Dk Mwinyi azitaka nchi za SADC kuimarisha taasisi za utawala bora

Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi akizungumza kwenye Baraza la Idd lililofanyika Makao Makuu ya Polisi Zanzibar leo Aprili 10, 2024.

Muktasari:

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumatano Aprili 17, 2024 wakati akifungua mkutano wa mafunzo kwa wajumbe na wataalamu wa kamati ya Sadcopac katika kupambana na rushwa na kuhamasisha uwazi

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amezitaka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuziimarisha taasisi za utawala bora wa sheria na kukuza uwajibikaji ili ziwe na upeo mkubwa kufanya chunguzi zinazoleta tija kwa masilahi ya mataifa hayo.

Amesema taasisi za Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mamlaka za Kuzuia Rushwa na mabunge yana mchango mkubwa katika kuyafikia matarajio ya mataifa hayo.

Dk Mwinyi ametoa  kauli hiyo leo Jumatano Aprili 17, 2024 wakati akifungua mkutano wa mafunzo kwa wajumbe na wataalamu wa kamati ya Sadcopac katika kupambana na rushwa, kuhamasisha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa mali zisizo rejesheka.

“Ni muhimu kwa nchi zetu kuzijengea uwezo taasisi hizi zifanye kazi kwa ufanisi, taasisi hizi pia zifanye ziara za kimafunzo za kujengeana uwezo na kujifunza mbinu bora za kisasa katika kutekeleza majukumu yao, sambamba na kuendelea na utoaji wa mafunzo kama haya tunayoyafungua leo,” amesema Dk Mwinyi.

Amesema mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa, kuwepo kwa uwazi katika matumizi ya rasilimali za umma na kuhimiza uwajibikaji katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo na kuimarisha huduma za jamii, ni mambo ya misingi na yenye mchango muhimu katika kuchochea kasi ya maendeleo ya mataifa hayo. 

Dk Mwinyi  amesema nchi zitaweza kupiga hatua kubwa za maendeleo kwa haraka kwa kuzingatia kuwepo kwa rasilimali nyingi zinazoweza kuwa vyanzo vikuu vya kukuza uchumi ikiwa vitasimamiwa vyema na kutumika kwa misingi ya kisheria, uwazi na uwajibikaji. 

Amesema Serikali zote mbili, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zinafanya jitihada kubwa katika kukabiliana na vitendo vya rushwa na kuhimiza uwazi na uwajibikaji.
Miongoni mwa hatua zinazozichukuliwa na Serikali hizo ni pamoja na kuzijengea uwezo taasisi kwa mafunzo ili kuzipatia weledi, kuzipatia vifaa vya kufanyia kazi na kuzijengea miundombinu bora.

Kwa upande wa Zanzibar, Dk Mwinyi amesema Serikali inaendelea kupambana na rushwa na kuhimiza uwajibikaji na uwazi kwa kuanzisha mifumo mbalimbali ya huduma zikiwemo za kifedha na kuanzisha utaratibu wa kusomwa kwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hadharani.

Naibu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Tanzania, Wendy Massoy amesema lengo ni kuwakutanisha watu hao ni katika kupata mbinu mpya za uwajibikaji ambao ni muhimu katika Serikali.
“Imelenga namna jinsi gani inasimamia matumizi kwa zaidi ni upande wa rushwa na rasilimali,” amesema Massoy.

Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabau za Serikali Zanzibar, Dk Othman Abbas Ali amesema wanatarajia kupata uelewa wa utekelezaji wa kazi zao katika maeneo mapya ya kusimamia fedha za umma na rasimali za serikali.

“Hapa ni kuongeza fursa za kuwekeza hapa nchini katika maeneo tofauti na kuishauri Serikali uwekeji mifumo sahihi kukusanya mapato na mbinu bora za kuisaidia,” alisema.