Wafanyabiashara walalamika foleni ya malori

Foleni ya malori yakiwa katika Barabara ya Tanzam kutoka Mbeya kwenda Tunduma.

Songwe. Wafanyabiashara mkoani Songwe wamelalamikia foleni ya magari katika Barabara ya Tanzam kutoka Mbeya kwenda Tunduma kuwa inachelewesha mzunguko wa biashara.

Hayo yamezungumzwa katika kikao Cha Baraza la Biashara la mkoa wa Songwe kinachoendelea kufanyika leo Jumatano Septemba 13 mwaka huu, kuwa kuwepo kwa foleni katika barabara hiyo imekuwa kikwazo cha biashara hivyo kuiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kumaliza tatizo hilo ili kurahisisha usafirishaji na uchukuzi.

Mkurugezi wa Hoteli ya Ukinga Hill iliyopo Tunduma, Forbat Kyando amesema kutokana na kuwa barabara hiyo ni nyembamba na wakati huo magari yanayopita ni mengi hali inayosababisha uchelewaji wa usafirishaji katika eneo lenye umbali wa kilometa 35 unatumia saa 2 au zaidi kusafiri.

"Nashauri malori yasiruhusiwe kuingia barabarani wakati nyaraka hazijawa tayari yasiingie barabarani kwani ndiyo yanayoongeza msongamano," amesema Kyando.

Mkulima mwekezaji wa kahawa, George Nzunda amesema kutokana na foleni na magari kusimama muda mrefu katika eneo la Senjele, Kata ya Nanyala wilayani Mbozi, imesababisha mnada wa kahawa Mbozi kudorora baada ya wanunuzi wa kutopenda kuja Songwe kushiriki mnada huo.

"Mnada ulianzishwa kwa lengo la kuwapa nafasi wazalishaji wa Kahawa kushiriki na kujionea lakini imekuwa vigumu, nashauri Serikali itoe ulinzi (escort) kwa wanunuzi wa kahawa wanaokuja ili wasipoteze muda kusafiri," amesema Nzunda.


Kwa upande wake Mkuu wa mkoa Songwe, Dk Francis Michael amemwagiza Kamanda wa Polisi mkoani hapa kutoa ulinzi kwa wanunuzi wanaoingia ili waweze kuja kununua kahawa na kuleta fedha mkoani kwetu.

Vilevile amesema suala la foleni Tunduma ameunda kikosi kazi ambacho kila siku kinahakikisha foleni haijitokezi, lakini pia amebaini kwamba wapo mawakala wa mpakani ambao wanatoa magari kuyaingiza barabarani pasipokuwa na nyaraka matokeo yake magari yanakaa barabarani.

"Nimekaa nao nimewaelekeza mawakala hao tumeelewana, lakini katika kipindi cha siku mbili hizo wenzetu Wazambia wanajenga barabara hivyo kusababisha magari kupita taratibu lakini wakimaliza mambo yatakaa vizuri," amesema Dk Francis.

Aidha zaidi ya malori 900 huingia kutoka Bandari ya Dar es Salaam kila siku katika mpaka wa Tunduma, lakini uwezo wa kuyapitisha ni malori 400 tu kwa siku.