Kilio cha wabunge, wakulima kuhusu ushuru wa korosho chasikika

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akizungumza na wadau wa korosho nchini.

Muktasari:

  •  Juni 28, 2018, Serikali ya Tanzania ilibadilisha kufungu cha 17A cha Sheria ya Sekta ya Korosho ili kuruhusu ushuru unaotokana na mauzo ya korosho ghafi nje ya nchi kuingizwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali

Dodoma. Kilio cha wabunge wa Tanzania cha kurejesha asilimia 65 ya ushuru wa mauzo ya nje ya korosho ghafi kwenye Mfuko wa Kuendeleza zao hilo, kimesikika baada ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kutamka majadiliano yanaendelea vizuri.

Pia, Bashe amesema katika mazungumzo ya awali, Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia suala hilo.

Juni 28, 2018, Serikali ilibadilisha kufungu cha 17A cha Sheria ya Sekta ya Korosho ili kuruhusu ushuru unaotokana na mauzo ya korosho ghafi nje ya nchi kuingizwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Akizungumza katika mkutano wa Bodi ya Korosho, (CBT) leo Ijumaa, Aprili 26, 2024 uliowashirikisha wadau wa korosho nchini, Bashe amesema wamepeleka maombi katika Wizara ya Fedha kutaka ushuru huo wanaoupata kwa asilimia 50, waupate kwa asilimia 100 kwa kuwa ni fedha ya wakulima.

“Majadiliano yangu na Wizara ya Fedha yanaendelea vizuri. Kwanini tunataka Exporty Levy asilimia 100, tunataka mfumo wa ruzuku na ruzuku ya pembejeo kwa wakulima wakorosho iendelee hela ya export levy sio ya kujenga madarasa,” amesema.

Amesema anaamini katika mabadiliko ya sheria watafanikiwa na kwamba akikwama atarejea kwa wabunge.

Bashe amesema anashukuru Mungu Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imebeba ajenda kama ajenda yao na kuwa alipeleka hoja kwao, wakamuelewa na kuibeba kama hoja yao.

“Hakuna mkulima masikini anayeweza kuendesha zao la korosho kwa kujigharamia mwenyewe, ni lazima mkono wa Serikali uwepo na nataka kuwaambia katika mazungumzo ya awali mheshimiwa Rais ameridhia, ameelewa,” amesema Bashe.

Amesema wamekubaliana asilimia 50 ya ushuru huo, utalipa madeni ya pembejeo yaliyopo hadi msimu huu.

Bashe  amesema kiasi kilichobakia kitaendelea kutolewa kama ruzuku ya pembejeo hadi madeni hayo yatakapoisha kisha kiasi chote asilimia 100 kitakwenda na kitatumika katika kuendeleza zao la korosho.

Amesema sasa majadiliano yako kati ya Wizara ya Fedha na Wizara ya Kilimo juu ya utekelezaji wa jambo hilo.


Walichokisema wabunge na wakulima

Mkulima wa zao hilo, Muhamed Sadala amesema kutokuwepo kwa ushuru wote katika mfuko huo, kumewafanya kupata pembejeo zisizotosheleza mahitaji yao ya kilimo.

“Kama watarejesha kutainua kwa kiasi kikubwa zao hili maana kama ulikuwa ukihitaji mifuko 20 ya mbolea sasa utapata yote,”amesema.

Mkulima mwingine wa Wilaya ya Newala mkoani Mtwara, Bushia Pannali amesema pamoja na kurejesha kiasi chote cha ushuru katika mfuko wa kuendeleza zao hilo, ni vyema pembejeo sasa zikawafikia kwa wakati.

“Sisi hapa kwetu Septemba korosho zinaanza kudondoka kwa hiyo kama ni pembejeo tunatakiwa kupata mapema Mei ili tupate tija katika kilimo,”amesema.

Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota amesema Serikali ya awamu ya tano ilifuta fedha zote lakini alipokuja Rais Samia kwa kuona umuhimu wa suala hilo, alirejesha asilimia 50 ya ushuru huo kwenye mfuko wa kuendeleza zao hilo.

“Zao la korosho linahitaji uwekezaji mkubwa, zile fedha zitasaidia katika utafiti, itasaidia maofisa ugani, kununua pembejeo na viwatilifu, zitalipa madeni ya viwatilifu na pembejeo na vifungashio vya miaka iliyopita. Kwa sababu kila mwaka ulikuwa ukiisha na madeni,”amesema.

Amesema ikienda fedha yote kwenye mfuko huo itakwenda kupunguza madeni, kuendeleza sekta hiyo na kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Takwimu zilizopo Wizara ya Kilimo zinaonyesha kwa mwaka huu uzalishaji umefikia tani 305, 000.

“Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa ukiongeza upatikanaji wa viatilifu na uzalishaji utaongezeka,”amesema.

Mbunge wa Ndanda (CCM), Cecil Mwambe amesema wakulima wenyewe waliona kuna haja ya kuweka vivutio kwa watu wanataka kujenga viwanda nchini na kuwavunja moyo wanunuzi kupeleka nje ya nchi korosho ghafi hivyo kuamua kuweka ushuru huo.

“Kurejeshwa kwa fedha hizo kutafanya mkulima au mnunuzi asikatwe tena fedha za pembejeo na fedha yote itatumika kwenda kununua viatilifu na pembejeo za korosho. Hiyo fedha ilikuwa ya wakulima kwa hiyo hata Serikali ilivyochukua ilikuwa inawakosea wakulima,”amesema.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Amesema itapunguzwa tozo walizokuwa wakitozwa wakulima na wanunuzi kugharamia pembejeo.

Amesema mnunuzi alikuwa akikatwa Sh110 kwa kila kilo kwa ajili ya kugharamia pembejeo na kinachobakia kinachangiwa na Serikali.

Mwambe amesema kwa sababu wanakwenda kurejesha ushuru huo wao watashauri Serikali isimkate tena mnunuzi badala yake fedha hiyo iende kwa mkulima ili kuongeza mapato.

Kwa mujibu wa aliyekuwa Waziri wa Fedha ambaye sasa ni Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango lengo lilikuwa ni kuyafanya makusanyo hayo kuwa ni sehemu ya mapato ya Mfuko Mkuu wa Serikali.

Fedha hizo zilikuwa zikipelekwa katika Mfuko wa Kuendeleza zao la Korosho pamoja na gjharama za uendeshaji wa bodi ya korosho.

Hatua hiyo ya kuondoa asilimia 65 ya mapato yanayotokana na mauzo ya zao hilo, ilileta mjadala mkali ndani nan je ya Bunge, ukitafisiriwa kuwa litarudisha nyuma zao hilo ambalo linahitaji uwekezaji mkubwa.

Mjadala huo kati ya Serikali na wabunge, ulianzia kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ambayo wakati huo ikiongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia.

Hata hivyo, Serikali katika Muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2023, Serikali ilirejesha asilimia 50 ya fedha hizo kwenye mfuko wa kuendeleza zao hilo.