisha hapa nilipo sasa, kwa sababu baada ya kusota mtaani kwa muda tangu lilipotoka kwenye filamu ya Furaha Iko Wapi ya 20 Pacent nilitafutwa na Yusuf Mlela ambaye alitaka kuniweka kwenye filamu yake lakini sikuweza kutokea.

“Nakumbuka nikiwa njiani kuelekea sehemu ya tukio nilipata ajali na nafasi yangu ilichukuliwa na Diana Kimaro, nakumbuka muongozaji wa filamu hiyo alikuwa Lamata na alinipa moyo sana.

‘’Sikufanya hiyo kazi lakini nilifika eneo la tukio na ndipo Lamata aliponiona na kuniambia kuwa kukosa kazi moja siyo mwisho wa kazi nyingine, maneno yake niliyapokea yalinitia moyo sikukata tamaa,” anasema.

Sophia anasema baada ya muda mfupi, alimtafuta Lamata wakakutana akamuelezea ukuaji wake na familia yake na ndipo alipopata nafasi ya kuonekana zaidi kwenye sanaa akianza na tamthiliya ya Mzazi Mwenzangu na sasa Jua Kali inayofanya vizuri kwenye DSTV.


Lamata ni mama 

Licha ya kuwa Lamata ni muongozaji wa filamu hiyo ya Jua Kali, Sophia anasema pia anamuona kama mama kwani amekuwa akiwapa ushauri wa vitu mbalimbali.

“Lamata nje ya uongozi wake kwenye kazi amekuwa mlezi anatufundisha maisha, anaishi na sisi kama ndugu tunafanya kazi kwa raha kwa sababu tupo na kiongozi wakati huohuo mzazi,” anasema na kuongeza;

“Kwa upande wangu hadi nilichukua uamuzi wa kung’oa meno ni kutokana na kupenda kazi na namna ninavyoishi vizuri na Lamata amenitoa sehemu moja kwenda nyingine, ilinipa sababu ya kuhakikisha namfanyia kitu bora kitakachotoa fundisho kwa watazamaji,” anasema.


Hamjui baba yake 

Licha ya umaarufu wake anasema hajawi kumuona baba yake kuanzia amezaliwa.
“Sijawahi kumuona baba yangu, mama yangu aliniambia alinikataa tangu nikiwa tumboni hivyo nimepambana na mama hadi hapa nilipo sasa.
“Baba yangu alinitafuta baada ya kusikia nimezaa na mtayarishaji wa muziki, siwezi kumtaja hapa akiamini kuwa sasa nina fedha lakini hakuwahi kuniona wala mimi sijawahi kumuona zaidi ya kuisikia sauti yake huenda napishana naye barabarani bila kufahamu kama ndiye mzazi wangu,” anasema muigizaji huyo.


Alivyonusurika kifo

Sophia anasema kuwa ana mshukuru Mungu kwa kuwa sasa yupo hai baada ya kunusurika kifo akiwa na mama yake.

“Ni kweli tulikuwa tunaishi Magomeni nyumba ya kupanga, nakumbuka kabla ya kulala tulikuwa tunacheza karata na mama ni mchezo ambao anaupenda, siku hiyo nilimfunga akakasirika, akalala.

“Mimi huwa sipendi kusali, lakini siku hiyo sijui ilikuwaje nilisali na ndipo nikalala haikunichukua muda kama dakika nne hadi tano nikapitiwa na usingizi, lakini dakika chache baadaye nikahisi moto mkubwa unawaka nikafungua dirisha kuchungulia ni kweli kulikuwa na moto wa kutisha nje.

“Nilichokifanya nikamkurupusha mama yangu tukatoka nje zilikuwa ni nyumba za kizamani  zile za kugawanywa kwa korido ndefu, huku vyumba na kule vyumba mama mwenye nyumba alikuwa anapaka rangi vyumba vyake akatoa vitu kwenye korido hivyo ndio vilikamata moto kwa kasi,” anasema.

Sophia anasema katika tukio hilo yeye na mama yake waliokoka lakini   mama mwenye nyumba aliteketea na kufariki humo ndani.

“Huwa sijawahi kulisahau tukio hili ni miaka minne au mitano nyuma lakini hadi leo nimekuwa nikimshukuru Mungu kwa kuendelea kunipa nafasi ya kuishi kwani kuna ambao walishindwa kutoka wakafariki mimi ni nani nisishukuru” anasema msanii huyo aliyeishia kidato cha tatu.


Filamu imempa laki 5 

Sophia anasema siyo kweli kwamba filamu zinalipa kama watu wanavyosema huko mtaani kwani amewahi kuambulia laki tano tu.

“Mimi nadhani tamthiliya ndiyo zimenipa maisha, kwa upande wa filamu fedha yangu kubwa ni laki tano ambayo nilipewa na Irene Paul, nilifanya naye kazi kwenye filamu ya kwanza kabisa, lakini awali nilishapata  laki tatu kutoka kwa 20 Pacent,” alisema.
“Lakini maisha yangu yamebadilishwa na tamthiliya napata fedha za kutosha kumudu harakati za kila siku ,” anasema.


Kisa kulia, apata laki tatu 

Nani anamkumbuka  Neema wa 20 Pacent? Unaweza kumkumbuka vizuri, basi Sophia ndiye Neema mwenyewe, sikia anavyosema jinsi alivyopatikana. Kumbe kulia napo ni dili.

“Walikuja watu wakawa wanatafuta mtoto mdogo ambaye anaweza kulia mfululizo, kuna rafiki yake mama yangu alikuja kumwambia kuhusu hilo na ndipo mama alinipeleka huko kulikuwa na watoto zaidi ya mia, lakini nilifanikiwa kupita na kutuzwa fedha nyingi tu.

“Zoezi lilitaka mtoto anayeweza kulia sana, kwa watoto wote nilishika nafasi ya kwanza na kulipwa laki tatu,” anasema.