Airbus A220 – 300 inavyoisababishia hasara ATCL

Dar es Salaam. Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ilipata hasara ya Sh56.64 bilioni katika mwaka wa fedha 2022/23 ikiwa ni ongezeko la asilimia 61, ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita.

Ripoti ya mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2022/23 imebainisha kuwa shirika hilo limeendelea kupata hasara kwa miaka sita mfululizo, licha ya kuwa inapokea ruzuku kutoka serikalini.

Ripoti hiyo ilitaja sababu zinachangia hasara zikijumuisha kuwapo kwa gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli za ATCL, pamoja na gharama zisizoepukika kama vile za ukodishaji na bima kwa ndege ya Airbus A220 - 300 isiyofanya kazi kutokana na matatizo ya kiufundi ikiwamo kutu na kasoro za injini.

Ripoti hiyo ilinukuu, “ mwaka wa fedha 2022/23, ATCL ilipokea ruzuku ya Sh31.55 bilioni kwa ajili ya kugharamia mishahara ya wafanyakazi, mafunzo ya majaribio na ruzuku ya Sh7.45 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.”

“Matatizo haya yamegunduliwa na mtengenezaji wa ndege hiyo na yameathiri idadi ya ndege za aina hii kote ulimwenguni. Kuharibika kwa ndege ya Airbus A220 - 300 kuliathiri mwenendo wa safari za ndege, hivyo kusababisha ATCL kukosa mapato na kushindwa kufidia gharama za kudumu za ndege iliyoharibika” imesema ripoti hiyo.

Ripoti ya CAG imesema kutatua changamoto hiyo Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuundwa kwa timu ya wataalamu inayofanya tathmini ya masuala ya kiufundi ya ndege, kifedha na utendaji wa ATCL katika biashara ya usafiri wa anga.


Endelea kufuatilia katika mitandao ya Mwananchi Digital