Hivi ndivyo Tanzania inavyoweza kukabili athari za mafuriko

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), mvua za masika zilizoanza wiki ya nne ya Februari katika maeneo mengi zinatarajiwa kuisha wiki ya tatu na ya nne ya Mei, 2024

Dar es Salaam. Uwepo wa utashi wa kisiasa, matumizi ya sayansi kupewa nafasi na kubainishwa kwa maeneo hatarishi ni miongoni mwa hatua zilizopendekezwa na wanazuoni kukabiliana na athari za mafuriko Tanzania.

Mapendekezo ya wanazuoni yametolewa katika kipindi ambacho maeneo mbalimbali nchini yanakabiliwa na athari za mafuriko ambayo hadi sasa yameondoa uhai wa watu takribani 58 na kuacha wengine bila makazi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi aliyoitoa Aprili 14, 2024 mikoa iliyoathiriwa na mafuriko hadi sasa ni Lindi, Njombe, Tanga, Pwani, Manyara, Mbeya, Geita, Arusha, Morogoro na Rukwa.

Mwonekano wa mojawapo ya maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo wilayani Rufiji

Tayari ripoti ya maafa ya mafuriko hayo imeshakabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, huku hatua kadhaa zikitangazwa kuchukuliwa, ikiwamo kukarabati miundombinu iliyoharibika.

Wakizungumza na Mwananchi Digital kwa nyakati tofauti, wataalamu wa udhibiti wa majanga, wameonyesha ombwe la mbinu za kukabiliana na hali hiyo, jambo linalofanya ukubwa wa athari kujirudia kila janga linapotokea.

Utashi wa kisiasa

Kunahitajika kuwapo utashi wa kisiasa ili kupata suluhu ya muda mfupi na ya kudumu juu ya athari za mvua na mafuriko, kama inavyofafanuliwa na mtaalamu wa majanga wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Egidius Kamanyi.

Anasema utashi wa kisiasa ndiyo utakaoifanya Serikali ione umuhimu wa kujali na kulinda watu wake dhidi ya majanga.

“Utashi ndiyo utakaozalisha sababu ya kuanzisha mchakato wa kutafuta suluhu au namna ya kukabiliana na majanga kwa mbinu za kisayansi,” amesema Dk Kamanyi.

Sayansi ipewe nafasi

Dk Kamanyi amesema  kuendelea kwa majanga ya mafuriko na mengine, kunasababishwa na hatua ya Serikali kulazimisha kuikwepa sayansi katika maeneo yanayohitaji taaluma hiyo.

“Tuchukulie mfano kwenye miji yetu, ujenzi umefanyika bila mpangilio, baadhi wamefuata vyanzo vya maji na hawakuzingatia mbinu za kisayansi. Bado Serikali inaendelea kuruhusu ujenzi holela,” amesema.

Kuipa nafasi sayansi, anaeleza ni hatua ya kutoruhusu uendelezwaji wa eneo lolote bila kufanyika upembuzi yakinifu na utafiti wa kisayansi ili kufanya makisio ya athari zinazotarajiwa.

“Mfano ukienda Sweden ukaenda Italia unakuta nyumba zimejengwa juu ya mito na mikondo ya maji, mtu anaingia kwake kwa boti si teknolojia tu, sayansi imepewa nafasi yake,” anaeleza.

Mbinu kuwang’oa wa bondeni

Mwanazuoni huyo aliyebobea katika taaluma ya udhibiti wa majanga, anasema mara nyingi Serikali inachukua hatua ya kutaka kuwahamisha wananchi kutoka maeneo hatarishi, lakini haifanikiwi.

Pamoja na kushindikana huko, Dk Kamanyi anasema hakujafanyika tathimini ya kujua kwa nini watu wanaoishi mabondeni au maeneo hatarishi kwa mafuriko wanagoma kuhama wanapoamrishwa na Serikali.

Jawabu la hilo linatokana na utafiti uliowahi kufanywa na Dk Kamanyi na kubaini  wengi wanagoma kuhama kwa hofu ya kutenganishwa na watu waliowazoea.

“Nilibaini watu wengi kwenye maeneo hayo wanaishi kindugu. Akiwa hana kitu ataenda kwa jirani ataomba atapewa, akikosa fedha ataenda kwa jirani atapewa chakula atakula, sasa huyu unapotaka kumhamisha anawaza hivi kwa maisha yangu nitaishije,” anaeleza.

Sababu nyingine anaeleza ni ukaribu na maeneo ya utafutaji, mathalani wakazi wa Jangwani, jijini Dar es Salaam.

“Mtu anakaa Jangwani anajua asubuhi anaenda Kariakoo kwa mguu, anasukuma mkokoteni anapata chochote anarudi kwa mguu nyumbani, familia inapata chakula. Ukimpeleka Mabwepande hatakuelewa, atafikaje Kariakoo?” amehoji Dk Kamanyi.

Uhamishaji wananchi kutoka eneo moja kwenda lingine, Dk Kamanyi anasema unapaswa kuhusisha kuwekwa kwa miundombinu itakayowashawishi na kuwawezesha kuishi ama kama walivyokuwa wanaishi awali au zaidi.

Dk Kamanyi anasisitiza pendekezo lake hilo kwa hoja kuwa, uhamishaji wananchi haupaswi kugubikwa na ahadi hewa bila utekelezaji na kwamba, ndicho kinachofanywa na Serikali.

“Siyo unawapeleka eneo fulani unawatelekeza, Serikali inapaswa kuandaa miundombinu na mazingira yatakayowawezesha kuishi vizuri katika makazi mapya,” anasema Dk Kamanyi.

Miongoni mwa maandalizi anayosema ni muhimu kufanywa kabla ya kuwahamisha wananchi ni ujenzi wa maeneo ya kupata huduma muhimu zikiwamo za afya, elimu, maji, malazi na uchumi.

Amesema hayo yaambatane na kuwajengea barabara na kuruhusu daladala kufanya safari za kwenda kwenye eneo kama hilo ili kurahisisha usafishaji.

Yote hayo anasema yasifanyike kabla ya kuwauliza wananchi wenyewe, waeleze mazingira ambayo wangetamani kuishi kwa utulivu, kisha washawishiwe kulingana na uwezo wa Serikali.

Dk Kamanyi amehoji iliwezekanaje kuwahamisha wananchi wakati wa vijiji vya ujamaa na ishindikane sasa?

Mtazamo huo unashabihiana na kilichoelezwa na Dk Enock Makupa, mtaalamu wa udhibiti wa majanga wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), anayesema utaratibu unaotumika kuwahamisha wananchi ndiyo unaofanya wakubali au wakatae.

Utaratibu sahihi, Dk Makupa anasema unapaswa kuanza kwa kutoa elimu jambo ambalo aghalabu hufanyika, kisha kuwaonyesha makazi mbadala, akifafanua hapo ndipo lilipo tatizo.

“Unakuja Serikali inamfuata mwananchi ikimtaka kuhama kutoka eneo moja kwenda lingine, inamwambia utahamia sehemu fulani nitakupa mabati na tofali, unapomuhamisha umemkuta ameshajenga nyumba, unatarajia atakubali kuhama?” amehoji Dk Makupa.

Anasisitiza tatizo la wananchi kugoma kuhama mabondeni halipo kwao, bali taratibu zinazotumika na Serikali kuwahamisha ndilo tatizo.

“Serikali inapaswa kuandaa eneo na kuweka miundombinu yote muhimu ndipo iende kushawishi wananchi kuhama, huku ikiwaonyesha kwamba mtahamia hapa,” anaeleza Dk Makupa.

Serikali ikubali kugharimia

Ili kufanikisha yote, Dk Makupa anaeleza ni muhimu Serikali ikubali kutumia fedha nyingi katika kukabiliana na mafuriko.

Wakazi wa Dar es Salaam wakisaidiwa kuvushwa katika eneo lililojaa maji. Jangwani. Picha na Maktaba 

Dk Makupa anasema upatikanaji wa fedha unaweza kutokana na kuachana na baadhi ya vipaumbele, kama vile sherehe za kitaifa, badala yake kiasi kilichotengwa kitumike kuandaa mazingira hayo.

Wananchi wanaoishi katika eneo la Bonde la Msimbazi Jijini Dar es Salaam,wakiendelea kubomoa nyumba zao kwa ajili ya kupisha mradi wa uendelezaji wa bonde hilo ili kukabiliana na mafuriko. Picha na Michael Matemanga

Wataalamu watumike

Mwanazuoni huyo anaeleza kunahitajika wataalamu kwa ajili ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu majanga kama hayo, lakini bado hawatumiki kwa kazi hiyo.

“Mara nyingi tunaona yakitokea majanga Serikali inaunda kamati za Bunge, huko wanaenda kutembelea ilhali hawana utaalamu wanaishia kufanya mambo kisiasa, kesho hali inajirudia,” anasema.

Maeneo hatarishi yabainishwe

Kwa mtazamo wa Dk Makupa, ili kupunguza athari za mafuriko ni muhimu Serikali iyabaini maeneo hatarishi kwa janga hilo na yawekwe alama ili wananchi wasiruhusiwe kuishi.

Baadhi ya magari yakiwa yamesimama katika barabara kuu ya Hanang. Picha na Maktaba

“Tukifanya hivyo, mafuriko yakitokea tunapunguza madhara kwa wananchi na mali zao, kwa kuwa hawataishi tena kwenye maeneo hatari, hivyo watakuwa salama,” anasema.

Jambo lingine linalopaswa kufanyika kwa mujibu wa Dk Makupa, ni utolewaji wa elimu kwa wananchi juu ya majanga ya asili na namna ya kuyaepuka.

Hata hivyo, mwanazuoni huyo anaeleza kuwapo changamoto katika mfumo wa utendaji wa kamati za maafa kuanzia ngazi ya Taifa hadi vijiji.

Anasema kamati hizo ndizo zenye jukumu la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majanga, lakini mara nyingi zilizopo ngazi ya vijiji hazijui zifanye nini.

“Wananchi wengi hawana ufahamu na majanga hayo ya kiasili, zile kamati za maafa zilizopo kwenye ngazi za kata zinashindwa kutekeleza majukumu yao kwa kuwa hawajui kazi ya kufanya. Kuna mfumo wa maafa lakini haufanyi kazi,” anasema.

Anapendekeza kuwapo mbinu mpya ya kutoa taarifa ya tahadhari za majanga, mbali na inayotumika sasa kwa maana ya redio, runinga na mitandao ya kijamii.

“Inaonekana bado Tanzania kuna wananchi hawawezi kuvifikia vyanzo hivi vya taarifa, kwa hiyo Serikali itafute mbinu zaidi kuwafikia wananchi wote,” anasema.

Kwa mujibu wa Dk Makupa, ili kuyakabili majanga hayo hatua zinapaswa kuchukuliwa katika msimu wa jua kali, badala ya kusubiri mafuriko ndipo itafutwe mbinu ya kuokoa wananchi.

“Kipindi ambacho hakuna mvua juhudi kubwa zielekezwe kwenye ujenzi wa miundombinu ya kudhibiti mafuriko,” anaeleza.

Kauli ya Serikali

Katika mkutano na waandishi wa habari, Msemaji Mkuu wa Serikali, Matinyi alisema Serikali inatarajia kujenga mabwawa mawili wilayani Rufiji ikiwa ni hatua za muda mrefu za kukabiliana na athari za mafuriko katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa Matinyi, mabwawa hayo mawili yanayojengwa Rufiji ni kati ya 127 ambayo Serikali inatarajia kuyajenga katika mikoa mbalimbali nchini na tayari upembuzi yakinifu umeshafanyika.

Alisema mengine 14 ujenzi wake umeshaanza katika maeneo kadhaa nchini.

"Aprili 20, 2024 Serikali itatangaza zabuni ili kumpata mkandarasi atakayejenga mabwawa hayo 127," alisema  Matinyi.

Rais Samia Suluhu Hassan, Aprili 12, 2024 alisema baada ya mafuriko yanayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini, Serikali inatarajia kufanya tathmini kubaini hatua za kudumu zitakazochukuliwa kukabili au kupunguza kiwango cha athari zake nchini.

Alisema hayo katika hafla ya kumbukizi ya miaka 40 ya hayati Edward Sokoine mkoani Arusha.

“Licha ya kuwa baadhi ya maeneo yaliyoathirika yamekuwa yakikumbwa na mafuriko kwa kujirudia, bado ninaona kuna sehemu kama Serikali tunaweza kuboresha. Ni kweli hatuwezi kuzuia mafuriko moja kwa moja lakini tunao uwezo wa kupunguza athari,” alisema.

Hata hivyo, alisema hatua mbalimbali zimechukuliwa kwa waathirika wa mafuriko, ikiwamo kupeleka misaada ya chakula na dawa, na hifadhi za muda.