Wakili wa kujitegemea Oscar Ngole akutwa amefariki dunia nyumbani kwake Moshi

Wakili Oscar Ngole enzi za uhai wake

Muktasari:

  • Aliwahi kuwa wakili wa Serikali, wenzake wasimulia walivyokutana wiki iliyopita

Moshi. Wakili wa kujitegemea Mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, Oscar Ngole amekutwa amefariki dunia nyumbani kwake Soweto.

Omega Ngole, kaka wa marehemu Oscar (42) amethibithisha kifo cha ndugu yake ambaye awali aliwahi kuwa Mwanasheria wa Serikali.

Aliondoka kwenye nafasi ya wakili wa Serikali mwaka 2011 na kuwa wakili wa kujitegemea.

Amesema Oscar amefariki dunia jioni ya Mei 7, 2024 akiwa nyumbani kwake.

Kuhusu sababu za kifo amesema mwili upo Hospitali ya St. Joseph, iliyopo Kata ya Soweto, Manispaa ya Moshi kwa uchunguzi zaidi na kwamba, madaktari ndiyo watakaothibitisha sababu za kifo chake.

"Amefariki jana jioni, hivi sasa tunaandaa taratibu za mazishi na tutaenda kumpumzisha mkoani Njombe. Tutamzika Jumamosi, Mei 11," amesema Omega.

"Niko njiani nakuja Moshi nikifika madaktari watatuambia sababu za kifo chake ni nini, maana ndio wanafanyia kazi," amesema. 

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Kanda ya Kilimanjaro, Philip Njau amesema kifo cha ghafla cha wakili huyo kimewashtua.

Amesema wiki iliyopita walikuwa naye mahakamani.

"Tumepokea kwa masikitiko kifo cha mwenzetu, wiki iliyopita tulikuwa naye mahakamani alikuwa ni mzima, taarifa ya kifo chake kwa kweli zimetushtua na hatujui ni kitu gani ambacho kimetokea," amesema.

"Alikuwa ni Mwanasheria wa Serikali, na amekaa hapa Moshi kwa muda mrefu,  baadaye alivyoacha akaingia kwenye uwakili wa kujitegemea, tukawa naye hapa mkoani Kilimanjaro kwa muda mrefu, tumeshirikiana kwenye kazi," amesema.

Mwanasheria wa Serikali Mkoa wa Kilimanjaro, Tamari Mndeme amesema Oscar alikuwa wakili mzuri walipokuwa wakifanya kazi pamoja na kwamba, alikuwa akifanya kazi kwa weledi mkubwa.

"Tumesikitika kwa namna ambavyo tumesikia msiba ulivyotokea, hatukutegemea hivyo, maana amekufa ghafla, lakini ndiyo hivyo kazi ya Mungu haina makosa, tutamkumbuka," amesema.

"Alikuwa ni wakili mzuri wa Serikali na tumefanya naye kazi, ni mtu aliyekuwa akijituma na alifanya kazi kwa weledi," amesema.