Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utunzaji ngozi kwa wanaume wazua mjadala

Muktasari:

  • Ngozi ya wanaume kwa kawaida huwa na mafuta zaidi na ni nene kidogo kuliko ya wanawake, lakini bado hukumbwa na matatizo kama vile chunusi, ukavu, kuungua na jua, au uzee wa mapema.

Dar es Salaam. Kwa miongo kadhaa, huduma ya ngozi maarufu ‘skincare’ ilionekana kama jambo la wanawake, ikiambatana na watu maarufu, watu wa mitandao ya kijamii na wanamitindo wa urembo. Lakini mtazamo huo kwa sasa unabadilika.

Idadi inayoongezeka ya vijana wa kiume, hususan wa kizazi cha Gen Z, sasa wanahusudu huduma ya ngozi kama sehemu ya kawaida ya usafi binafsi na kujitunza.

“Ngozi yenye afya ni kama usafi wa kawaida kama kupiga mswaki au kubadili soksi,” anasema Jumanne Isiah, mfanyabiashara kutoka Tabata. “Tuwe wakweli, vumbi, jua, moshi wa bodaboda, msongo wa mawazo na jasho, ngozi yako inapitia mambo mengi sana kila siku.”

Isiah anakanusha mawazo kuwa huduma ya ngozi ni dalili ya ubatili. “Ni suala la afya, kujiamini na heshima.”

“Kutunza ngozi yako hakupunguzi uanaume wako. Lakini kuipuuza? Kunaweza kukugharimu mvuto na haiba yako.”

Kwa Joseph Samwel, mhudumu wa benki jijini Dar es Salaam, anasema msukumo wa kuanza kutunza ngozi yake ulitoka kwa mpenzi wake.

“Nilianza kutumia losheni ya kulainisha ngozi kwa sababu mpenzi wangu aliniambia naonekana kama nazi iliyochoka.

“Mwanzoni nilihofia watu watasema nini. Lakini baadaye ofisi nzima ikaanza kuniuliza natumia nini.”

Vijana wengi wa kiume hukua wakiambiwa kuwa ‘wanaume wa kweli’ wanapaswa kuonekana wamekauka, kana kwamba ngozi kavu ni ishara ya nguvu.

“Ninapenda kuonekana msafi, lakini nafanya kwa kificho,” amesema Brian Lucas, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kwa upande mwingine mbunifu wa picha, Daniel Sebastian, anasema kutunza ngozi ni sehemu ya nidhamu binafsi. “Nguvu ya kweli ni pamoja na mwonekano, huwezi kutengeneza ubunifu mzuri halafu unatembea na ngozi iliyoharibika, haiingii akilini.”

Lucy Jackson, mfanyabiashara kutoka Sinza anasema ngozi yenye afya haina jinsia. “Haijalishi kama wewe ni mwanaume au mwanamke, ngozi ya kila mtu hukusanya uchafu, mafuta na kuharibiwa na jua.”

Anaongeza kama mwanaume anaweza kutunza gari lake, viatu vyake vya michezo na ndevu zake, kwa nini asiitunze ngozi yake? “Uanaume siyo kuwa mchafu, ni kuonekana nadhifu na kujitunza,” anasema.

Mkazi wa Katoro, Mkoa wa Geita, Masumbuko Joseph anasema: “Ngozi ya mwanaume inapaswa kuwa kiume ume, siyo inakuwa lainilaini. Kwa hiyo mimi siwezi kufanya mambo hayo kwanza hata mke wangu hawezi kunielewa. Yaani niwe laini kweli?.”

“Tena wakati mwingine huwa nasahau kupaka kabisa mafuta, na huwa napaka nikivaa pensi lakini nikiwa navaa suruali hata mwezi sipaki na wala sijali,” anasema.

Mhudumu wa nyumba ya kulala wageni jijini Dodoma, Mariam Abdallah anasema nina uzoefu wa miaka 10 kwenye hii kazi lakini naweza kusema asilimia 80 ya wateja wanaume wanaokuja kulala huwa hawana mafuta wala vitana vya kuchania nywele.

“Asubuhi ikifika wanaume wengi sana huulizia mafuta na vitana. Kwa hiyo hilo la wanaume kutunza ngozi, lipo kwa wachache wengi wao hawapaki mafuta na wakiomba hupaka kwenue viganja vya mikono pekee,” anasema Mariam.

Alichokisema daktari

Akizungumzia hilo, Dk Magnus Msango amesisitiza kutunza ngozi ni muhimu kwa wanaume sawa na ilivyo kwa wanawake.

“Tunapozungumzia huduma ya ngozi, tunazungumzia kujitunza na kuilinda ngozi yako.”

“Kwa wanawake, huduma ya ngozi imezoeleka. Lakini kwa wanaume, bado inaonekana ni jambo lisilofaa. Huo ni mtazamo potofu,” anaongeza.

Anaeleza kuwa wanaume wengi hupuuzia huduma ya ngozi kwa kuogopa kuonekana kama si wanaume wa kweli. “Kama mwanaume, unapaswa kuitunza ngozi yako kama unavyotunza afya ya mwili wako.

 “Kutunza ngozi yako kunasaidia kuimarisha afya na mwonekano wako.”

Dk Msango pia anaeleza lishe bora ina mchango mkubwa katika afya ya ngozi.

“Lishe yenye matunda na mboga za majani inaweza kuzuia uharibifu unaosababisha ngozi kuzeeka mapema.” anasema.

Anaongeza ni vyema kuepuka vyakula vyenye sukari nyingi, vitafunwa vilivyosindikwa na wanga uliokobolewa. Pia anasisitiza umuhimu wa kunywa maji mengi ili kuilainisha ngozi kutoka ndani.

Kwa kuwa mitazamo inaanza kubadilika polepole, wanaume wengi sasa wanaelewa kuwa huduma ya ngozi siyo kuhusu kuonekana ‘mwororo’ bali kuwa na afya, kujiamini na kuwa nadhifu.

Umuhimu kwa wanaume

Kwa mujibu wa mtandao wa menshealth.com, huduma ya ngozi si urembo au suala la jinsia, bali ni sehemu ya afya ya mwili. Wanaume wanapopaswa kujali ngozi yao kama sehemu ya usafi wa kila siku na kujitunza.

Umuhimu huu ni mkubwa, unagusa afya ya ngozi, mwonekano wa nje na hata kujiamini, kwani humsaidia mwanaume kudumisha afya ya ngozi kama ilivyo kwa mwanamke, huhitaji usafi, unyevu na ulinzi dhidi ya mionzi ya jua na uchafu.

“Huduma ya ngozi husaidia kuondoa uchafu, mafuta na vumbi vinavyoweza kuziba vinyweleo. Kuzuia magonjwa ya ngozi kama chunuzi, mba na upele na huhifadhi unyevu asilimia wa ngozi, pia humsaidia mwanaume kuzuia kuzeeka mapema,” unaeleza mtandao huo.

Mwanaume anayeitunza ngozi yake kwa kutumia bidhaa zenye viambato vya kulinda dhidi ya jua na zile zenye antioxidants, husaidia kupunguza mikunjo ya uso, kulinda ngozi dhidi ya miale hatari ya jua inayoharakisha uzee wa ngozi na kudumisha ngozi kuwa laini na yenye afya.

Pia ina faida zaidi kwake kwani humwongezea kujiamini na kuonekana bora. Ngozi safi na yenye afya huongeza kiwango cha kujiamini, mwanaume anayejali ngozi yake huonekana nadhifu, aliyejitunza na ni muhimu kwake hasa kazini au mahusiano ya kijamii na kimapenzi.

Hata hivyo, wanaeleza kuwa utofauti wa ngozi ya mwanaume huwa na mafuta mengi zaidi na ngozi ngumu, hivyo inahitaji huduma ya kipekee kulingana na aina ya ngozi kwa mfano, wanaume wengi hupata chunusi au harara kwa sababu ya ngozi ya mafuta na ndevu.