Dk Biteko: Tuheshimiane, sitaki mazoea

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akipungia mkono wananchi alipoenda kukagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kupoza umeme cha Uhuru kilichopo wilayani Urambo Mkoa wa  Tabora, jana. Na Mpigapicha Maalumu

Muktasari:

  • Dk Biteko ameonyesha kutoridhishwa na utendaji wa kampuni hiyo tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kumuelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mhandisi Felchesmi Mramba kuzieleza taasisi zote zilizo chini yake kuacha mazoea.

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameagiza kuondolewa kazini kwa Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi na Matengenezo ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO), Mohamed Abdallah kutokana na kusuasua kwa ujenzi wa laini ya umeme kutoka Tabora hadi Urambo.

Dk Biteko ameonyesha kutoridhishwa na utendaji wa kampuni hiyo tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kumuelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mhandisi Felchesmi Mramba kuzieleza taasisi zote zilizo chini yake kuacha mazoea.

Naibu Waziri Mkuu amesema hayo leo Machi 27, 2024 , alipotembelea mradi wa kituo cha kupoza umeme cha Uhuru kilichopo wilayani Urambo, Mkoa wa Tabora na kukuta ujenzi wa kituo hicho ukielekea kukamilika, lakini ujenzi wa laini ya umeme haujaanza.

Amesema kuchelewa kwa ujenzi wa laini hiyo kutaisababishia Serikali hasara, kwani mkandarasi wa kituo cha kupozea umeme atashindwa kukiwasha kwa sababu hakuna umeme, hivyo atalazimika kusubiri na kipindi chote atakachosubiri atakuwa akilipwa.

“Septemba 17, 2023 nilimtuma Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga kuja kukagua mradi huu ambaye aliwapa maelekezo ya kuukamilisha, pia nilimtuma aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Meja Jenerali Paul Simuli kuja kukagua mradi huu Desemba 17, 2023 naye alitoa maelekezo ambayo hayajatekelezwa.”

“Hatari ni kwamba, mkandarasi wa kituo atamaliza mapema Juni, lakini hapatakuwa na umeme kwa sababu ya kusuasua kwa mkandarasi anayejenga laini ya kutoka Tabora kuja hapa, bahati mbaya mkandarasi huyo ni kampuni yetu Tanesco ya ETDCO. Nimeuliza meneja mkuu wa kampuni hii yuko wapi wameniambia amenitumia mwakilishi, yaani mimi waziri wa sekta niko hapa yeye yuko Mwanza amenitumia mwakilishi,” amesema Dk Biteko.

Kufuatia hilo, akamuelekeza Katibu Mkuu, Mramba kumuondoa kazini meneja mkuu wa ETDCO kwa kushindwa kusimamia kazi hiyo na miradi mingine inayosimamiwa na kampuni hiyo, akieleza kuwa mingi ni kichefuchefu.

“Tusidharauliane, mimi waziri siwezi kuja hapa kulalamika natoa maelekezo, kwanza nikuelekeze katibu mkuu muondoe haraka meneja mkuu wa kampuni hiyo utafute mtu mwingine halafu upeleke hiyo taarifa kwenye bodi.

“Pia, Katibu Mkuu waambie Tanesco na mashirika mengine yote yanayofanya kazi chini ya wizara ya nishati tuheshimiane, sitaki mazoea, hizi kazi ni za wananchi na lazima waone matokeo,” amesema Dk Biteko

Mashirika hayo ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (Pura), Tanesco, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA).

 Dk Biteko amewataka watendaji wanaoona kwamba hawawezi kuishi na kutafsiri maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kujiondoa kwenye nafasi zao wenyewe ili kutorudisha nyuma juhudi za Serikali kutatua changamoto za wananchi.

Amesema Rais ametoa fedha kujenga laini ya umeme kutoka Tabora-Ipole-Mlele hadi Mpanda Mjini kwa urefu wa kilomita 393 na kwamba ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Ipole umefikia asilimia 89, Mlele umefikia asilimia 87 na Mpanda Mjini umefikia asilimia 90, huku laini ya umeme ujenzi wake ukifikia asilimia 47.

Dk Biteko amesema nia ya Serikali ni kuwapa wananchi umeme na siyo maneno na ndiyo maana utekelezaji wa miradi mbalimbali unaendelea, ukiwamo mradi wa Julius Nyerere ambao tayari mashine moja imeshaanza kuzalisha megawati 235, huku mashine nyingine ikikamilishwa mwezi huu ili kuingiza megawati 235 nyingine na hivyo kumaliza kabisa changamoto ya upungufu wa umeme.

Mbunge wa Urambo (CCM), Magreth Sitta amemshukuru Dk Biteko kwa kukagua mradi huo na kutoa maelekezo yatakayouwezesha kukamilika kwa wakati na kuondoa changamoto ya umeme kukatika mara kwa mara.

Pia, amemshukuru Rais Samia kwa kupelekea fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, maji, afya katika jimbo lake la Urambo.