Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia: Tunataka amani na utulivu

Muktasari:

  • Agusia ripoti ya amani, ataka makundi ya wagombea yavunjwe baada ya matokeo. Azindua hema Kanisa la Mwamposa, maombi maalumu yafanyika.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema sifa njema kuhusu utulivu na amani iliyopo Tanzania iendelezwe katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Amesema hayo leo, Julai 5, 2025, alipozindua hema (jengo la ibada) la Kanisa la Arise and Shine Tanzania linaloongozwa na Mtume Boniface Mwamposa, Kawe jijini Dar es Salaam, akigusia sifa hiyo kama ilivyoainishwa katika ripoti ya hivi karibuni ya Global Peace Index (GPI) iliyotolewa na Taasisi ya Uchumi na Amani (Institute for Economics and Peace – IEP).

"Zaidi ya yote niwaombe tuendelee kuliombea Taifa letu ili lidumu katika umoja, amani, utulivu na mshikamano kama tulivyo," amesema na kuongeza:

"Habari njema ni kwamba jana (Julai 4) nilisoma mtandaoni na leo msaidizi wangu alikuwa ananionyesha kwamba kumefanyika tathmini huko na Tanzania ndiyo nchi ya kwanza ndani ya Afrika Mashariki kwa utulivu na amani."

Kutokana na hilo amesema: "Sasa hii ni sifa njema na niwaombe wote tunapoelekea kwenye jambo kubwa lile (Uchaguzi Mkuu), demokrasia ya nchi twende tuweke utulivu, amani, umoja na mshikamano wetu."

"Najua katika jambo lile makundi ni mengi, jana (Julai 4) nilikuwa nasoma taarifa za chama changu (CCM) wananiambia waliochukua (fomu kutia nia) nafasi za ubunge ni karibu 4,000 na kitu. Waliochukua nafasi za udiwani ni 30,000 na mamia juu. Sasa hapo ni makundi mengi kweli kweli," amesema na kuongeza:

"Lakini tukimaliza shughuli za mchujo wote tunarudi tunakuwa kitu kimoja na tunakwenda kwa pamoja katika lile jambo kubwa. Kwa hiyo makundi yote yale ni waumini wenu, niwaombe sana maaskofu, wachungaji na viongozi wa dini kusema na waumini."

Amesema katika kipindi kuelekea uchaguzi kutakuwa na makundi lakini watakaopata bahati ya Mungu wakachaguliwa wakapelekwa mbele, makundi yarudi kuwa kitu kimoja.

"Tanzania iwe moja ili twende mbele tukakabili jambo letu kwa umoja. Niwaombe sana viongozi wa dini tusaidieni hilo," amesema.


Kuhusu ripoti

Katika ripoti hiyo, Tanzania imetajwa kuwa nchi yenye amani zaidi Afrika Mashariki kwa mwaka 2025.

Katika viwango hivyo vya mwaka huu, Tanzania imeshika nafasi ya 73 kati ya nchi 163 zilizopimwa duniani, na kuongoza ukanda wa Afrika Mashariki mbele ya Rwanda (91), Uganda (113), Kenya (127), Burundi (133), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (160) na Sudan Kusini (161).

Ripoti hiyo, ambayo huchapishwa kila mwaka na IEP yenye makao yake makuu Sydney, Australia, hupima hali ya amani duniani kwa kutumia viashiria 23, ikiwemo usalama wa kijamii, kiwango cha migogoro ya ndani na ya kimataifa na hali ya kijeshi katika nchi husika.

Licha ya kushuka kwa nafasi nane kutoka nafasi ya 65 mwaka 2024, Tanzania inaendelea kushikilia sifa yake kama mojawapo ya mataifa tulivu zaidi barani Afrika, huku ikiongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa miongo kadhaa Tanzania imekuwa ikisifika kwa ustahimilivu wa kisiasa, mshikamano wa kijamii na utulivu wa ndani usiotetereka sana hata wakati wa misukosuko ya kisiasa au kiusalama inayolikumba eneo la Maziwa Makuu na Pembe ya Afrika.


Kuzingatia maadili

Rais Samia katika hotuba yake ya takribani dakika 20 mbele ya maelfu ya waumini wa kanisa hilo na wageni wengine waalikwa, amesema Mungu ameshusha dini ziwe miongozo kwenye maisha na kwamba, zote zina miongozo ya kuendesha maisha ya mwanadamu.

"Ni imani yangu hema hili litatumika kujenga jamii yenye maadili na hofu ya Mungu kama tunavyoendelea kufanya. Kupitia hofu ya Mungu ndipo mwanadamu anasimama kuwa mtu wa Mungu. Usipokuwa na hofu ya Mungu unakuwa mnywadamu. Hema hili liendelee kufanya kazi hiyo kwa Watanzania wengi," amesema.

Samia amesema jitihada za kujenga maadili zimevuka mipaka ya Tanzania ndiyo maana raia wa China aliyetoka kwao ameungana na kanisa hilo kujenga hema hilo.

"Nasema haya nikijua kwamba dunia inabadilika sana tena kwa haraka, kichocheo ni Tehama, kwa mazuri na kwa mabaya ni muhimu kutumia teknolojia kwa tahadhari ili tuwakinge vijana na maporomoko ya maadili. Tuitumie kufikia malengo ya kujipatia maarifa na kujiendeleza," amesema.

Amelipongeza kanisa hilo kwa kutumia teknolojia kupitia runinga na redio kusambaza elimu ya dini, neno la Mungu na maadili mema kwani wapo ambao kutokana na sababu mbalimbali hawawezi kufika maeneo ya kuabudia.

Samia amesema Serikali inaendelea kuunga mkono taasisi za dini na ndiyo mwelekeo wake.

"Ndiyo maana mnaona tunakwenda sambamba na taasisi za dini ili tuwe na jamii yenye amani," amesema.

Amesema kwa nyakati tofauti taasisi hizo zinaguswa na madhila yanayowafika watu.

"Natoa shukrani kwa taasisi zinazoshughulikia matatizo ya jamii na kufanya kazi na jamii ni utumishi wa Mungu na wenye maana mbele ya Mungu, mnapofanya Mungu naye anashusha neema zake," amesema na kuongeza:

"Niwahakikishieni niko pamoja nanyi na taasisi zote za dini, Serikali hutoa msamaha kwa anayepokea ila wanasema hakuna 'free lunch' inapotolewa kuna mahali fedha imetolewa," amesema.


Urais kazi

Awali, Jakaya Kikwete, Rais mstaafu wa awamu ya nne baada ya kukaribishwa na Samia kuzungumza amewashukuru maaskofu kwa maombi waliyofanya kwa Rais akisema kazi ya urais ni kubwa kwani ameifanya, hivyo anajua.

"Ina changamoto nyingi lakini wakati wote ukipata wenzako wanakuombea ndipo unapata nguvu ya kukabiliana na changamoto zilizopo, mmefanya jambo kubwa sana, ninyi mmezoea mnaweza kuona ndogo. Ila kuongoza Taifa lenye watu milioni 61 ni kazi kubwa, endeleeni kuliombea Taifa liendelee kuwa na amani na utulivu. Mwenye jicho baya kama mlivyosema asipate nafasi," amesema.


Ombi kwa Rais

Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Calvary Assemblies of God (CAG), Askofu Dunstan Maboya amemuomba Rais Samia kuwashirikisha viongozi wa dini yanapotokea mambo magumu yanayohusu dini ya Kikristo.

Amesema kwa kufanya hivyo mambo hayo magumu yanaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kuwa viongozi wameendelea kudhihirisha kuwa licha ya kuwa Serikali haina dini ila Watanzania wana dini.

Askofu Maboya amemtaka Rais Samia kuendeleza ustahimilivu kwa kile alichoeleza ana jukumu gumu la kuongoza nchi yenye watu wenye mawazo na mitazamo tofauti.

"Kuongoza watu milioni 60 inahitaji neema ya ulinzi wa maombi. Kazi unayoifanya ni ngumu na nzito, unahitaji jicho la kuona mbele na linapatikana kwenye maombi. Unahitaji msaada wa Mungu katika kazi unayofanya," amesema na kuongeza:

"Kanisa halitaacha kuliombea Taifa na watawala ili nchi yetu iendelee kuwa na amani. Kama watawala hawatawekwa mikononi mwa Bwana ni rahisi adui kuingia. Hatuna ugomvi na dhehebu lolote wala mtu yeyote zaidi ya kuwahamasisha Watanzania kufanya kazi, kwa kuwa tunaamini asiyefanya kazi asile. Tunasisitiza watu kulipa kodi kwa kuwa ndiyo msingi wa maendeleo."

Akisoma risala, Askofu Mpeli Mwaisumbe wa kanisa hilo lililoanzishwa mwaka 2010 kwa lengo la kutoa huduma za kiroho kwa jamii amesema walijiwekea lengo la kujenga hema hilo ambalo kwa sasa ujenzi wake umefanyika kwa awamu ya kwanza.

"Tulianza kujenga Juni 2024 na awamu ya kwanza ya ujenzi imekamilika Julai 2025. Itakapokamilika awamu ya pili, jumla ya gharama za ujenzi itakuwa Sh15 bilioni ambazo ni fedha za sadaka.

"Tunakushukuru pia Rais kwa upendo wako kwetu, ujenzi wa kanisa hili una mchango wa sadaka yako uliyoiwasilisha kwetu kupitia mkuu wa mkoa kwa kuagiza kanisa letu lisisumbuliwe tunapomuabudu Mungu katika eneo hili," amesema.

Amemuomba Rais Samia aridhie kulitoa eneo hilo ambalo liko chini ya umiliki wa Serikali kuwa eneo lao la kudumu ili wawe na sehemu ya uhakika ya kuabudu.

Ombi hilo pia limetolewa na mtumishi mwingine wa Mungu, Tony Kapola aliyeomba eneo hilo la Kawe liachwe kuwa sehemu ya ibada ya Kanisa la Arise and Shine.

Rais Samia akijibu ombi hilo akisema amelichukua, atakwenda kulifanyia kazi.