Watu 1,530 wajitokeza kliniki ya madaktari bingwa Morogoro

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro wa (kushoto) Daniel Nkungu akiwa na Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi (katikati) wakati wakizungumza na vyombo vya habari. Picha na Johnson James

Muktasari:

  • Baadhi ya wagonjwa  ni wale waliohitaji kufunga safari kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili

Morogoro. Mganga kiongozi wa kliniki ya madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo, figo, tumbo, pua, meno, koo, masikio na magonjwa ya ndani na njia ya mkojo, Amani Malima amesema kwa siku mbili walizofanya kazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro,  wamepokea wagonjwa  zaidi ya 1,500.

Hata hivyo, Dk Malima amesema baadhi ya wagonjwa hao ni wale waliohitaji kufunga safari kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Amesema walipanga kuwaona wagonjwa 2,000 sambamba na kufanya upasuaji kwa wagonjwa 100, lakini hali inaonesha kutakuwa na ongezeko kubwa.

Madaktari bingwa hao wameweka kambi mkoani Morogoro kwa wiki moja kwa lengo la kutoa huduma kwa wagonjwa.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Mei 8, 2024, Dk Malima ambaye pia ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Tumbi ya Mkoa wa Pwani, amesema huduma hiyo waliyoianza kuitoa Jumatatu Mei 6 wagonjwa wengi wamejitokeza.

Hata hivyo, amesema wagonjwa saba wamepatiwa rufaa kutokana na magonjwa yao kuonekana hayawezi kutibika hospitalini hapo na sasa wanatakiwa kwenda Hospitali ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Afya kutoka Wizara ya Afya, Dk Caroline Damiani amesema lengo la kliniki hiyo ni kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi, zaidi ya wananchi 7,000 wamenufaika na kliniki hiyo nchi nzima.

“Lengo la kliniki yetu ni kuhakikisha huduma inasogea karibu na wananchi, tunaamini mpaka kliniki hii ya siku tano itakapofika tamati, wagonjwa wengi watakuwa wamepata huduma,” amesema Dk Damiani.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema kitendo cha wananchi wengi kujitoeza ni ishara kuna wagonjwa wengi wanaotakiwa kupewa tiba za kibingwa.

“Mwitikio huu wa wagonjwa 1,530 kujitokeza ndani ya siku mbili ni ishara kwamba, tunao wahitaji wa huduma za kibingwa kwenye maeneo yetu, niwaombe ninyi madaktari, wagonjwa wote watakaofika kwenye kliniki wapatiwe matibabu maana wengi hawa hawana uwezo wa kuzifuata hospitali kubwa,” amesema Malima.

George Michael, mkazi wa Turiani aliyefika kupata huduma, amesema madaktari hao wanajua kinachokusumbua kwenye mazungumzo.

“kiukweli hawa ni madaktari bingwa, mimi binafsi nilikuwa nasumbuliwa ugonjwa kwenye koo langu, nilikosa raha kwa muda, nilipofika kwenye kliniki nikaongea na daktari akagundua changamoto yangu na kupewa matibabu hivyo huduma hii ni nzuri kwetu,” amesema Michael.