‘Serikali iboreshe mifumo kudhibiti fedha za umma’

Muktasari:

  • Serikali imetakiwa kuboresha mifumo ya kusimamia na kudhibiti fedha za umma, ili kudhibiti mianya ya ubadhirifu ulioibuka katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Dar es Salaam. Serikali imetakiwa kuboresha mifumo ya kusimamia na kudhibiti fedha za umma, ili kudhibiti mianya ya ubadhirifu ulioibuka katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Hayo yamesemwa leo Novemba 8 na Mhariri wa siasa wa gazeti la Mwananchi, Peter Elias leo Jumatano Novemba 8, 2023 wakati akifungua mada ya Mwananchi Space inayosema ‘Nini kitarajiwe kuhusu ripoti ya CAG baada ya maazimio ya Bunge?’

“Natarajia kuona Serikali ikiweka mifumo wa kudhibiti fedha za umma mifumo ipo lakini baadhi ya watu wanatumia vibaya, hili azimio la Bunge ninaamini jambo hili liwe endelevu, mifumo ijiendeshe yenyewe kuweza kudhibiti upotevu wa mapato ya umma,” amesema.

Amesema anaamini azimio lililotolewa na Bunge la Tanzania litaiamsha Serikali kutengeneza mifumo imara ya udhibiti wa fedha za umma.

Peter amesema Serikali inapaswa itekeleze kama ambavyo imeazimiwa na Bunge kwa kuwa mambo yamebadilika ikilinganishwa na mwaka 2019 ambapo Bunge iliingia mgogoro na Profesa Mussa Assad aliyekuwa CAG wakati huo ikilinganishwa na sasa.

“Bunge limetoa azimio jingine waliotajwa wanapaswa kuwajibika, mimi binafsi natarajia kuona wahusika wakiachia nafasi zao. Kwa Watanzania utamaduni wa kujiuzuru bado haupo wanatarajia kutenguliwa wanapaswa wajitathmini wenyewe au wajiuzuru mpaka Februari 2024 Serikali iwasilishe Bungeni katika utekelezaji wa hili,” amesema.

Peter amesema Serikali inapaswa kuanzisha uchunguzi dhidi ya wahusika kuangalia namna ya kurejesha fedha za umma zilizopotea.

“Tunategemea wapo wazembe waliotumia madaraka vibaya na upotevu wa fedha kwa namna yoyote Serikali ingalie namna ya kurudisha hizo fedha na hatua za kisheria zichukuliwe ni masuala ya jinai isiishie kujiuzuru hatua kali zichukuliwe iwe fundisho kwa viongozi wengine wanaopata dhamana,” amesema Peter.

Amependekeza kuwa ukaguzi wa CAG kutanua mawanda mapana kufika maeneo ambayo hafiki na kwamba anachokiangazia CAG ndiyo jicho la Bunge kufanya azimio, bila yeye Bunge halina meno.

“Kilichofanywa kilitarajiwa na wengi wangependa kuona Bunge linasimamia rasilimali za Taifa na si kuwa sehemu ya serikali,” amesema.