Ajali Ruvu yasababisha msongamano wa magari mitaani

Muktasari:

  •  Mabasi yaliyohusika kwenye ajali hiyo ni Sauli la Dar - Mbeya na New Force Dar -Tunduma.

Kibaha. Abiria wanaoingia na kutoka Dar es Salaam wameendelea kupata adha ya foleni kutokana na barabara ya Morogoro – Dar es Salaam kufungwa katika eneo la Ruvu, Kibaha mkoani Pwani.

Kufungwa kwa barabara katika eneo hilo kumetokana na ajali iliyohusisha magari matatu yaliyoteketea kwa moto leo alfajiri ambapo mawili kati ya hayo ni mabasi ya abiria na lori la mafuta.

Kutokana na hali hiyo, askari wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Pwani, wameelekeza magari kutumia barabara ya zamani inayoingilia Mlandizi na kutokea jirani na ukumbi wa Jeshi la Kujenga Taifa (Ruvu JKT).



Hata hivyo, kutokana na baadhi ya madereva kukaidi utaratibu ulioelekezwa wa kupitia kwa zamu kila upande, umetokea msongamano mkubwa wa magari.

pia malori makubwa yamekwama pembezoni mwa barabara hiyo ya mchepuko na mengine yameshindwa kupitia .

Hadi sasa 7:30 mchana idadi kubwa ya magari ambayo yanatoka Dar es Salaam kwenda mikoani yako kwenye foleni inayoanzia Visiga hadi Mlandizi huku Askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji wakiendelea kuzima moto kwenye lori lililowaka kwa mara ya pili.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo wamefika eneo la tukio.

Endelea kufuatilia tovuti na mitandao yetu kwa habari zaidi