Bomoabomoa yashika kasi Bonde la Msimbazi

Muktasari:

  • Ni baada ya nyumba kuwekwa alama zikitakiwa kubomolewa.

Dar es Salaam. Kazi ya kubomoa nyumba kupisha mradi wa maendelezo ya Bonde la Msimbazi inaendelea kwa kasi, baada ya kuwekewa alama ya X kuashiria zibomolewe na wahusika wameshafidiwa.

 Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) unaosimamia mradi huo, umeweka alama hizo katika mitaa ya Msimbazi Bondeni, Kigogo na Suna.

Mwananchi Digital imeshuhudia baadhi ya wakazi wa maeneo hayo wakibomoa nyumba zao na wengine wakihamisha mali zao.

Ofisa Habari Mwandamizi wa Mradi wa Bonde la Msimbazi, Raphael Kalapilo, amesema jana Aprili 15, 2024 kuwa kubomoa kwa hiari ndicho kitu walichokuwa wanataka wananchi wafanye, ili waondoke na mali zao.

Wakazi wa mtaa wa Magomeni Suna wanaopitiwa na mradi wa Bonde la Msimbazi wakiwa wanahamisha mali zao.

“Naweza kusema shughuli ya bomoabomoa imeanza rasmi baada ya kuweka alama katika nyumba zinazotakiwa kubomolewa, hii ni baada ya kukamilisha malipo,” amesema.

Amesema wananchi 2,155 kati ya 2,329 waliokubali kulipwa fidia wameshalipwa.

Mradi wa uendelezaji wa Bonde la Msimbazi unatekelezwa, ili kukabiliana na mafuriko na kuboresha matumizi ya ardhi katika eneo la chini la bonde hilo.

Mradi huo unatarajiwa kugharimu Dola milioni 260 za Marekani (Sh675 bilioni) na unafadhiliwa na Benki ya Dunia.

Habiba Mondoma, akizungumza kwa niaba ya wananchi wanaopitiwa na mradi huo, amesema uwekaji wa alama na matangazo mitaani yanayotolewa kuhusu ubomoaji yameongeza kasi ya wananchi kubomoa kwa hiari.

Amesema baadhi ya nyumba ambazo watu walishaondoka, zilianza kutumiwa vibaya na baadhi kupangisha kwa watu ambao hawakuwa wakijua kuhusu ubomoaji.

Wananchi wanaopitiwa na mradi wa bonde la Msimbazi wakiwa wanabomoa nyumba zao.

Habiba amesema baadhi ya wananchi wanaotoka maeneo hayo bado wanakwenda kujenga au kuishi katika makazi holela kwa kuwa fedha walizolipwa wanalalamika kuwa ni ndogo.

“Fedha zimekuwa ndogo kutokana na kutopewa fidia ya ardhi, fedha ambayo walau ingetosha mtu kwenda kununua eneo lililopimwa, lakini matokeo yake hatukulipwa zaidi ya Sh4 milioni ambayo tulipewa kama kifuta jasho na Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.

“Hii ni baada ya awali kulalamika kulipwa nyumba tu kwa kile mamlaka ilichoeleza eneo letu lilikuwa hatarishi, hivyo kukosa uhalali wa kulipwa fidia ya ardhi,” amesema.

Mwenyekiti wa Magomeni Suna, Salim Hamis, amesema ameridhishwa na shughuli za uhamishaji zinazotekelezwa japo kuna changamoto ndogo.

Ameiomba Serikali kuwaangalia waliokumbwa na bomoabomoa mwaka 2016 kabla ya kuwekwa zuio la Mahakama la kuzuia ubomoaji ili nao walipwe.

“Katika kulifanikisha hili nashauri hata ingetumika ramani ya zamani ya eneo hilo badala ya kuwaacha bila kitu,” amesema.

Kalapilo akizungumzia hilo amesema ni ngumu kuwalipa watu hao kwa kuwa katika maeneo yao hukukuwa na kitu ambacho kinaonekana cha kuwezesha uthamini kufanyika kwa mujibu wa sheria za fidia ya ardhi.