Dereva asimulia abiria walivyonusurika kifo ajali ya mabasi mawili Ruvu

Kibaha. Dereva wa lori lililogongwa na mabasi mawili ya Kampuni ya New Force na Sauli na kusababisha vifo vya watu wawili na kujeruhi wengine watatu, amesimulia namna ajali hiyo ilivyotokea huku abiria wakisalimika.

Dereva huyo aliyejitambulisha kwa jina la Musiyimana Musimana alisema ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana saa 10 alfajiri eneo la Ruvu, mkoani Pwani.

Akizungumza jana na Mwananchi, Musimana alisema baada ya ajali kutokea abiria walipitia mlangoni kutoka na mizigo yao.

Alisema walipakiwa kwenye mabasi mengine ya kampuni husika na kuendelea na safari kabla ya mabasi yaliyopata ajali kulipuka takribani dakika 45 baadaye.

Alisema miongoni mwa majeruhi ni askari wawili wa Jeshi la Zimamoto, Hamis Kungwi na Elias Bwire waliopata majeraha wakati wakitekeleza jukumu la kuzima moto uliolipuka baada ya magari hayo kugongana.

“Hawa askari walikuwa wanazima moto ulioanza kuwaka, walipokuwa wanaendelea kuuzima ukatokea mlipuko mwingine kule kwenye lori la mafuta,” alisema dereva huyo.

Akizungumza na gazeti hili akiwa eneo la tukio, Musimana alisema alikuwa akitokea Dar es Salaam kwenda Rwanda, alipofika eneo ilipotokea ajali, kulikuwa na gari limeharibika.

“Ilikuwa saa 10 alfajiri, nikaona kuna gari mbele yangu limesimama, nikalazimika kusimama ili kuona namna ya kufanya, nilisimama pale kwa dakika kama 30, baadaye nikaona mabasi mawili yanakuja yakiwa yameongozana, moja lilitaka kulipita lingine, alipogundua mbele kuna gari linakuja akalazimika kurudi upande wa pili akasimama ghafla, lile basi la nyuma yake likamgonga na yeye akaja kugonga gari langu,” alisimulia. Alisema baada ya nusu saa, ndipo ukatokea mlipuko wa moto kwenye tenki la mafuta la Basi la Sauli.

Alisema baada ya ajali hiyo, watu wawili walibanwa chini ya basi la New Force, “nahisi ndiyo hao waliokufa.”

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge alisema tukio hilo limemsikitisha na ajali imetokea kwa sababu ya uzembe wa madereva wa mabasi yote mawili.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Piusi Lutumo alisema chanzo cha ajali ni dereva wa Basi la Sauli lenye namba za usajili T668 DTF, Idd Aloyce, mkazi wa Mafinga kuendesha gari bila kuchukua tahadhari.

Alisema basi hilo lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mbeya liligonga ubavuni lori la mafuta lililokuwa limeegeshwa kando ya barabara. "Basi hilo lilikuwa limeongozana na basi la Golden Deer linalomilikiwa na Kampuni ya New Force, lenye namba za usajili T175 DZU, likiendeshwa na Burton Jacob, mkazi wa Mbeya ambalo nalo lililigonga kwa nyuma basi la Sauli na kusababisha vifo vya watu wawili,” alisema.