Dk Mpango kufungua mkutano wa Shirikisho la Wakaguzi Afrika

Baadhi ya wadau wa mkutano wa 10 wa Shirikisho la wakaguzi wa ndani Afrika (AFIIA), wakiwa katika ukumbi wa mikutano wa AICC, Arusha leo Jumanne Aprili 16,2024 ambapo kesho Makamu wa Rais Dk Philip Mpango anatarajiwa kuufungua. Picha na Janeth Mushi

Muktasari:


  • Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango atakuwa mgeni rasmi katika mkutano wa 10 wa Shirikisho la Wakaguzi wa Ndani Afrika (AFIIA) Arusha.

Arusha. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa 10 wa Shirikisho la Wakaguzi wa Ndani Afrika (AFIIA), utakaofanyika kesho Aprili 17, 2024 mkoani Arusha.

Pamoja na masuala mengine, wahasibu hao wa ndani wanatarajia kujikita zaidi katika kuangalia utendaji kazi wao, lengo likiwa kusaidia taasisi za Serikali za Afrika kuboresha utendaji kazi wake.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo Aprili 16, 2024, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Saada Mkuya amesema mkutano huo unaowaweka pamoja wahasibu wa ndani, unalenga kubadilishana uzoefu hasa katika matumizi ya teknolojia katika kukuza kada hiyo.

Amesema wadau hao watajadili namna ya kuboresha utendaji kazi wao, ikiwemo suala la usalama wa mtandaoni.

“Tunatarajia kesho Aprili 17, 2024, Dk Mpango atafungua mkutano huu ambao kwa pamoja wataalamu hawa kutoka nchi mbalimbali ikiwemo za Afrika, watabadilishana uzoezi, kwani mazingira ya sasa yameimarika, tuna ukuaji mkubwa wa teknolojia, kuna suala la usalama wa mtandaoni, akili bandia, hivyo ni vema tubadilishane mawazo ili kuimarisha taaluma.

“Tunapozungumzia suala la ukaguzi wa ndani lazima liende sambamba na utawala bora katika kuhakikisha wanasimamia kikamilifu fedha na kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo,” ameongeza Dk Saada.

Rais wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIA), Zelia Njeza amesema kabla ya kufunguliwa mkutano huo, wataanza na mkutano wa viongozi wa shirikisho hilo wakiwemo viongozi wa taasisi za umma, binafsi kutoka Tanzania, Afrika na nchi nyingine nje ya bara la Afrika.

Amesema mkutano huo umeshirikisha wataalamu hao kutoka nchi 27 za Afrika na wengine kutoka nje ya bara hilo ambapo wanategemea utaleta chachu ya utendaji kazi katika kada hiyo, ambapo washiriki zaidi ya 1,000 wanatarajiwa kushiriki.

“Tutajikita zaidi kuangalia utendaji kazi wetu, lengo kuu ni kuhakikisha tunasaidia taasisi na Serikali kuboresha kazi zao. Tumeona tukiwa na sauti moja kama Afrika tunaweza tukasaidia nchi zetu za Afrika kutoka hapa hadi kufika mbele.

“Tumejikita zaidi katika masuala ya teknolojia kuelezea jinsi teknolojia inavyokuwa kwa kasi, masuala ya mazingira, tutajadili masuala mbalimbali kuangalialia uhalisia wa Afrika, kuna masuala ya ubadhirifu, tuna wataalamu wa utawala bora, hivyo tutakuwa na wawezeshaji kutoka mataifa mbalimbali,” ameongeza.