Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bomu la nyaya katika majengo

Muktasari:

  • Wananchi wazungumzia wanayopitia, huku wataalamu wakitoa ushauri wa nini cha kufanya, kuondoa nyaya zinazoning’inia mitaani.

Dar es Salaam. Mbali ya Kariakoo kuwa eneo lenye msongamano wa watu na vyombo vya moto kutokana na biashara zinazofanyika, kuna utandazaji holela wa nyaya zikiwamo za umeme, hali inayotishia usalama.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika mitaa ya Kariakoo ikiwamo ya Nyamwezi, Mchikichi, Muhonda, Congo, Magila na Narung’ombe umebaini uwepo wa nyaya hizo ambazo si mali ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Nyingi huwekwa ili kuunganisha mifumo ya kimtandao kwenye maduka ikiwamo kamera za usalama (CCTV) na zile za inteneti (Fiber).

Baadhi ya nyaya hizo zimeunganishwa moja kwa moja kwenye nguzo za umeme za Tanesco bila kutenganishwa au kupitishwa kwenye miundombinu yake, huku zingine zikiwa jirani na miundombinu ya shirika hilo na majengo.

Zipo pia nyaya zinazoning’inia, huku zingine zikipita juu ya bati hivyo kuhatarisha usalama wa watu na mali zao pale utakapozuka moto kwa kuwa ni rahisi kuenea kwa haraka katika majengo mengine ambayo yamesongamana.

Si hivyo pekee, kwa mazingira ya Kariakoo hakuna njia za dharura za kupita hivyo kuongeza hatari.


Wasemavyo wananchi

Japhari Mzalendo, mfanyabiashara katika Mtaa wa Nyamwezi na Mchikichi, anasema hitilafu ya umeme ni jambo la kawaida Kariakoo kutokana na ukiukwaji wa taratibu za ujenzi.

“Mamlaka zinazotoa vibali vya ujenzi zinapaswa kufuatilia kwa karibu. Wapo wanaoomba kibali cha kukarabati au kujenga kitu kimoja, lakini wanatekeleza kingine tofauti. Hii imekuwa chanzo kikubwa cha ‘short circuit’ (hitilafu ya mzunguko wa umeme) zinazoleta ajali za moto,” anasema.

Rehema Rajab, mfanyabiashara wa vijora Mtaa wa Nyamwezi anasema mlundikano wa nyaya ni tatizo, si tu kwa usalama pia usumbufu katika shughuli zao.

“Hivi karibuni jirani yangu alikumbwa na moto uliotokana na cheche za umeme, bahati nzuri tuliuzima kwa haraka kabla haujaleta madhara makubwa,” anasema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kariakoo Magharibi, Said Omary anasema nyaya zilizotandazwa kiholela katika mtaa huo, hususani za kamera za CCTV na ving’amuzi zimekuwa zikichochea majanga ya moto hitilafu ya umeme inapotokea.

“Siku si nyingi Mtaa wa Mchikichi na Swahili, ghorofa liliwaka moto. Tatizo likazidi kuwa kubwa kwa sababu kulikuwa na nyaya nyingi zilizotundikwa juu ya geti la jengo. Moto uliendelea kushika kasi kutokana na nyaya hizo,” anasema.

Anasema Tanesco limeanza kuchukua hatua kwa kuondoa nyaya zilizo wazi katika maeneo ya Kariakoo ili kupunguza hatari ya ajali zinazotokana na hitilafu ya umeme.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Severin Mushi anasema kutapakaa kwa nyaya ni tatizo na wamekuwa wakifanya mazungumzo na Tanesco kulitatua.

“Tumeshaongea na mamlaka husika ya umeme kwa sababu nyaya nyingine hazitoi moto na ufungwaji wake umekuwa ni hatari kwa jamii na wafanyabiashara,” anasema.

Anasema kuna haja ya kukaa kikao kingine kujadili jambo hilo ili kuepuka madhara makubwa zaidi.


Jeshi la Zimamoto

Moja ya majukumu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa mujibu wa Sheria ya Zimamoto ya mwaka 2007, Sura ya 426 ni kusimamia ujenzi wa majengo ya makazi na biashara kabla ya kuanza ujenzi au ukarabati wake.

Kamanda wa jeshi hilo Mkoa wa Ilala, Peter Mabusi anasema wananchi hawazingatii utaratibu huo, jambo linalochangia ajali za moto na kusababisha uokoaji kuwa mgumu zaidi.

Anasema moja ya changamoto wanazokumbana nazo katika uokoaji ni muingiliano wa miundombinu ya umeme na majengo kujengwa kwa ukaribu.

“Kisheria, umbali kati ya jengo na jengo haupaswi kuwa chini ya mita 2.5. Lakini ukienda maeneo mengi ya mjini, hususani Kariakoo, majengo yamegusana kabisa,” anasema.

Anasema hali hiyo inatokana na kutokuwapo ufuatiliaji wa karibu katika hatua za awali za ujenzi na miundombinu ya umeme kuwa chini, hali inayowapa ugumu wanapokwenda kuzima moto au kufanya uokoaji.

“Watu wanajenga bila kufuata utaratibu, kwani hakuna mtu anayepaswa kujenga au kukarabati jengo bila kupata kibali kutoka Zimamoto, tunapitia ramani ya ujenzi na kutoa ushauri wa kiusalama ili kuepusha majanga,” anasema Kamanda Mabusi.

Anasema ili kuepuka usumbufu wa kwenda ofisi za Zimamoto wamesogeza huduma katika halmashauri zote kwa gharama ya Sh30,000 kutoka Sh300,000 za awali.

Kamanda Mabusi anasema wakati umefika kwa mamlaka husika kuanza kuweka miundombinu ya umeme chini ya ardhi badala ya juu ili kupunguza hatari za moto na kurahisisha shughuli za uokoaji.

“Tunapoendelea kukua kiteknolojia, tunahitaji pia kuhakikisha nyaya zinapitishwa chini ya ardhi. Hii itasaidia katika usalama na kuzuia miguso isiyo salama kati ya nyaya na majengo,” anasema.

Anasema licha ya hitilafu ndogondogo za umeme kama vile transifoma kulipuka au nyaya kugusana, bado kuna matumizi mabaya ya vifaa vya umeme kwenye nyumba nyingi na kuwa chanzo cha moto.

“Watu wanatumia vifaa vya umeme, halafu hawazimi joto linapoongezeka linasababisha moto, pia wengine wana nyaya za zamani au waliweka bila wataalamu, nyaya zimebaki wazi, ni hatari kubwa,” anasema.

Kamanda Mabusi anatoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanawatumia mafundi wenye weledi kusambaza umeme majumbani, kufuata sheria na kupata vibali vya ujenzi kutoka zimamoto kabla ya kuanza kazi yoyote ya ujenzi.


Mtaalamu wa ujenzi

Mhadhiri katika Chuo Kikuu Ardhi, Profesa Geraldine Kikwasianasema mtu yeyote anayejenga ni lazima awasiliane na mamlaka ya miundombinu inayopita, ikiwamo ya umeme na maji.

“Yeyote anayejenga akiona nguzo ya umeme hatakiwi kuigusa bali anachotakiwa kufanya ni kuwasiliana na Tanesco ambao wataangalia kama watatakiwa kuihamisha moja kwa moja au kwa muda,” anasema.

Anasema wakiona inafaa kuhamisha wanatoa gharama ili mjenzi aendelee na shughuli zake. Hata hivyo, anasema hilo halifanyiki badala yake wanaofanya hivyo ni vishoka.

Kutokana na uchache wa rasilimali watu, anasema ufuatiliaji umekuwa hafifu japokuwa kwa sasa wamekuwa wakipokea taarifa kwa haraka baada ya kutengenezwa makundi ya Whatsapp.


Kauli ya Tanesco

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange anasema kuna utaratibu mahususi wa kushirikiana na taasisi nyingine kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi kwa usalama na ufanisi.

“Kwa mujibu wa sheria, hairuhusiwi taasisi kuingilia miundombinu ya umeme bila kushirikiana nasi. Kuna utaratibu tumekubaliana na taasisi mbalimbali kama vile TTCL, kuhakikisha shughuli zao haziathiri mfumo wa umeme wala kuhatarisha maisha ya wananchi,” anasema.

Akizungumzia hali ya Kariakoo, anasema inakabiliwa na changamoto ya miundombinu kutokana na wingi wa huduma zinazotolewa katika eneo hilo maarufu kwa biashara.

“Eneo la Kariakoo lina shughuli nyingi za kibiashara, hivyo mahitaji ya umeme ni makubwa. Wingi wa nyaya unaoonekana ni kwa sababu ya huduma zinazotakiwa na wafanyabiashara katika eneo hilo, ambazo ni muhimu kwao,” anasema.

Twange anasema Tanesco itaendelea kushirikiana na uongozi wa Kariakoo na taasisi nyingine ili kupata suluhisho la pamoja kuhusu changamoto zilizopo.

“Tutaendelea kufanyia kazi maeneo yote yenye changamoto na kwa kushirikiana na viongozi wa maeneo husika na kampuni nyingine, tunaamini tutafikia muafaka unaowanufaisha wananchi wote,” anasema.


Mipango Miji

Idara ya Ardhi na Mipango Miji Jiji la Dar es Salaam imeonya kuhusu kasi ya ujenzi holela unaogusa miundombinu ya umeme.

Mkuu wa idara hiyo, Maduhu Ilanga anasema licha ya jiji kuwa na utaratibu wa kutoa vibali vya ujenzi kwa mujibu wa sheria, baadhi ya wananchi wamekuwa wakijenga bila vibali wala kufuata miongozo ya kitaalamu, hali inayoathiri miundombinu ya umeme, maji na barabara.

“Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya mwaka 2007 inataka kila aliye na mpango wa ujenzi kupata kibali na kufuata michoro iliyoidhinishwa, lakini wananchi wengi hawafanyi hivyo. Wengi wanajenga bila kupimiwa maeneo, wanajenga kwenye njia za umeme na hii ni hatari kubwa,” anasema.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Ilanga anasema wameanzisha kitengo maalumu cha Development Control (Udhibiti wa Maendeleo ya Ujenzi), ambacho kazi yake ni kufuatilia miradi yote ya ujenzi kuona kama inafuata sheria ya mipango miji na kukagua utekelezaji wa vibali vilivyotolewa.

Anasema wameanza kushirikiana na sekta binafsi wakiwamo wachora ramani na wakadiriaji majenzi ili kuhakikisha wanasimamia kwa karibu miradi ya ujenzi na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wananchi kabla ya kuanza ujenzi.

“Hatuwezi kukabiliana na changamoto hii kwa kutumia Serikali pekee, tumeamua kushirikisha sekta binafsi kwa kupata njia mpya katika kuwezesha ujenzi rafiki,” anasema.

Kwa maeneo ya Kariakoo, Ilanga anasema nyumba nyingi hazikupangwa kuwa maduka, lakini wamiliki wameongeza ngazi za nje ili kufikia sehemu za juu walizogeuza maduka.

“Changamoto ni kubwa kuna viwanja vimejengwa vyote hadi kukosa njia ya kupita. Kutokana na Serikali kuliona hilo iliundwa timu maalumu kupita maeneo haya na wataleta mapendekezo ili hatua zichukuliwe,” anasema.


Mtazamo wa mtaalamu

Mtaalamu wa umeme, Josephine Mutashobya anasema nyaya nyingi zinazotumika kwenye nyumba na taasisi za umma huwa zinachakaa, hali inayosababisha kinga ya waya (insulation) kuharibika na hatimaye kuleta mgusano kati ya nyaya.

“Nyaya za umeme huwa zinachoka kutokana na mabadiliko ya joto, hii inasababisha insulation ya waya kuchakaa na unapokuwa worn (umeharibika) kuna uwezekano mkubwa wa mgusano kati ya waya na waya, husababisha shoti na moto kuwaka,” anasema.

Anasema hali hiyo ni hatari zaidi kwenye maeneo yenye msongamano mkubwa wa makazi, ambako nyumba zimejengwa karibu na nguzo au nyaya za umeme.

Kwa mujibu wa viwango vya kimataifa vya usalama wa umeme (kama IEC na IEEE) na miongozo ya mamlaka za usambazaji umeme nchini, kuna umbali maalumu wa usalama kati ya jengo na nyaya kulingana na kiwango cha msongo wa umeme.

Anasema kwa nyaya za msongo wa chini, jengo linatakiwa kuwa angalau mita 1.5 hadi 2.0 kutoka kwenye nyaya au nguzo ya umeme, huku kwa msongo wa kati ni mita 3.0 hadi 4.0. Kwa nyaya za msongo wa juu, umbali salama unaweza kufikia mita 6.0 au zaidi.

Hata hivyo, changamoto iliyopo anasema ni namna baadhi ya miji na mitaa imejengwa bila mpango, hali inayolazimisha mamlaka za umeme kusambaza huduma hiyo kwa kuzingatia mazingira yaliyopo hata kama hayakidhi viwango vya usalama.

“Ukweli ni kwamba kuna maeneo umeme umefika kutokana na uhitaji mkubwa lakini mazingira yake si salama, hivyo kuna haja ya ukaguzi wa mara kwa mara na kutoa elimu kwa wananchi,” anasema.

Kuhusu hatari zinazoweza kutokea endapo viwango vya umbali havitazingatiwa, anasema ni mshtuko wa umeme kwa watu wanaoishi jirani, moto, uharibifu wa nyaya, usumbufu wa huduma za umeme na hatari kwa mafundi wa Tanesco au kampuni binafsi wanapofanya matengenezo.


Nini kifanyike

Mutashobya anasema kwa maeneo yenye nafasi finyu, nyaya huwekwa chini ardhini, lakini gharama yake ni kubwa na matengenezo huhitaji utaalamu wa hali ya juu.

“Ni suluhisho ambalo linaweza kusaidia, lakini gharama yake ni kubwa mno. Wateja wachache tu wanaweza kumudu ndiyo maana ni muhimu zaidi kuhakikisha miundombinu iliyopo angalau inakaguliwa mara kwa mara,” anasema.

Anatoa wito kwa mamlaka husika kuwekeza zaidi kwenye ukaguzi na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu hatari zinazotokana na kuishi karibu na nyaya za umeme, huku akisisitiza ushirikiano na wananchi.

Anasema wananchi wanatakiwa kuwa wa kwanza kutoa taarifa pindi wanapoona nyaya zimelegea, zimeshika paa au kuna mabadiliko kwenye nguzo jirani. Wasingoje madhara yatokee ndipo watoe taarifa.