Waandaaji Oscars wachunguza 'kibao cha Will Smith'

Muktasari:

  • Muigizaji sinema, Will Smith jana (Jumatatu) alimuomba radhi Chris Rock kwa kumzaba kibao mchekeshaji huyo, wakati waandaaji wa Tuzo za Oscars wakisema wanaanza uchunguzi wa tukio hilo.


Los Angeles, Marekani (AFP). Muigizaji sinema, Will Smith jana (Jumatatu) alimuomba radhi Chris Rock kwa kumzaba kibao mchekeshaji huyo, wakati waandaaji wa Tuzo za Oscars wakisema wanaanza uchunguzi wa tukio hilo.

Smith, ambaye alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya Muigizaji Bora, alipanda jukwaani wakati wa sherehe hiyo na kumchapa Rock kibao shavuni baada ya kufanya utani kuhusu staili ya nywele ya mkewe, Jada Pinkett Smith.

"Ningependa kuiomba radhi kwako Chris hadharani. Nilikuwa nje ya akili zangu, nilikosea. Nilinyanyaswa na kitendo changu hakikumuakisi mtu ambaye nataka niwe," aliandika nyota huyo wa filamu ya "King Richard" katika ukurasa wake wa Instagram.

"Vurugu za aina yoyote ni sumu na zinabomoa. Tabia zangu jana usiku katika sherehe za tuzo hazikubaliki na hazisameheki," alisema Smith.

"Utani kwangu ni sehemu ya kazi, lakini utani kwa hali ya afya ya Jada ulikuwa mkubwa sana kwangu kuustahimili na nilichukua hatua kwa hasira."

Jada Pinkett Smith anaugua ugonjwa wa alopecia, unaosababisha nywele kunyonyoka na Jumapili nusu ya kichwa chake ilikuw aimekatwa nywele.

Tuzo hizo za 94 zilikuwa zikielekea mwisho wakati muigizaji na mchekeshaji, Rock aliposema kuwa Pinkett Smith anaonekana kuwa tayari kwa toleo jipya la filamu ya "G.I. Jane 2" -- filamu ya matoleo mfululizo inayohusu mwanajeshi mwenye upara.

Baada ya mwanzo kuonekana anacheka, Smith alipanda jukwaani na kumnasa kibao Rock.

Baadaye alirejea kitini na kufoka kwa sauti: "Mdomo wako mchafu ukae mbali na jina la mke wangu."

Tamko la Smith limekuja saa kadhaa baada ya waandaaji wa Oscars kulaani kitendo chake na kusema wanaangalia uwezekano wa kuchukua hatua.

"Tumeanza rasmi kulirejea tukio hilo na tutaangalia hatua zaidi kwa mujibu wa sheria zetu, kanuni na Sheria ya California," taarifa inasema.

Watu maarufu kutoka Tinseltown na kwingineko walipokea tukio hilo kwa mshtuko na mshangao na wengine kulilaani.

"Angeweza kumuua. Huko ni kushindwa dhahiri kujizuia na ni vurugu," mtengenezaji filamu, Judd Apatow alisema katika akaunti yake ya Twitter na baadaye kuifuta.

Nyota wa filamu za "Star Wars", Mark Hamill alisema uchekeshaji unakuwa na ujanja sana wa kuwamudu watu wasiojizuia hasira wanapoguswa.

Wachekeshaji wengine waliungana na Rock, wakilalamikia kulipuka kwa Smith kuwa kunaweza kuamsha watu kuiga na hivyo kuwaweka hatarini wachekeshaji wengine wanapokuwa jukwaani.