Zungu ataka Takukuru ichunguze wanufaika Tasaf

Muktasari:

Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu asema wapo watu wanaowachomeka majina ya ndugu zao kama wanufaika wa wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).

Dodoma. Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu ameagiza Serikali kupeleka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza uwepo wa watu walioingiza ndugu zao kama wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), jijini Dar es Salaam.

Zungu amesema hayo leo Jumatano Aprili 17, 2024 baada ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete kujibu maswali ya nyongeza ya Rehema Migilla, mbunge wa Ulyankulu.

Migilla amehoji, Serikali ina mpango gani wa kuongeza kiwango inachotoa kwa kaya masikini kutoka Sh20, 000 za sasa ili watu hao waweze kujikimu kulingana na hali ya uchumi.

Pia amehoji, “je Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wale wote waliorukwa kipindi cha utambuzi wanaingizwa kwenye mpango wa kusaidia kaya masikini?”

Akijibu maswali hayo, Ridhiwani amesema nia ya Serikali ni kuona malipo ya wanufaika yanakuwa makubwa lakini mpango huo umekuwa ukitelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wahisani ambao huingiza zaidi ya asilimia 60 kwenye mfuko huo.

Amesema lengo ni kusaidia kutatua tatizo la umasikini uliokidhiri nchini.

“Maboresho yanayofanyika ni sehemu ya kuona mfuko unapanuliwa au fedha zinaongezeka zaidi ili kufikia malengo ambayo Bunge lako na wananchi wangetamani tufikie,” amesema.

Amesema Serikali inaendelea kufanya mazungumzo na wahisani, lengo likiwa ni kuona fedha hizo zinaongezeka ili ikiwezekana zitoke Sh20, 000 kwenda hata Sh100,000.

Amesema shehia au mtaa ndiyo inayotumika kutambua wahusika na baada ya utambuzi kamati hukaa kutambua kama waliotajwa ni wahusika kweli au wamechomekwa.

Amesema baada ya kukamilika, hubandikwa majina ya watu wote na wale ambao hawajaridhika kwa kuenguliwa. Upo pia utaratibu wa kukata rufaa.


Baada ya kujibu swali hilo, Zungu amesema bado watu wanachomekwa na kutoa mfano wa Kata ya Ilala kuna mama mwenye umri wa miaka zaidi 70 hajaingizwa kwenye wanufaika wa mfuko huo.

Zungu ambaye ni mbunge wa Ilala amesema wameingizwa watu wengine wenye umri mdogo na rufaa ilikatwa lakini amekataliwa.

Kwa mtazamo wa Zungu, hilo linawezekana likawepo nchi nzima.

“Msiharibu nia njema ya Serikali kwa watu ambao wanaingiza ndugu zao kwa masilahi ya pesa ambazo zinawalenga wazee,” amesema.

Akijibu hoja hiyo, Ridhiwani amesema wamesikia na watalifanyia kazi suala hilo.

Kwa majibu hayo, Zungu amesema: “Eeh! pelekeni na Takukuru wakachunguze Kata ya Ilala, Mtaa wa Sharifu Shamba.”

Katika swali la msingi, mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka alihoji Serikali inafanya juhudi gani kuboresha Tasaf kwa wasiojiweza.

Akijibu swali hilo, Ridhiwani amesema Serikali imeendelea kuboresha mfuko huo kwa kutekeleza mambo mbalimbali.

Amesema maboresho hayo ni kutanua wigo wa maeneo ya utekelezaji wa mpango kutoka halmashauri 42 kwa awamu ya kwanza hadi halmashauri zote nchi nzima katika awamu ya tatu.

Ridhiwani amesema wanafanya uboreshaji wa taratibu za utambuzi wa walengwa, katika awamu tatu za utekelezaji wa Tasaf uliwezesha kutambuliwa kwa kaya milioni 1.2, sawa na asilimia 86 ya kaya katika ama vijiji, mitaa au shehia zote nchini ambao ni ongezeko kubwa la walengwa.

Amesema aina na afua za miradi zimeboreshwa kwa kulenga kuwainua wananchi kiuchumi.

“Mathalani awamu ya kwanza ililenga ujenzi wa miundombinu ya huduma za jamii, awamu ya pili iliendeleza ujenzi wa miundombinu na miradi ya kuongeza kipato kwa makundi maalumu, na awamu ya tatu miradi imelenga mpango wa kunusuru kaya masikini zaidi,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kufanya maboresho ya Tasaf ili kuhakikisha manufaa makubwa yanaendelea kuwakwamua wananchi wasiojiweza kiuchumi ili kuondokana na umasikini uliokithiri.