#LIVE: Miili ya wanafunzi ikiagwa Arusha

Muktasari:

  • Wanafunzi wanaoagwa ni Winfrida Emanuel aliyekuwa anasoma awali, Abigail Peter  darasa la sita, Abialbol Peter (awali), Morgan Emanuel (awali), Articia Emanuel darasa la tatu, Shedrack Emanuel  darasa la sita, Dylan Jeremiah, Noela Jonas (awali) na Brian Tarangie


  • Wanafunzi na muokoaji walifariki dunia baada ya gari la shule hiyo lenye namba za usajili T 496 EFK kutumbukia kwenye korongo lililokuwa limejaa maji Mtaa wa Engosengiu, alfariji ya Aprili 12, 2024.

Update: Saa 8.14 mchana

Waombolezaji wakiaga miili ya wanafunzi nane wa Shule ya Msingi Ghati Memorial iliyopo jijini Arusha na muokoaji mmoja waliokufa maji Aprili 12, 2024. Picha na Bertha Ismail


Update: Saa 8.00 mchana

Askofu Isack Amani wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha akibariki miili ya wanafunzi nane wa Shule ya Ghati Memorial jijini Arusha waliokufa maji Aprili 12, 2024. Picha na Janeth Mushi

Update: Saa 7.34 mchana

Arusha. Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa akitoa mkono wa pole wa Sh5 milioni kwa famiia ya msamaria mwema Brian Tarangie aliyefariki dunia alipokuwa akiwaokoa wanafunzi wa Shule ya Msingi Ghati Memorial.

Mkono huo wa pole umetolewa na Mtahengerwa kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Picha na Janeth Mushi


Update: Saa 6.10 mchana

Simanzi, majonzi na vilio vimetawala katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Sinoni jijini Arusha baada ya kuwasili miili tisa  ikiwamo  minane ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Ghati Memorial, waliofariki kwenye ajali baada ya gari la shule walilokuwamo kutumbukia kwenye korongo  lililojaa maji.

Mamia ya wananchi wamejitokeza leo Jumapili Aprili 14, 2024, kuaga miili hiyo ya watoto waliofariki kwenye ajali hiyo ya Aprili 12, 2024 pamoja na mtu mmoja aliyekuwa akijaribu kuwaokoa wanafunzi hao.

Baadhi ya wazazi na walezi wa wanafunzi wanane waliokuwa wakisoma Shule ya Msingi Ghati Memorial wakiomboleza katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Sinoni leo Jumapili Aprili 14, 2024. Picha na Janeth Mushi

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa anaongoza mamia ya waombolezaji waliojitokeza kuaga miili hiyo wakiwamo wazazi wa wanafunzi hao na wanajumuiya ya shule waliyokuwa wanasoma wanafunzi hao.

Wanafunzi wanaoagwa ni Winfrida Emanuel aliyekuwa anasoma awali, Abigail Peter  darasa la sita, Abialbol Peter (awali), Morgan Emanuel (awali), Articia Emanuel darasa la tatu, Shedrack Emanuel  darasa la sita, Dylan Jeremiah, Noela Jonas (awali) na Brian Tarangie. Miili hiyo iliwasili uwanjani hapo saa 5:32 asubuhi na kabla ya kushushwa kwenye gari, wazazi wao walitangulia.

Baada ya wazazi hao kukaa katika sehemu maalumu iliyoandaliwa kwa ajili yao, miili hiyo ilianza kushushwa katika viwanja hivyo, huku wazazi wakisikika kuita watoto wao kwa uchungu pale ilipokuwa ikitajwa kwa majina wakati wanashushwa.

Katika tukio hilo, familia mbili zimebaki na upweke baada ya kila moja kupoteza watoto wawili pekee waliokuwa nao.

Kabla ya kuagwa kwa miili hiyo, ibada maalumu inatarajiwa kufanyika uwanjani hapo, kisha kuchukuliwa na familia zao kwa ajili ya mazishi.


Update: Saa 4 asubuhi

Miili minane ya wanafunzi waliokuwa wakisoma katika Shule ya Msingi Ghati Memorial na mmoja wa muokoaji aliyejaribu kuwasaidia wanafunzi hao katika ajali, inatarajiwa kuagwa leo Aprili 14, 2024 katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Sinoni.

Wanafunzi na muokoaji huyo walifariki dunia baada ya gari la shule hiyo lenye namba za usajili T 496 EFK kutumbukia kwenye korongo lililokuwa limejaa maji Mtaa wa Engosengiu, alfariji ya Aprili 12, 2024.

Waliofariki katika ajali hiyo ni Winfrida Emanuel aliyekuwa anasoma darasa la awali, Abigail Peter  darasa la sita, Abialbol Peter (awali), Morgan Emanuel (awali), Articia Emanuel darasa la tatu, Shedrack Emanuel  darasa la sita, Dylan Jeremiah, Noela Jonas (awali) na Brian Tarangie ambaye alikuwa anawaokoa watoto hao.

Leo katika viwanja hiyo inatarajiwa kufanyika ibada ya kuwaaga huku waombolezaji wakiwa wameshawasili ikiwamo familia za watoto hao na viongozi wa dini huku miili hiyo ikiwa inasubiriwa kuwasili.

Vifo vya watu hao vimekuwa ni pigo kubwa kwa familia zao kwa kuwapoteza wapendwa wao katika ajali iliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini huku zikileta maafa na uharibifu wa miundombinu.

Katika ajali hiyo, mashuhuda wanasimulia kwamba gari hilo lilikuwa likipita kuwachukua wanafunzi majumbani mwao na lilipofika eneo la Dampo, walikuta limejaa maji lakini dereva akaamua kupita kabla ya kuzidiwa na maji hayo na gari kuangukia kwenye korongo.

Wanafunzi walionusurika kwenye ajali hiyo wanasimulia kwamba dereva wa gari hilo alidharau ushauri wa mwalimu aliyekuwamo kwenye gari hilo wa kumtaka kutopita kwa kuwa maji yalikuwa mengi, lakini alilazimisha, akapita.

“Kilichosababisha gari letu kusombwa na maji ni anko (dereva) kudharau maneno ya Matroni wetu aliyemuonya asipite baada ya kukuta maji yameongezeka tofauti na mwanzo tulivyopita lakini alimgeukia akacheka na akaendelea na safari,” alisimulia mwanafunzi, Glory Daniel (8). 

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa alisema ajali hiyo imetokana na uzembe wa dereva kudharau maji yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku jijini Arusha na kuelekeza maji yake katika njia mbalimbali ikiwAmo katika korongo hilo la Sinoni.

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo kutoka Jeshi la Polisi Tanzania, Awadh Haji alisema wanamshikilia dereva wa gari hilo kwa uzembe wake.


Endelea kubaki hapa kwa taarifa zaidi