Faida, hasara ongezeko la matumizi ya plastiki

“Kadiri uchumi unavyokua na matumizi ya plastiki ndivyo yanavyokua zaidi,” anasema Mchumi mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora.

Mchumi huyo alitoa maoni hayo alipoulizwa na gazeti hili juu ya kuongezeka kwa thamani ya plastiki inayoagizwa nje ya nchi. Kwa mujibu Benki Kuu ya Tanzania (BoT), thamani ya plastiki na bidhaa zake iliyoingizwa nchini mwaka 2022/23 ilikuwa Sh1.678 trilioni.

Hilo ni ongezeko la asilimia 57 ikilinganishwa na Sh1.066 trilioni mwaka 2019/20 na ongezeko la asilimia 72 kati ya mwaka 2021/22 ambapo thamani yake ilikuwa Sh1.833 trilioni.

Ongezeko la plastiki linatokea licha dunia, ikiwepo Tanzania kujiunga kwa pamoja kupunguza matumizi ya plastiki kwa sababu za kimazingira, kama kuharibu bayoanuai ya bahari na ardhi, afya ya binadamu na wanyama na mabadiliko ya tabianchi.

Profesa Kamuzora alisema bunifu za plastiki zimekua kwa kasi na kugusa matumizi sehemu nyingi kabla ya dunia haijajua madhara yake. “Dunia imeshituka baadaye kuhusu madhara. Plastiki inatumika kwenye nguo, vyombo, magari yetu mengi yanatengenezwa plastiki ngumu, sasa fikiri mbadala wake ni nini,” alihoji.

Mhadhiri mwingine wa uchumi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Timoth Lyanga anasema ongezeko la plastiki inayoingia nchini ni ishara kuwa malighafi hiyo inakuza uendeshwaji wa sekta za viwanda na sekta nyingine kama za ujenzi.

“Viwanda mfano vya vifaa vya ujenzi vinatumia malighafi hiyo kwa kiwango kikubwa, hususan kwenye utengenezaji wa bidhaa kama mabomba ya aina mbalimbali, vifaa vya kuhifadhia bidhaa nyingine kama saruji, jambo linaloashiria muunganiko na ukuaji wa sekta mbalimbali,” anasema.

Dk Lyanga anasema kukua kwa sekta hizo kunaashiria kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za kijamii na ukuaji wa uchumi wa watu. Hata hivyo, mchumi huyo anasema jambo la muhimu kuzingatia ni aina zipo nyingi za plastiki.

Mchechemuzi wa mabadiliko ya tabianchi kwenye mitandao ya kijamii, Baraka Machumu anasema kuna uingiliaji kwa sababu nchi zinazotuzunguka nyingi bado hazijaweka marufuku au usimamizi bado, hivyo ni vigumu kuzuia hata nchini.

“Nchi jirani kama Burundi, Rwanda na DR Congo hawana marufuku ya uwindaji wa wanyamapori kama Kenya, inavyofanya. Muingiliano wa mipaka huleta changamoto, na ni muhimu kushirikiana kwa utekelezaji wa marufuku hizi kwa faida ya nchi zote,” alisema.
 

Marufuku ya plastiki Tanzania

Marekebisho ya kanuni za Usimamizi wa mazingira (marufuku wa matumizi ya mifuko ya plastiki na mifuniko/vizibo ya chupa za plastiki) ya mwaka 2022 yalitia mkazo wa aina na matumizi ya plastiki yanayoruhusiwa, ikifafanua kwa undani kanuni za mwaka 2019.

Kanuni hizo kifungu cha saba zinasema, “Mifuko yote ya plastiki, bila kujali unene wake, hairuhusiwi kuingizwa, kusafirishwa, kutengenezwa, kuuzwa, kuhifadhiwa, kusambazwa na kutumika Tanzania Bara”.

“Mtu (mtu binafsi au taasisi) haruhusiwi kuuza au kutoa kwa ajili ya kuuza vinywaji au bidhaa zilizofungwa kwa plastiki isipokuwa aina ya bidhaa hizo ni lazima zihifadhiwe kwa njia hiyo,” inasema sehemu ya saba ya kanuni hizo.

Akifafanua kuhusu plastiki iliyokatazwa kwa matumizi, Ofisa Mwandamizi kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Arnold Mapinduzi anasema sheria hairuhusu matumizi ya mifuko yoyote ya plastiki kuuzwa au kutumika kwa mifuko yote yenye mishikio au isiyo na mishikio kwa bidhaa ambazo sio lazima zihifadhiwe hivyo.

“Kilichoruhusiwa ni vifungashio vya plastiki kwa bidhaa zenye ulazima wa kufungashwa kwenye vifungashio zilizotengenezwa kwa malighafi za plastiki, lengo ni bidhaa hizo zisiharibike kabla hazijafika kwa mlaji au kuharibika kabla ya muda wake uliokusudiwa. Ili kulinda ubora wa bidhaa,” anasisitiza.

Mapinduzi anafafanua kuwa kifungashio lengo lake ni kufunga bidhaa ifike sokoni, sio kufungashia pale sokoni au buchani.

“… ukifanya pale sokoni au buchani hicho ni kibebeo umembebesha na hilo ni haramu, sheria imekataza,” alisema.

“Vilevile kifungashio lazima kionyeshe nani aliyefungashia hiyo bidhaa ili kukiwa na tatizo tupate nani wa kumtafuta ili watu wapate haki zao,” anasema Mapinduzi.
“Kionyeshe uwezo wa kubeba ni kiasi gani na kinaisha lini matumizi yake, lakini hivi ambavyo tunabebeshwa nyama, karoti, njegere kule sokoni havifai na sheria inasema ni kosa kubadili kifungashio kuwa kibebeo”.

Ofisa huyo alisema Kamati za mazingira na maofisa mazingira wana jukumu kubwa la kusimamia haya kwa mujibu wa sheria na kiongozi wa hawa ni wakurugenzi wa halmashauri. Watu hawa wanatakiwa wafanye kazi kwa pamoja na kunapotokea kuhitaji usaidizi NEMC ipo.
 

Mbadala, suluhu ya plastiki

Profesa Kamuzora alisema matumizi yake ni makubwa na mbadala ni mgumu. Akitoa baadhi ya mbadala kwa plastiki tena kwa baadhi ya bidhaa anasema ni kama katani inayotumika kutengeneza nguo, kamba, vibebeo lakini alihoji uwepo wake kama nchi ipo tayari kuendeleza teknolojia hiyo.

Anatoa mfano, “…kama sasa Serikali imepiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki katika jitihada za kupunguza matumizi ya plastiki lakini mbadala wa hayo ni mgumu”.
Profesa Kamuzora anashauri kuwekeza kwenye tafiti na kuendeleza teknolojia zilizokuwa zikitumiwa na wazee kama utengenezaji wa vikapu, mazulia na vibebeo vinavyotengenezwa na majani.

“Hapa Serikali ilitakiwa kutafiti katika majani haya na kuwekeza na baadaye kuweza kada kwenye vyuo vya ufundi za ufundishaji stadi hizi. Hapo Serikali inaanza uzalishaji mkubwa wa bidhaa hizi,” anasema na kutoa mfano wa nchi kama China zilizoendeleza teknolojia ya dawa kutoka kwa watu wao wa zamani.

Anaongeza kuwa kuachana moja kwa moja na bidhaa hizi bila mkakati ni sawa na makatazo yanayotolewa na wataalamu wa afya juu ya kula vyakula fulani bila kuwapa watu mbadala wao.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utu na Mazingira (HUDEFO), Sarah Pima alisema maboresho ya sheria za mazingira yatasaidia kuthibiti uzalishaji wa plastiki.

“Tuna imani sasa mwongozo wa kuwawajibisha wa wazalishaji plastiki kuhusika kwenye kurejeleza utasaidia kwenye vita hii,” alisema na kukumbusha Serikali iliwataka wazalishaji wa chupa za plastiki wote nchini kuhakikisha wanashiriki katika kurejeleza.
Maelekezo haya yalitolewa na NEMC na yanatarajia kuisha Machi, 2024.
 

Hasara za plastiki kwenye bioanuai, Afya na Uchumi

Sheria ya usimamizi wa mazingira ya 2004 kifungu cha sita, “Mtu yeyote anayeishi Tanzania atakuwa mdau na atawajibika kutunza na kuendeleza mazingira na kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu shughuli au jambo lolote ambalo kwa kiasi kikubwa linaweza kuathiri mazingira”.

Tafiti ya 2017 yenye jina “Uzalishaji, matumizi, na hatima ya plastiki zote zilizowahi kutengenezwa” ya wasomi wa Marekani inasemea uzalishaji na utupaji wa plastiki unachangia mabadiliko ya tabianchi kupitia uzalishaji wa gesi joto kwa sababu inatokana na nishati kisukuku (Fossil fuel).

“Mchakato wa kutengeneza plastiki unahitaji nishati nyingi, na utupaji mbaya wa plastiki husababisha kutoa hewa ya kaboni na methane. Uchafuzi wa plastiki unaharibu baoanuai, ukiathiri michakato asilia inayosaidia kudhibiti hali ya hewa” inasema tafiti hiyo.

Hata hivyo, Mapinduzi anasema pia zipo tafiti zinazonyesha tani milioni 8 hadi 10 zinaingia baharini kila mwaka na tafiti hizo zinaelekeza hadi 2050 plastiki itakuwa nyingi zaidi kuliko samaki kwenye maji.

“Zipo kesi za kuonyesha samaki wanakufa kwa kula au kukosa hewa kutokana na plastiki” alisema na kufafanua sekta hizo muhimu za kiuchumi zinazotegemewa na watu wengi zitakuwa kwenye shaka.

Sio tu kuagiza lakini sasa hivi bidhaa zilizotengenezwa kwa plastiki zimeongezeka mfano ni viti ambavyo havikuwepo zamani… hivyo ni changamoto na usimamizi wake sio rahisi.

“Hakuna matatizo na bidhaa ambazo zinaweza kurejelezwa kwa urahisi ila tatizo nihizi nyingine ambazo ndizo zinazagaa mitaani, zinaziba mitaro kinachoziba kule ni plastiki ukiachana na uwezo wa miundombinu hiyo hata kwenye mifumo ya majitaka ukifuatilia ni plastiki,” alifafanua.

Ukiacha athari hizo suala jingine ni madhara ya kiafya na plastiki yoyote ikiingia kwenye mwili wa binadamu au mnyama haimeng’enywi.

“…tumepata kesi wakimeza kama wanyama lazima watakufa… hata ikiingia kwenye tumbo la binadamu havimeng’enyi vikaisha na vinaweza kubaki na kurithiwa na kwenda kwenye mifumo mingine ya mwili,” alisema.

Zipo tafiti zinaonyesha wamekuta chembechembe ndogondogo za plastiki kwenye maziwa ya mama, na nyingine kwenye mkojo wa binadamu kuanzia miaka nane na kuendelea.

Kuna kemikali sumu inayoshika plastiki ambayo inafanya isitoe hewa inapoingia kwenye mfumo ya mwili wa binadamu au wanyama inaanza kujenga na ndio unasikia kesi ya saratani, na huathiri pia mfumo ya uzazi.

“Sasa hatutaki kuwa na Taifa lisilo na nguvu kazi, au haliwezi kuzalisha na kuwa na taifa lenye watu mizigo kwa magonjwa mengi na unakuta bajeti ya wizara inatumika kwenye tiba na kuhudumia haya badala ya kwenda maeneo mengine” anasema.

Kwa mujibu wa wizara ya Afya kwa mwaka taasisi ya Saratani ya Ocean Road ilisamehe Sh37.29 bilioni kwa baadhi ya wagonjwa waliotibiwa 2022/23 kwenye Taasisi ya saratani ya Ocean Road na Sh13.9 bilioni mwaka 2021/22.

Ocean Road ilihudumia jumla ya wagonjwa 43,922 ikilinganishwa na wagonjwa 37,882 katika kipindi hicho.