Chalamila aonya vijana wanaotukana Serikali kisa kukosa ajira

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila. Picha na Maktaba

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewataka wanafunzi kuacha kuitukana  Serikali zinapokosekana ajira kwa kudai kutelekezwa na baada ya kumaliza masomo yao.

Chalamila ameyasema hayo jijini Dar es Salaam leo  Ijumaa Aprili 19,2024 katika hafla ya kupandishwa hadhi ya Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (DarTu), kuwa Chuo Kikuu baada ya kuwa chuo kikuu kishiriki kwa miaka 20.

Amewataka wanafunzi kujiuliza iwapo ni muhimu kuendelea kulalamika au kutumia walichopata ili watatue tatizo, maana chanzo cha kuwepo kwa chuo cha DarTu na kuweka kwa bodi ya mikopo ni Serikali.

Amesema wamepewa nyenzo wakazitumie vizuri ili zikawasaidie kutafsiri upya ulimwengu wa ajira nje ya chuo chao na hata wanapokosa wasiwe wepesi wa kutukana Serikali, kwani wamepewa wigo mpana wa kuweza kuchagua mambo mengi ya kufanya siku za baadaye.

Pia amesema maanguko ya vyuo vikuu ni matumizi mabaya ya fedha, hivyo amewataka chuo cha DarTu kisiingie katika historia hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amewataka wakuu wa vyuo kuacha kuwakumbatia wanafunzi wanaofanya vibaya, ili kupata wafanyakazi wenye ubora.

"Kama mwanafunzi alikuja akiwa vizuri lakini akaanza kufanya vibaya anatakiwa kuachia ngazi ili kupata watu wenye ubora kwa kufikiria kuwa unayembeba leo anakwenda kutibia mgonjwa au kujenga majengo, kitu gani kitakwenda kutokea siku za usoni," amesema Mkenda.

Pia, amesema ili kuendana na soko la ajira wamebadilisha mitaala ya elimu na inatakiwa vyuo kuelimisha wanafunzi kuchangamsha ubongo, ili kuendana na soko la ajira.

Hata hivyo, Profesa Mkenda amesema Serikali inaendelea kuongeza wigo wa mikopo kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wa vyuo vyote vya umma na binafsi bila ubaguzi.

Awali Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (DarTu), Askofu Alex Malasusa amesema masomo ya dini yasidharauliwe kwani yanawajenga watu katika misingi ambayo ipo katika maisha ya kawaida.

Dini mbili ya Kikristo na Kiislamu zilizopo nchini zinawaandaa vizuri Watanzania katika maisha ya baadaye, hata inapozungumziwa rushwa na kukosekana kwa uzalendo vyote  vinapatikana katika vitabu vya Biblia na Quran.

Amesema inatakiwa kuendelea kutafakari kama Taifa kuhusu masomo ya dini ili yasijekuachwa kwani yana umuhimu wake kwa jamii.

"Watu wakitaka kujiunga kwenye vyuo wanaeleza sifa ya masomo lakini wanaingiza neno isipokuwa masomo ya dini, hivyo kuna haja ya kuendelea kutafakari kuhusu masomo ya dini kwani yana umuhimu wake," amesema Askofu Malasusa.

Pia amesema elimu inayotolewa na DarTu haina ukakasi kwani imekuwa ikikidhi vigezo vya kutoa wanataaluma kitaifa na kimataifa licha ya uwepo wa changamoto kadhaa.

Katika kuwasaidia wanafunzi kufikia malengo yao ya kusoma elimu ya juu amesema wanaamini kuwa Serikali itaendelea kuboresha mikopo ya wanafunzi, kwani wapo  wanaotumia posho zao za kujikimu kulipia ada.

Amesema kumekuwa na maombi ya udahili wa wanafunzi lakini inashindikana kutokana na ufinyu wa eneo licha ya kuwa na mpango wa kutanua chuo hicho.

"Chuo kina wanafunzi 4,500 na watu wamekuwa wakituma maombi kwa wingi kutokana na kile tunachokitoa hapa, hivyo tuna uhitaji wa majengo mengine kwa lengo la kudahili wanafunzi wengi zaidi," amesema Malasusa.