Chuo Kikuu cha Aga Khan kukuza afya ya akili kuanzia ngazi ya elimu ya msingi

Mhadhiri wa Shule ya Ukunga na Uuguzi ya  Chuo Kikuu cha Aga Khan, Dk Stewart Mbelwa akiwajengea uwezo wanafunzi namna ya kukabiliana na tatizo la afya ya akili

Muktasari:

 AKU yawajengea uwezo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari namna ya kukabiliana na tatizo la afya akili

Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) kimechukua hatua ya kipekee kukuza utamaduni wa ustawi wa akili kuanzia ngazi ya msingi ya elimu nchini.

Hivi karibuni AKU iliendesha warsha iliyowakutanisha wanafunzi wa shule za sekondari na walimu kutoka maeneo mbalimbali, kukuza uelewa wa afya ya akili na usimamizi wa msongo wa mawazo kwa wanafunzi.

Mtaalamu wa afya ya akili na mhadhiri katika Shule ya Uuguzi na Ukunga ya AKU, Dk Stewart Mbelwa amesisitiza umuhimu wa kushughulikia masuala ya afya ya akili miongoni mwa wanafunzi, hasa katika kuchagua masomo yanayoainisha kazi zao za baadaye.

“Kila hatua ya maisha ya mwanafunzi kuna mizigo mingi ya mawazo, lakini kundi hili mara nyingi halizingatiwi linapokuja suala la kulinda afya yao ya akili,” amesema Dk Mbelwa.

“AKU imejitolea kuwawezesha wanafunzi ngazi ya msingi kushughulikia changamoto hizi na kuhakikisha kuwa hazizuii maendeleo ya masomo au kuwanyima wanafunzi haki yao ya elimu.”

Amesema matatizo ya afya ya akili miongoni mwa wanafunzi yamekuwa yakiongezeka, lakini mara nyingi yanapuuzwa katika mijadala na mipango inayolenga ustawi wa akili.

Dk Mbelwa amesisitiza dharura ya kushughulikia suala hili, hasa katika shule za umma.

Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Sega iliyopo Morogoro,  Elly Sarakikya amesema ni umuhimu washauri nasaha katika shule kutoa msaada wa kutosha kwa wanafunzi wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali.

"Ikiwa hatutashughulikia mahitaji ya afya ya akili ya wanafunzi hawa na kuzingatia tu mafanikio ya masomo, kuna hatari ya kuendeleza watu wenye matatizi ya akili ambazo hazijatatuliwa,”amesema Sarakikya.


Mshauri kutoka Shule ya Sega, Grace Msele ametilia mkazo umuhimu wa kuingiza elimu ya afya ya akili katika mitalaa na kuhakikisha wanafunzi wanapata mifumo ya msaada ya kutosha ndani ya mazingira ya shule.

 “Tunapaswa kutambua kuwa afya ya akili ya watoto inahusiana sana na mafanikio yao ya masomo na ustawi wao kwa ujumla,”amesema Grace.

“Wakati taswira ya elimu nchini Tanzania inavyobadilika, kuna haja ya dharura kwa watunga sera na wadau kutambua umuhimu wa elimu ya afya ya akili katika shule.

“Kwa kuipa vipaumbele mipango ya ustawi wa akili, shule zinaweza kuunda mazingira yanayowasaidia wanafunzi katika maendeleo yao na kuhakikisha mafanikio yao ya masomo.”

“Inatakiwa shule zote ziukubali huu mwelekeo wa kubadilisha elimu, hivyo kukuza kizazi cha watu imara na wenye nguvu wanaoweza kufanikiwa katika masomo na maisha binafsi,”amesema Grace.