CAG aeleza kiini mashirika ya umma kupata hasara

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere akizungumza wakati akisoma ripoti yake mbele ya waandishi wa habari kwa mwaka 2022/23 leo Jumatatu, Aprili 15, 2024 mjini Dodoma. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Dosari za utendaji zasababisha robo ya mashirika ya umma kupata hasara, nakisi

Dar es Salaam. Mashirika ya umma 58 kati ya 215 yaliripoti kupata hasara au nakisi kwa miaka miwili mfululizo mwaka 2021/22 na 2022/23 au kwa mwaka mmoja wa fedha uliopita. Idadi hiyo ni zaidi ya robo ya mashirika ya umma.

Ripoti ya mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2022/23 imeonyesha  hasara hiyo ilitokana na ‘dosari za kiutendaji zinazosababisha utendaji usioridhisha katika uwekezaji au uendeshaji wa biashara, au kupata msaada wa fedha kutoka serikalini’. 

Mashirika yaliyopata hasara, nakisi

Miongoni mwa mashirika yaliyopata hasara ni Shirika la Reli Tanzania (TRC) ambalo limepata hasara mfululizo kwa miaka miwili. Katika mwaka wa fedha 2022/23, shirika hilo lilipata hasara ya Sh100.7 bilioni, ikilinganishwa na hasara ya Sh190.01 bilioni katika mwaka wa fedha 2021/22.

Kampuni ya Uwekezaji ya TANOIL imepata hasara ya Sh76.56 bilioni kwa mwaka wa fedha 2022/23, ikilinganishwa na hasara ya Sh7.84 bilioni kwa mwaka wa fedha uliopita.

Sababu kuu ya hasara ya kampuni hii ilikuwa mafuta yaliyoagizwa kutoka nje kuzuiwa kwa sababu ya TANOIL kushindwa kuwalipa wauzaji. Athari ya mafuta yaliyozuiwa ni gharama kubwa za kuyahifadhi ambazo ni  (Sh12.9 bilioni ikilinganishwa na Sh6.1 bilioni mwaka uliopita).

Sababu nyingine ilikuwa ukusanyaji duni wa mapato ambapo katika mwaka wa fedha wa 2022/23, mapato ya kampuni kutokana na mauzo ya mafuta yalipungua kwa Sh296 bilioni  ambayo ni asilimia 49. Hii ilitokana na kupungua kwa kiwango cha mafuta kilichouzwa kikiwa ni lita milioni 112 ziliuzwa katika mwaka wa fedha 2022/23 ikilinganishwa na lita milioni 264 zilizouzwa mwaka uliotangulia.

Shirika la Masoko la Kariakoo limepata hasara ya Sh41.57 bilioni, ambayo ni kubwa kuliko hasara ya Sh517.97 milioni iliyopatikana katika mwaka wa fedha uliopita 2021/22. Ripoti ya CAG imebainisha kuwa sababu kuu ya hasara hii ni kusitishwa kwa ukusanyaji wa mapato katika eneo la soko la Kariakoo. Hii ni baada ya tukio la moto wa mwaka 2020 ulioteketeza jengo la soko hilo.

Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) imepata hasara kwa miaka miwili mfululizo. Katika mwaka wa fedha wa 2022/23, kampuni ilipatata hasara ya Sh894 milioni ikilinganishwa na hasara ya Sh19.23 bilioni katika mwaka wa fedha 2021/22. 

Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) imeendelea kupata hasara kwa miaka sita mfululizo. Mwaka wa fedha wa 2022/23 Kampuni ilipata hasara ya Sh56.64 bilioni. Mwaka uliopita kampuni ilipata hasara ya Sh35.23 bilioni.

Mashirika yenye mtaji hasi

Ripoti hiyo pia ilibaini mashirika ya umma 11 yaliyokuwa na mtaji hasi katika mwaka wa fedha uliomalizika Juni 30, 2023. Sababu kuu za mtaji hasi kwa mashirika hayo zilitajwa kuwa malimbikizo ya hasara kwa muda mrefu na madeni makubwa wanayoingia mashirika hayo, ili kufadhili shughuli zao.

Kampuni ya ATCL yenye mali za Sh339.39 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 61 ya mtaji unaohitajika. Mashirika mengine ni Kampuni ya STAMIGOLD ambayo inanakisi ya asilimia tisa, Kampuni ya Gesi Tanzania asilimia 13 na  Kituo cha Kompyuta Chuo Kikuu cha Dar es Salaam asilimia 39.

Kwa mashirika yasiyo ya kibiashara Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania ina mtaji wa Sh6.49 bilioni sawa na asilimia mbili pekee ya Sh262.53 bilioni inayohitajika.

Mashirika mengine ni  Mfuko wa Maendeleo ya zao la Pamba   wenye nakisi ya asilimia 12, Bodi ya Pareto Tanzania asilimia  71,  Bodi ya Maziwa Tanzania asilimia 43 na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Anga asilimia 62.

Vilevile, CAG alibaini mashirika 63 yenye madeni ya muda mfupi zaidi kuliko mali za muda mfupi; ambapo 13 kati ya hayo yalikuwa mashirika ya umma ya kibiashara, huku 50 yalikuwa mashirika yasiyo ya kibiashara.

Uwiano wa ukwasi ulikuwa kati ya asilimia moja hadi 98. Hivyo basi, taasisi hizi zinaweza kushindwa kulipa mikopo na kuchelewesha malipo kwa wazabuni.

Aidha, mashirika ya umma 28 (12 ya kibiashara na 16 yasiyo ya kibiashara) yalikuwa na uwiano mbaya wa madeni (jumla ya madeni yote dhidi ya jumla ya mtaji) kwa zaidi ya asilimia 100. Hii inaonyesha mashirika haya, kwa kiasi kikubwa, yanategemea mikopo kujiendesha.

Hii inasababisha kuwa na hatari kubwa ya kifedha kutokana na gharama kubwa za kuhudumia madeni.


Usimamizi wa bajeti katika mashirika ya umma

CAG amebaini Serikali haikutoa Sh1.01 trilioni kwa mashirika 50 ya umma kama ilivyopangwa katika mwaka wa fedha 2022/23.

Vilevile, mashirika ya umma 66 hayakukusanya fedha kiasi cha Sh284.71 bilioni kutoka katika bajeti ya vyanzo vya ndani katika mwaka wa fedha 2022/23.

Pia, ripoti hiyo ilibaini mashirika ya umma manane yalitumia zaidi ya bajeti kwa kiasi cha Sh21.14 bilioni bila idhini ya Ofisa Masuuli au Bodi ya Wakurugenzi.