Matinyi: Serikali haitatumia nguvu kuhamisha wanachi Rufiji

Mwonekano wa mojawapo ya maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo wilayani Rufiji

Muktasari:

  • Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema wananchi wa wilaya ya Rufiji walipewa taarifa, lakini wengi hawakupenda kuondoka katika maeneo hayo wakidai wamezoea changamoto ya maji kwa miaka yote ya maisha yao.

Dar es Salaam. Kutokana na athari za mafuriko katika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Mobhare Matinyi amesema Serikali haiwezi kutumia nguvu kuwahamisha wananchi walio karibu na Bonde la Mto Rufiji.

Amesema wakazi wa Rufiji kwa muda mrefu wamepewa taarifa juu ya uwepo wa athari hizo na wa mkoa wa Morogoro nao wana taarifa tangu mwaka jana.

Matinyi amesema hayo leo Aprili 12, 2024 wakati akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kufahamu kwa nini Serikali isiwaondoe wananchi hao walioathiriwa na mafuriko katika eneo la Bonde la Rufiji,

msemaji huyo wa Serikali, amesema wananchi wa Rufiji mwaka 2020 walipewa viwanja na sasa wakati wa janga la mafuriko viwanja 600 vimepimwa kugawiwa bure kwa wananchi, ili wahame.

“Wananchi wetu wengine hawapendi kuhama katika kipindi hiki cha mvua, wananchi wengine kwa sababu ya maji mengi kulikuwa na kujisahau pengine huu si mwaka wa mafuriko, hivyo wakasogea eneo karibu na bonde kwa sababu ya kilimo, mazoea na kujiamini,” amesema.

Ameongeza kuwa kuna ugumu wa kuwatoa wananchi, Serikali isingependa kutumia nguvu, bali inachofanya ni  kuwaelimisha  na kuwapa eneo jingine wanaloweza kwenda,” amesema Matinyi, aliyeitisha mkutano huo kuzungumzia hali ya mvua zinazoendelea nchini na mafuriko.

Matinyi amesema wananchi walipewa taarifa juu uwezekano wa maeneo yao kufurika, lakini wengi hawakupenda kuondoka katika maeneo hayo wakidai wamezoea changamoto ya maji kwa miaka yote ya maisha yao.

Kiongozi huyo wa Serikali amesema kutokana na mafuriko wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani, watu wawili wamefariki, wawili wengine katika wilaya ya Kibiti na mmoja wilaya ya Kisarawe.

“Majeruhi wawili wilayani Kibiti na watatu wapo Kisarawe, lakini kuna uharibifu wa mazao mengi ya chakula mahindi, mpunga, ufuta, ndizi mihogo na mtama, makazi ya barabara, makazi, madaraja nguzo ya umeme, shule na kituo cha afya Mhoro Rufiji kimesomwa na maji,” ameeleza Matinyi.

Amesema kata 12 kati ya 13 za wilaya ya Rufiji na kata tano kati ya 13 za wilaya ya Kibiti na kata moja ya Kisarawe zimeathiriwa.

Kwa takwimu za watu waliokumbana na majanga, Matinyi amesema 1,014 wameokolewa katika wilaya ya Rufiji pekee.


Bwawa la Mwalimu Nyerere na mafuriko

Akitoa historia ya Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, Matinyi amesema bonde hilo limekuwa na historia ya mafuriko na Serikali kutokana na hali hiyo ibuni mradi wa kuyatumia maji kuzuia mafuriko.

“Mwaka 2019 ujenzi wa bwawa ulianza na sasa upo asilimia 98 ukiwa vinu tisa vya kuzalisha umeme wa megawati 2115, bwawa hilo lina uwezo wa kuhifadhi maji lita za ujazo bilioni 32.782,”amesema.

Matinyi amesema Machi mwaka huu bwawa hilo lilisaidia kukusanya maji ambayo kwa kiasi kikubwa yangevamia makazi ya wananchi ambapo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lilitangaza rasmi maji ndani ya bwawa kufikia kima chake.

Amesema mvua kubwa za El nino zilikuwa zinapitisha maji kufikia mita za ujazo 8,445 kwa sekunde, hivyo bwawa lilipofikisha kima kilichotakiwa kilipaswa kuruhusu maji kuendelea na safari yake.

“Tangu Oktoba bwawa hilo lilikuwa linahifadhi maji na kufikia Machi lilijaa. Bahati ya maji kuhifadhiwa ambayo yangeleta maafa tangu Oktoba yalifikia mwisho,” amesema.

Matinyi amesema wingi wa maji hayo hayafikii maji yaliyopita mwaka 1974 ambayo ni mita za ujazo 13,212 kwa sekunde wakati bwawa bado halijajengwa


“Nidokeze mwaka 2020  mita za ujazo 7,144 kwa sekunde zilikuwa zinapita kwenye bwawa hilo sasa 8,445 ndio zinapita zimeachana kidogo tu,” amesema na kuongeza kuwa kwa kuzingatia athari hizo, bwawa hilo lilijengwa kuzuia mafuriko na baada ya kukusanya maji mengi uwezekano ulipungua.


Tanesco kuruhusu maji

Matinyi amebainisha kuwa hatua ya kufungulia maji kwenye bwawa la Nyerere vipimo vya kitaalamu vilitumika ambapo Februari mwaka huu, Tanesco imekuwa ikiruhusu maji lita za ujazo 3,000 hadi 6,000.

“Kuna wakati imefikia ujazo 7,000 maana yake ni nini tusingekuwa na hii bwawa mafuriko yangeanza kutusumbua eneo la bonge la Rufiji ingetusumbua kuanzia Oktaba mwaka jana,” amesema.

Msemaji huyo wa Serikali ameongeza kuwa “Tulipita Novemba, Desemba, Januari, Februari na kwa kuwa mvua ziliendelea kama Mamlaka ya Hali ya Hwa Tanzania (TMA) ilivyotabiri na maji yalikuwa mengi, hivyo Shirika la Umme Tanzania (Tanesco) likachukua tahadhari likawataarifu mamlaka,” ameongeza.

Kinachoendelea sasa, Matinyi amesema bwawa limefikia ukomo wake wa kuchukua maji na yaliyobaki yanaendelea na safari yake kwenda baharini na ni maji mengi isiyo ya kawaida.

“Kwa kawaida mto Rufiji unapokuwa kwenye mvua za kawaida mita za ujazo ni 1400, 1500 kwa sekunde lakini sasa ni zaidi ya mita za ujazo.

Amesema hisia kwamba Bwawa la Julius Nyerere limesababisha mafuriko si za kweli, kwani bwawa hilo limechelewesha mafuriko ambayo yangetokea Oktaba mwaka jana.

Matinyi amesema bwawa hilo limesaidia upatikanaji wa taarifa za haraka za mafuriko kutoka Tanesco ya watu kujiandaa.aaaaaa