Bei ya viazi mbatata yapaa Morogoro

Magunia ya viazi mbatata kutoka  Mbeya yakiwa katika Soko la Mawenzi. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

Viazi mbatata ni zao linalolimwa msimu mzima wa mwaka mkoani Mbeya

Morogoro.  Kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Jijini Mbeya zimesababisha bei ya viazi mbatata katika masoko mbalimbali ya Manispaa ya Morogoro kupanda bei kutoka Sh58,000 kwa gunia hadi Sh73,000.                                                                                                       Pia, bei ya kipimo cha sado cha viazi mbatata ni kati ya Sh4,000 na Sh6,000

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Aprili 16, 2024, mfanyabiashara wa viazi wa Soko la Mawenzi mjini Morogoro, Halima Haruna amesema bei imepanda baada ya kuharibika kwa miundombinu ya barabara na madaraja kwenye maeneo yanayolima viazi hasa mkoani Mbeya.

Halima  amesema usafirishaji wa zao hilo umekuwa mgumu hasa kutoka shambani na kupeleka sokoni.

Amesema kwa sasa barabara nyingi za shamba zimekatika na zingine zinapitikana kwa shida.

“Magari yanakwama, yanachukua muda mrefu barabarani, na hata viazi vyenyewe vikifika sokoni vingi vinakuwa vimeharibika, kwa hiyo tunaopata hasara ni sisi tunaoagiza mzigo ambao mara nyingi huwa tunaulipia kabisa,” amesema Halima.

Akizungumzia msimu wa uzalishaji, amesema hivi sasa viazi mbatata vinalimwa msimu mzima wa mwaka, “havina msimu hivi viazi, sasa hivi vinapatikana kwa shida kwa sababu ya uharibifu wa barabara tu.”

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Umoja wa Wauza viazi mbatata Soko la Mawenzi, Thomas Kabogo amesema pamoja na kuharibika Kwa miundombinu bei ya bidhaa hiyo imepanda baada ya baadhi ya wafanyabiashara kutoka Zanzibar kwenda kuvinunua moja kwa moja shambani kwa bei ya juu.

"Wakulima nao wanawakimbilia hawa wafanyabiashara kutoka Pemba kwa sababu wananunua kwa bei kubwa, tunasikia huko Pemba na Unguja viazi vinauzwa bei ya juu sana, sasa sisi wafanyabiashara wa Morogoro na mikoa mingine tunalazimika kununua kulingana na bei wanayokuja nayo wenzetu kutoka Zanzibar," amesema Kabogo.

Kabogo amesema bei ya viazi shambani kwa sasa ni Sh58,000 hadi Sh60,000 kwa gunia na hata ubora wa viazi nao umekuwa mdogo kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Mfanyabiashara wa chipsi anayefanya biashara eneo la Barabara ya Kitope, Mwasiti Lindiati amesema kutokana na kupanda kwa bei ya viazi analazimika kupandisha bei ya chipsi kavu kutoka Sh1,000 na sasa anauza Sh1,500 kwa sahani moja.

"Zamani kabla ya kupanda Kwa viazi nilikuwa nauza chipsi Sh1,000 kwa sahani, lakini kwa sasa bei hiyo siuzi, na hata hizo chipsi za Sh1,500 nimelazimika kupunguza kipimo," amesema Mwasiti.